Mtoto akitafuta maudhui yasiyofaa Instagram mzazi kupata taarifa
Muktasari:
- Meta yaimarisha ulinzi kwa vijana Instagram, wazazi kupata taarifa za tahadhari
Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya Meta Platforms imeongeza wigo wa hatua zake za kulinda watoto na vijana wanaotumia Instagram, kwa kuanzisha mfumo utakaowajulisha wazazi au walezi pale watoto wanapohusishwa na maudhui hatarishi, ikiwemo yanayohusu kujiua au kujidhuru.
Hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa akaunti za watoto, unaolenga kuweka mazingira salama zaidi kwa watumiaji wenye umri wa miaka 13 hadi 17.
Kupitia mfumo huo, Meta inalenga sio tu kuzuia maudhui hatarishi kufikiwa kirahisi, bali pia kuongeza ushiriki wa wazazi katika kufuatilia ustawi wa watoto wao mtandaoni.
Kwa mujibu wa maelezo ya kampuni hiyo, wazazi au walezi wataweza kupokea taarifa kwa njia kadhaa kupitia mfumo wa usimamizi wa akaunti za watoto, ikiwa ni pamoja na arafa (notifications).
Mzazi atapata arafa kwenye akaunti yake ambayo imeunganushwa na akaunti ya mtoto, pia atapata barua pepe (email alerts), zitakazotumwa moja kwa moja kwa mzazi aliyesajiliwa.
Aidha, kupitia dashibodi maalumu itakayowaonesha mwenendo wa matumizi ya mtoto, ikiwemo aina ya maudhui anayoyatafuta au kuyatazama.
Arifa hizi zitatolewa pale mfumo wa akili unde (AI) utakapogundua mienendo inayoweza kuashiria hatari, kama vile utafutaji wa maneno yanayohusiana na kujiua, kushiriki au kuhifadhi maudhui ya kujidhuru, au kufuatilia akaunti zinazochapisha maudhui hayo.
Hatua hii imechukuliwa Meta imesema uamuzi huo umetokana na kuongezeka kwa wasiwasi wa kimataifa kuhusu afya ya akili ya vijana na athari za mitandao ya kijamii.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa baadhi ya vijana hukutana na maudhui hatarishi bila kutarajia, hali inayoweza kuchangia msongo wa mawazo, huzuni au hata vitendo vya kujidhuru.
Kwa kuweka mfumo wa kuwajulisha wazazi mapema, kampuni inalenga kutoa nafasi ya hatua za haraka kuchukuliwa na wazazi au walezi kKuimarisha mazungumzo ya wazi ndani ya familia kuhusu matumizi ya mtandao.
Vilevile, kupunguza uwezekano wa vijana kuathirika kimya kimya na maudhui hatarishi.
Aidha, wataalamu wa usalama mtandaoni wanasema ushirikishwaji wa wazazi ni nyenzo muhimu katika ulinzi wa watoto, kwani mara nyingi wao ndio wanaoweza kutoa msaada wa karibu na wa haraka zaidi.
Mbali na mfumo huo wa arifa, akaunti hizo za watoto na vijana zinaendelea kuweka vizuizi vya kupokea ujumbe kutoka kwa watu wasiojulikana, kudhibiti aina ya maudhui yanayoonekana kulingana na umri.
Akaunti hizo zina ukomo wa muda wa matumizi ya Instagram, hitaji la ruhusa ya mzazi kwa vijana chini ya miaka 16 kubadilisha baadhi ya mipangilio.
Hata hivyo, wachambuzi wa teknolojia wanaonya kuwa pamoja na maboresho hayo, bado kuna umuhimu wa elimu endelevu kwa wazazi na watoto kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii, kwani changamoto za mtandaoni hubadilika kadri teknolojia inavyoendelea kukua.
Mzazi Amina Ramadhan kutoka Dar es Salaam anasema hatua hiyo ni muhimu kwakuwa itaomgeza ulinzi na kupunguza wasiwasi kwake pale anapokuwa mbali na mwanaye anayetumia mtandao huo.