Mtendaji wa Kijiji, wenzake wahukumiwa kunyongwa

Muktasari:
- Aliyekuwa Mtendaji wa kijiji na wenzake wanane wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa makosa ya mauaji.
Njombe. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Njombe imewahukumu kunyongwa hadi kufa washtakiwa tisa akiwemo Beatus Salum aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Kipengere wilayani Wanging'ombe kwa makosa ya mauaji ya ndugu wawili.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Zabibu Mpangule baada ya washtakiwa kukutwa na hatia katika kesi ya mauaji namba 11 ya mwaka 2019.
Amesema washtakiwa hao wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na kosa la mauaji ya ndugu wawili, Francis Chaula na Fabio Chaula.
"Kwa kuzingatia kwamba hapa kuna makosa mawili ya mauaji ya watu wawili wasiokuwa na hatia mahakama hii kwa kila kosa inawahukumu washtakiwa wote kunyongwa hadi kufa sawa sawa na kifungu namba 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 ya 2022," amesema Mpangule.
Amesema hata hivyo kama kuna upande una haja ya kukata rufaa kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo unaweza kufanya hivyo ndani ya muda.
Amesema washtakiwa hao mnamo April 27, 2020 katika kijiji cha Kipengere wilayani Wanging'ombe waliwaua Francis Chaula na Fabio Chaula, ambapo taarifa za uchunguzi wa miili hiyo ambayo ilitolewa na daktari ni kuwa vifo vyao vimetokana na kuvuja damu nyingi uliosababishwa kupigwa na vitu vizito.
Amesema miongoni mwa washtakiwa hao wapo viongozi ambao ni mwenyekiti wa kijiji, mtendaji wa kijiji pamoja na mwenyekiti wa CCM ngazi ya tawi.
Amesema viongozi hao wanaingia kwenye hukumu hiyo kutokana na kufanya vikao vilivyokuwa vikihusu mauaji kama ilivyoelezwa na mshtakiwa namba 5 kwenye kesi hiyo wakiwa na kisasi cha kumuua Frank Chaula ambaye ni baba wa watoto hao kwasababu amekuwa akiwasumbua katika maeneo tofauti tofauti.
Mpangule amewataja washtakiwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kuwa ni Fabian Chaula, Geoffrey Ilomo, Aurelius Mgaya, Richard Chaula,John Bosco, Otumary Mtivike na Beatus Salum.