Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvua zaleta balaa shughuli zasimama

Mwendesha bodaboda na watembea kwa miguu wakitafakari namna ya kukatisha katika eneo lililofurika maji jirani na stesheni ya mabasi yaendayo haraka (Udart), Jagwani jijini Dar es Salaam kufuatia mvua zilizoendelea kunyesha jana. Picha na Michael Matemanga

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha zinaleta adha kwa wakazi wa jijini hapa na kusababisha baadhi ya shughuli kusimama.

Licha ya kuchimbwa kwa baadhi ya mito, ikiwepo ule wa Msimbazi na Mbezi, bado maeneo yanayozunguka mito hiyo hujaa maji kutokana na takataka.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Oktoba 31 mwaka huu ilitabiri kuwepo kwa mvua za vuli mwanzoni mwa Novemba hadi Desemba.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, wakazi hao walisema mvua hizo zimesimamisha baadhi ya shughuli zao.

“Sisi wakazi wa bondeni hatuwezi kutoka tukihofia nyumba kujaa maji na kusababisha madhara,” alisema Khadija Ali, mkazi wa Kawe Mnarani.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Amos Kazikazi, mbeba mchanga katika eneo la mto Mbezi aliyesema kwa sasa wanakaa macho kuhofia maji yanayoendelea kujaa na kusogelea makazi ya watu. “Tangu asubuhi nabeba mchanga kupeleka kwenye nyumba za huko juu, hapa natembea kwa tahadhari kuhofia kudondoka, napata fedha lakini nahatarisha maisha yangu. Kuna haja kwa Serikali kuwatoa hawa watu wanaoishi sehemu kama hizi zenye hatari,” alisema Kazikazi.

Nao wakazi wa Kinyerezi mwisho, wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, walimuomba atazame namna ya kuwajengea kivuko katika mto Kinyerezi ili kusiwapo na kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.

Walisema kwa siku tatu sasa wanavuka mto huo kwa shida huku wakilazimika kulipia Sh1,000 au Sh500 ili wavushwe kwa kubebwa au kwa bodaboda.

Ombi hilo walilitoa jana, baada ya Chalamila kutembelea eneo hilo na kushuhudia shughuli za uvushaji watu zikifanyika kwa pikipiki na kubebwa mgongoni.

Rashid Issa, mkazi wa Kinyerezi Kanga anayeishi ng'ambo ya mto huo, alisema amelazimika kuzuia watoto wake wawili kwenda shule kwa siku ya pili kwa kuhofia usalama wao. “Kwanza kuvuka hapa wawili uwe na Sh1,000 kwenda na Sh1,000 kurudi, naitoa wapi? Bado hela ya matumizi. Kama haitoshi upo kazini huko mvua ikinyesha unawaza watoto wapo katika hali gani, tunaomba Serikali itusaidie," alisema Issa.

Issa alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuwajengea kivuko cha watembea kwa miguu ili waondokane na shida hiyo inayojirudia kila msimu wa mvua.

Rukia Mwaita, ambaye ni mwanafunzi anakiri kupata shida ya kuvuka anapofika eneo alilosema hulazimika kumsubiri mtu atakayemuonea huruma amvushe.

Mwananchi lilizungumza pia na mwanafunzi wa Makongi Sekondari, Andrew Kilangi alisema kipindi kama hiki cha mvua hawezi kwenda shule kwa sababu njia anazopita zinajaa maji.

“Mvua ikinyesha mfululizo siendi shuleni, njia ya kwetu si rafiki ila kipindi cha mitihani naongea na wazazi nalala kwa rafiki zangu hadi nitakapomaliza mitihani narudi nyumbani,” alisema Kilangi.

Naye Paskali Andrew, mkazi wa Kipawa alisema chanzo cha maji ya mvua kujaa kwenye makazi yao ni kukosekana kwa mitaro inayoweza kuelekeza maji bonde la Msimbazi.

Diwani wa Kinyerezi, Leah Bernard alisema kutokana na suala hilo wamekuwa wakikosa usingizi wakati wa mvua kutokana na simu za wananchi kutaka ujenzi wa daraja ama kivuko kidogo. “Mto huu watu wengi wameshabebwa mvua zinapokuwa kubwa, tunaomba tupate hata kivuko cha waenda kwa miguu, tunaomba tupate suluhisho la kudumu kuhusu huu mto maana unahatarisha familia zetu," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chalamila aliwataka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Tanesco na Tarura kukaa pamoja na timu ya mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam kuangalia nini kinaweza kufanyika.

Hiyo ni kutokana na kuwa eneo hilo pia linapitisha miundombinu iliyo chini ya TPDC na Tanesco, hivyo kabla ya chochote kufanyika ni lazima washirikishwe.