Mtego wa ajira unavyowanasa vijana wengi

Muktasari:

  • Umewahi kuona mabango kwenye mbao, nguzo za umeme au kuta mbalimbali yakitangaza nafasi za kazi na kiwango fulani cha mshahara, mfano Sh270,000 au Sh370,000?

Dar es Salaam. Umewahi kuona mabango kwenye mbao, nguzo za umeme au kuta mbalimbali yakitangaza nafasi za kazi na kiwango fulani cha mshahara, mfano Sh270,000 au Sh370,000?

Je, umewahi kujiuliza kwanini inakuwa rahisi kutangaza fursa kama hizo wakati vijana kwa maelfu, wenye viwango tofauti vya elimu wanalia na uhaba wa ajira mtaani?

Kama kama huna majibu ya maswali hayo, je, umewahi kuona zilipo ofisi za kampuni zinazotangaza nafasi za kazi kama hizo au kukutana na walioajiriwa huko?

Mwananchi limekuja na majibu ya maswali yote uliyowahi kujiuliza kuhusu ajira hizo, baada ya uchunguzi wake uliofanya katika kampuni tatu tofauti.

Mwandishi wetu, aliyeomba na kufanya kazi katika kampuni hizo anasimulia undani wa ajira hizo, maisha ya waajiriwa na namna zinavyodumaza vijana kwa kujazwa matumaini yasiyowekewa msingi wa kufikiwa.

Matokeo yake vijana wengi wamejikuta wanashi kama mateka ambao hawana uwezo wa kujikwamua kutoka katika mikono ya wanaowatumikisha.

Mkurugenzi wa moja ya makampuni hayo, East Coast Marketing Company, Anizeth Msoka alisema wanayobandika mitaani ni matangazo tu, lakini utaratibu halisi hutolewa pale mwajiriwa anapofika ofisini.

Alipoulizwa kuhusua hali hiyo, Profesa Joyce Ndalichako, waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, alisema “sikuwahi kuona tangazo hilo, huku kwetu hayapo.

“Tunafanyia kazi iwapo kutakuwa na malalamiko lakini kama hakuna, hatuwezi kujua kuna nini kinaendelea wala kubaini changamoto zozote zinazowakumba hao wafanyakazi. Wewe niletee kesi nitafanyia kazi,” alieleza.


Naitwa kazini

Baada ya kufanya mawasiliano kupitia namba ya simu iliyoandikwa katika tangazo la kazi ili kujua utaratibu wa kutuma maombi na shughuli gani zinazofanyika, nilielekezwa niende ofisini nikiwa na barua za utambulisho kutoka Serikali za Mitaa.

Kwa sababu nilieleza natokea mkoani Manyara, nilipewa ruhusa ya kufika katika ofisi za kampuni yenye ajira karibu na Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi jijini Dar es Salaam.

Baada ya kupata barua kutoka Serikali za Mitaa, nilipiga simu kwenda ofisini kuwasilisha maombi yangu ya kazi na nilitakiwa kufika saa 2:30 asubuhi nikisisitizwa “zingatia muda”. Pia nilitakiwa kuzingatia mavazi ya kiofisi, kuwahi na kukamilisha taratibu zote zikiwemo barua.


Siku ya kwanza kazini

Nilipofika kituo cha Magufuli, nilielekezwa kwenda mbele zaidi kwamba ndipo ofisi iliopo. Ni katika nyumba namba 11, ambayo ni vigumu kujua kama ni ofisi ya kampuni, kwa kuwa hakukuwa na bango wala kielelezo chochote.

Pia, ni miongoni mwa nyumba bora zilizokuwepo katika eneo hilo, niliingia nikijiuliza kwanini ofisi ifichwe kiasi kile na kwanini isiwekwe hata bango kuitambulisha?

Wakati naingia ndani baada ya kuvuka geti, nikakutana na vijana kadhaa wakiwa katika pilika za kubeba mabeseni na ndoo mpya za taka, kila mmoja akijitwisha kwa uwezo wake.

Tofauti na nilivyoelekezwa kuvaa kiofisi, kati ya vijana niliyowakuta katika ofisi hiyo hakuwepo hata mmoja aliyevalia mavazi hayo, ingawa mimi pia sikuwa nimevaa hivyo, angalau ili kuonyesha uhalisia wa ugumu wa maisha na uhitaji wa kazi iliyotangazwa.

Kwa kiasi fulani nilijikuta nafanana na vijana waliokuwepo hapo na baada ya kupokelewa nilielekezwa katika chumba kinachoonekana kama ofisi, ili kuwasilisha barua na kufanyiwa usaili.

Sikuwa nimebeba vyeti vyangu na nilidhani hicho kingekuwa miongoni mwa vigezo vitakavyoathiri nia yangu ya kupata kazi, lakini haikuwa hivyo.

Nilikutana na mkurugenzi aliyeitambulisha kampuni kwangu kwa jina la East Coast Marketing Company.

Mkurugenzi alipokea barua za utambulisho na kunihoji maswali kadhaa ikiwemo ninapotokea, kazi nilizokuwa nafanya kabla na kunikabidhi kwa mmoja wa vijana.

“Hapa tuna vitengo mbalimbali lakini kwa sasa kilichobaki ni mauzo na masoko kwa hiyo utaanza kufanya kazi huko, kisha tutakubadilisha kwa siku za baadaye,” alisema mkurugenzi huyo.

Kwa kuwa mazungumzo yetu hayakuhusisha mshahara nitakaolipwa wala kusainishwa mkataba wowote, hapo ndipo nilianza kuona tatizo, lakini nilisubiri pengine hayo yangefanyika siku nyingine.

Mazungumzo hayo ndiyo yaliyokuwa usaili na tayari nikapewa kazi. Kijana niliyekabidhiwa kwake akaelekezwa aniongoze katika kazi kwa siku za mwanzo.

Baadaye nilibaini hapo ofisini wanaishi takribani vijana 12 wakifanya kazi za kutembeza vyombo mitaani kama machinga.

Vijana hawa wanatoka katika mikoa mbalimbali ambao, kama ilivyokuwa kwangu, walifika Dar es Salaam baada ya kuona vipeperushi vya matangazo ya ajira na kupiga simu kuomba nafasi.

Vijana hawa hatimaye wamekwama, hawana namna ya kurudi makwao.


Waitikia positive, correct

Kila kijana aliyeitwa na kuelekezwa jambo na kiongozi wao aliitikia kwa neno ‘positive’ na baada ya kudadisi niliambiwa kuwa ndiyo salamu na namna ya kuitika kwa jambo lolote utakaloambiwa katika ofisi hiyo, ikimaanisha ni kukubaliana na kila jambo.

Hali kama hiyo niliikuta katika kampuni zote tatu nilizofanya kazi katika maneno tofauti, eneo la kwanza waliitikia ‘sure’ na lingine ‘correct’ kote wakimaanisha maelekezo ni amri na hayapingwi.

Baada ya kumdadisi kijana niliyekabidhiwa kwake kuhusu neno ‘positive’ alisema ni ishara ya kukubali na kutii maelekezo, huku akinionya iwapo nitajibu kinyume nitajiweka katika mazingira magumu ya kupata fursa zaidi ndani ya ofisi.

Kampuni hizi huandaa mikutano na vijana wanaofanya nao kazi kila Jumapili kwa ajili ya kuwafundisha namna ya kutaja sifa za bidhaa wanazouza kwa harakaharaka, wakisema ni mbinu ya kumpunguzia hoja mteja.

Katika vikao hivyo, pia ndiko zinakotolewa ahadi za kupandishwa vyeo au kuhamishwa vitengo na ofisi ambazo kwa uhalisia hazipo, bali ni mbinu za kuwajaza vijana matumaini yasiyofikiwa.

Kampuni ya East Coast Marketing ili iweze kuaminika zaidi ilidai ina duka kubwa ‘Super Market’ eneo la Mwenge, Dar es Salaam lilioandikwa jina hilo na hata nilipolitafuta kupata uhakika wa hilo, sikuliona.


Mtaa kwa mtaa

Nikiwa ofisini hapo, kijana niliyekabidhiwa kama mwelekezaji wangu katika kazi, alipotea kwa dakika chache kisha akarudi na mabeseni 16 na ndoo tano za kutupia taka alizonikabidhi tayari kuanza safari ya kwenda kufanya kazi.

Sikupewa nauli wala fedha za chakula, lakini mwenyeji wangu aliniambia siku hiyo ulikuwa tutakwenda kufanyia kazi Kongowe mkoani Pwani (takriban kilometa 33).

Wakati nashangaa hukusu umbali wa safari, kijana alisema eneo hilo ni jirani zaidi kati ya maeneo ambayo huwa anapangiwa kwenda kufanya kazi, tena bila kupewa nauli wala fedha ya chakula.

“Ili kupata nauli tunaenda Mbezi Luis stendi ya daladala tunatembeza hizi ‘dustbin’ kwenye daladala, ukiuza moja umepata nauli ya kwenda safari yako, kurudi na kula utajua huko huko,” alisema.

Nilipomuulizi iwapo ofisi haitambui kukosa nauli, alisema inachohitaji ni mfanyakazi afike katika eneo alilopangiwa kwa mbinu yoyote.

Wakati najaribu kumuuliza kuhusu mshahara ili nisionekane mwenye tamaa, kijana alisema malipo ya mfanyakazi ni asilimia 10 ya mauzo ya siku, ambayo hukusanywa kwa kipindi cha wiki au mwezi kisha unakabidhiwa.

Hata hivyo, uhalisia wa soko ulivyo ni vigumu kuuza zaidi ya Sh15,000, hivyo kiwango kikubwa cha ujira alichowahi kupata mwenyeji wangu ni kati ya Sh1,000 na 1,500 kwa siku ambazo alisema zinamwezesha kula akiwa katika eneo la kazi.

Kutokana na hali hiyo ya kipato, alisema lengo lake kuu ni kutaka kurudi nyumbani mkoani Mwanza lakini ameshindwa ndani ya miezi nane aliyofanya kazi na hadi ameizoea kazi hiyo.

Licha ya ujira usioendana na ahadi katika tangazo la kazi, kijana huyo amejazwa matumaini ya kupatiwa fursa zaidi na taasisi hiyo, ambayo msingi wa kuyafikia hauonekani.

Miongoni mwa vitu anavyoahidiwa, alisema ni kufunguliwa tawi la taasisi hiyo na atakuwa meneja akisimamia wafanyakazi wengine na kwamba akifikia hatua hiyo ndipo atalipwa Sh270,000.

Pamoja na ahadi hiyo, alisema ameambiwa wapo wengine waliopewa cheo hicho katika mikoa mbalimbali, lakini nilipodadisi kwa uongozi wa kampuni nisubaini kuwepo kwa tawi na hawakueleza zilipo ofisi zao mikoani.

Maswali hayo nilimuuliza tukiwa kwenye daladala kuelekea Kongowe ambapo nilichangia Sh1,000 kati ya Sh3,000 ya nauli ya jumla tuliyopaswa kulipa.

Hadi tunafika Kongowe, ilikuwa saa 6:00 mchana, mwenyeji wangu alinielekeza kuacha mabeseni 10 katika moja ya maduka yaliyokuwepo karibu na kituo cha daladala na tulibaki na sita na ndoo tano za taka, tayari kwenda kuuza mtaani.

Alisema kwa kuwa mzigo ulikuwa mkubwa tusingeweza kuubeba wote na kuzunguka mitaa, hivyo tunapaswa kuacha kwa mfanyabiashara yeyote anayeonekana kuwa na bidhaa zisizohamishika haraka kwa usalama.

Nilibeba ndoo tano na mabeseni matatu, tukaanza kutembeza mtaani, huku nikihoji kama ile ndiyo kazi ya kitengo cha mauzo na masoko?

Alinijibu ndiyo kazi yenyewe, akinifundisha namna ya kuzungumza haraka haraka kutaja sifa za bidhaa na kushawishi wateja, huku akinisihi nisiwe naongea pindi atakapokuwa anazungumza na mteja.

Kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Jafes Nelson (23) alinipa moyo kuwa ugumu wa kazi ni siku za mwanzoni, lakini kadri nitakavyokuwa nafanya nitazoea kama ilivyokuwa kwake.

Mzunguko wa nyumba kwa nyumba, duka kwa duka ulifanikisha mauzo ya mabeseni mawili na ndoo tatu za kutupia taka.

Katika kila beseni moja, ofisi inahitaji Sh5,000 ambayo ndiyo bei yake halisi, wakati ndoo ya taka inatakiwa Sh2,000 na ili kupata hela ya nauli na chakula cha mchana unatakiwa kuuza bei ya juu zaidi.

Si rahisi kama unavyoweza kufikiria, katika wateja wote tuliozungumza nao hakuna aliyenunua beseni kwa bei zaidi ya Sh5,000 huku wengine wakitoa maneno machafu wanapotajiwa bei ya juu.

Ulifika wakati mwenzangu alilazimika kutia huruma kwa wateja akiwataka wanunue angalau tupate nauli ya kurudi Mbezi ilipo ofisi yetu. Hiyo ilikuwa yapata saa 10 alasiri na hatukupata chakula cha mchaka kutokana na kushindwa kuuza kwa bei ya juu zaidi.

Asilimia 10 ya mauzo ya mabeseni mawili ni Sh1,000 hivyo ndiyo ujira tuliopaswa kulipwa kwa siku hiyo. Nelson alisema kwa kawaida zaidi ya hiyo huwa anapata Sh1,500 na hakuwahi kupata zaidi.


Mambo yaleyale

Katika kampuni hii na nyingine mbili ambazo hazikuwa na majina, nilibaini zinafanya biashara mbalimbali, zikiwatumia vijana kutembeza bidhaa mtaani kama machinga ili kukwepa kodi.

Majina zinayotumia ukipiga simu ni tofauti na unayootajiwa ukifika ofisini na miongoni mwa sifa za kupata kazi ni kutokuwa mkazi wa Dar es Salaam.

Hazina makao rasmi, mbali na hii niliyotajiwa kama East Coast, nyingine mbili wafanyakazi wake wamedai wanahama karibu kila baada ya wiki.

Na baadhi ya kampuni hujitambulisha kwa majirani kama familia badala ya sikampuni, walieleza majirani wa East Coast Marketing Company, eneo la mbezi jijini Dar es Salaam.


Hakuna ruhusa, likizo

Katika kampuni hizo, mfanyakzi atakayeondoka hapaswi kurudi, hakuna bima na atakayeugua atatibiwa kisha atakatwa gharama alizotumia katika sehemu ya ujira wake.

Pamoja na hayo, vijana hao husalia katika kampuni hizo wakidai angalau mlo mmoja wanaoupata katika kampuni hiyo kuliko kurejea makwao, hali inayochangiwa na umaskini na kukosa kazi.

“Nyumbani hatuwezi kula hata usiku, bora mtu umepata nafasi hii unakula usiku unalala,” alisema Neema Matusela.

Hata hivyo, wengine wanasema wanalazimika kukubaliana na maisha hayo na hawana namna ya kufanya kwa kuwa hata wangefanya kazi kiasi gani fedha wanazolipwa haziwezi kufikia nauli ya kuwarejesha kwao.

Rajab Mmela (24) anayetokea Tabora, alisema anatamani kurudi nyumbani lakini fedha anazolipwa hazitoshi kupata nauli ya kufanikisha hilo.

Alisema wakati anaanza kazi alitarajia angelipwa kulingana na kima kilichowekwa katika tangazo, lakini amekutana na mambo tofauti baada ya kuwa ameshafika Dar es Salaam na hana namna ya kurudi kwao.

Lakini, alisema kuna wakati anawaza atakwenda kufanya nini akirejea nyumbani, hivyo amebaki njiapanda.


Elimu kikwazo

Kati ya vijana 12, wanaofanya kazi katika kampuni ya East Coast Marketing Company ni wawili tu waliofika kidato cha nne, wengine ni wahitimu wa darasa la saba.

Ofisi zinazotumika na kampuni husika ndiyo eneo la kulala, hivyo katika chumba kimoja wanalala vijana nane kila mmoja akiwa na godoro lake dogo kwa makadirio ni kati ya futi tatu kwa sita.

Huduma zinazopatikana katika makazi hayo ni chakula cha usiku, hivyo vijana wengi wanafurahia maisha hayo kutokana na historia ya walipotoka kukosa hata mlo mmoja kwa siku.


Anayeweza anafanya

Mkurugenzi wa Kampuni ya East Coast Marketing Company, Anizeth Msoka alisema kinachoonekana mtaani “yale ni matangazo kwa kuwa kampuni hiyo inafanya shughuli za masoko na mtu anaelekezwa utaratibu akifika ofisini.

“Mfumo wa ulipaji ni asilimia 10 kila mtu anaelekezwa, ambaye anaweza anafanya bro (kaka),” alisema.

Hata hivyo, Msoka alieleza kwa ufupi kwamba kampuni yake haipo mafichoni na kwamba kila kitu kimesajiliwa.


Tatizo ni ajira

Kwa mujibu wa Abbas tatizo la ajira ni moja ya sababu zilizomuingiza katika shughuli hiyo, suala ambalo Serikali imeweka mikakati kulipunguza kupitia kilimo, kwa mujibu wa bajeti ya mwaka 2022/2023.