Mtoto mwenye ualbino aliyeporwa apatikana ameuawa na kunyofolewa viungo

Baadhi ya maofisa wa Polisi wakichukua mabaki ya mwili wa mtoto mwenye Ualbino, Asimwe Novath (2) yaliyopatikana siku 19 tangu mtoto huyo apokwe katika mikono ya mama yake mzazi na watu wasiyojulikana. Picha na Ananias Khalula.

Muktasari:

  • Mwili wake wapatikana ukiwa umenyonyolewa viungo na kufungwa kwenye kiroba cha sandarusi.

Siku 19 tangu mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) anyakuliwe na watu wasiojulikana kutoka mikononi mwa mama yake, mwili wake umepatikana ukiwa umefungwa kwenye kiroba cha sandarusi.

Tukio la Asimwe kupokwa katika mikono ya mama yake lilitokea Mei 30, 2024 katika Kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Akizungumza leo Jumatatu Juni 17, 2024, Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba mkoani humo, Benjamin Mwikasyege amethibitisha kupatikana mwili wa mtoto huyo, huku baadhi ya viungo vyake (bila kuvitaja) vikiwa vimenyofolewa.

Mwikasyege amesema mwili wa mtoto huyo umepatikana ukiwa chini ya moja ya karavati iliyoko katika barabara ya Makongora, Kitongoji cha Kabyonda Kijiji cha Balele Kata ya Ruhanga wilayani Muleba mkoani humo.

“Tumekuta mwili umekatwa baadhi ya viungo vya mwili na kutelekezwa, ila niwahakikishie Jeshi la Polisi wana wataalamu, watafanya uchunguzi wa kina, kisha tutawajua waliohusika,” amesema Mwikasyege.

Huku akionyeshwa kukerwa na unyama huo, Mwikasyege amewataka wakazi wa Kijiji cha Balele na vinavyokizunguka kutoa ushirikiano kwa maofisa wa Jeshi la Polisi, ili kufanikisha watuhumiwa wa mauaji hayo wanatiwa mbaroni.

“Wananchi msiogope maana wananchi mnaogopa kusema mkihisi kila atakayesema atakamatwa, naomba mtoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi litawakamata waliofanya kitendo hiki na kutekeleza mwili wa mtoto Asimwe chini ya karavati hii,” amesema.


Mwili ulivyopatikana

Kwa mujibu wa Diwani wa Ruanga, Wilaya Muleba mkoani humo, Robert Mugabe, alipokea taarifa kutoka kwa msamaria mwema za kuwepo kitu kinachotoa harufu isiyo ya kawaida chini ya karavati hilo, ndipo alipowataka wananchi kufika na kukagua kilichomo.

Mugabe amesema wakazi wa eneo hilo walipofika na kupekua walitambua kuwa kilichokuwemo ni mabaki ya binadamu ndipo walipotoa taarifa Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine za Serikali.

“Nilipokea taarifa za awali kutoka kwa msamaria mwema kuwa kuna kitu katika daraja la barabara ya Ruanga Makongora kinachotoa harufu mbaya. Nikawaambia waangalie ni nini, ndipo walipobaini kuwa ni mabaki ya mwili wa binadamu,” amesema diwani huyo.


Kauli ya familia

Jitihada za kupata kauli ya mama mzazi wa marehemu (Asimwe) zimegonga mwamba baada ya kushindwa kuzungumza kutokana na majonzi ya tukio hilo.

Hata hivyo, mama mkubwa wa marehemu, Vestina Richard (23) akizungumza kwa niaba ya familia, ameeleza kusikitishwa na kushtushwa na taarifa hiyo, huku akiwalaani waliohusika kuondoa uhai wa mpendwa wao.

“Familia tunalaani vikali kitendo hicho, tunaomba Jeshi la Polisi kwa kuwa kuna watu wanashikiliwa, basi iharakishe upelelezi wake kama ikibainika wanahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria,” amesema Vestina.

Kutokana na kifo cha mtoto huyo, Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ualbino nchini (TAS) Mkoa wa Kagera, Eginas Rugemalila amesema matarajio yao ni kuona Serikali inachukua hatua za haraka kuwaimarishia ulinzi na usalama wao.

Rugemalila amesema kitendo hicho kimeibua si tu taharuki, bali hofu kwa jamii ya watu wenye ualbino hasa kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025.

“Kwa sasa tuna hofu kubwa huyu mwenzetu kanyofolewa viungo na mwili kutelekezwa, hatujui wauaji wako wapi. TAS tunaomba kukutana na Mkuu wa Mkoa (RC) kujua mwafaka wa usalama wetu katika kipindi hiki,” amesema Rugemalila.


Wanne mbaroni

Alipopigiwa simu na Mwananchi kuulizwa kuhusu watuhumiwa wanaoshikiliwa kuhusiana na tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel ameahidi kutoa takwimu halisi kwa vyombo vya habari hivi karibuni.

Awali, Jeshi hilo lilithibitisha kuwashikilia watu wanne, akiwemo baba wa marehemu (Asimwe), Novath Venant kwa tuhuma za kutoweka kwa mtoto huyo.

Kwa mujibu wa jarida la shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utetezi na ustawi wa watu wenye ualbino nchini la Under The Same Sun la Septemba hadi Desemba 2010, na la Julai hadi Septemba 2018, matukio hayo ya ukatili, ukatwaji, au unyofolewaji viungo vya mwili, au ufukuliwaji makaburi na mauaji ya kinyama dhidi ya watu wenye ualbino yalianza kuripotiwa na vyombo vya habari katika kipindi cha miaka ya 2006 kwa kuhusishwa na imani za kishirikina.

Juhudi mbalimbali zilianza kuchukuliwa kwa kushirikiana na Serikali ambazo ni pamoja na kuanzishwa kwa kambi za watu wenye ualbino ikiwemo kambi ya Kabanga (Kigoma), Buhangija (Shinyanga), Mitindo (Mwanza), Pongwe (Tanga), Kitengule (Tabora) na Mugeza (Kagera).

Hata hivyo, baadhi ya watu wenye ualbino, wakiwemo watoto waliokuwa katika kambi hizo wakati wa matukio hayo walianza kurejea makwao baada ya hali ya usalama kuonekana kuwa imeimarishwa.

Hali ya usalama kwa watu wenye ualbino iliboreshwa zaidi kati ya mwaka 2015 hadi 2019 ambapo halikuripotiwa tukio lolote la ukatili ama unyama dhidi yao hadi ilipofika Novemba 2, 2022, ambapo Mkazi wa Ngula wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Joseph Mathias (50) aliuawa kwa kukatwa mapanga kisha wakataji kutokomea na mkono wake.

Tukio lingine lilitokea Mei 4, 2024, Katoro mkoani Geita, baada ya mtoto mwenye ualbino, Julius Kazungu (10) kunusurika kifo baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali na mtu ambaye hakutambulika.

Kwa mujibu wa Under The Same Sun, kwa Tanzania na Afrika Mashariki, mtu mmoja katika kila watu 1,400 ana ualbino.