Mtanzania afungwa Ulaya kwa kutuma picha za maiti Facebook
Muktasari:
Mtanzania huyo, Omega Mwaikambo alituma picha za maiti ya mtu aliyefariki katika ukurasa wake wa Facebook inayoonyesha majeraha yake.
Tabia wanayoifanya watu wengi ya kutuma picha zisizofaa katika mitandao ya kijamii, imemponza Mtanzania anayeishi Uingereza na kusababisha ahukumiwe kifungo cha miezi mitatu na faini.
Mtanzania huyo, Omega Mwaikambo alituma picha za maiti ya mtu aliyefariki katika ukurasa wake wa Facebook inayoonyesha majeraha yake.
Mwaikambo, mwenye umri wa miaka 43, alituma video na picha za mwili wa marehemu uliokuwa kwenye begi na baadaye picha nyingine tano zikionyesha uso wa mtu huyo aliyefariki kutokana na ajali ya moto katika jengo la Grenfell Tower, Westminster, Uingereza.
Pia mtu huyo, ambaye inaelezwa kuwa alisoma Shule ya Sekondari Tambaza jijini hapa kuanzia 1988 hadi 1991 kabla ya kwenda Uingereza, ametakiwa kulipa faini ya Sh508,880 kwa mwathirika wa tukio hilo.
Tukio hilo limeripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari na kulaaniwa vikali na Waingereza.
Akitoa hukumu hiyo juzi, Jaji Tanweer Ikram wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Westminster, alisema: “Dunia nzima imeshtushwa na yaliyotokea hapa kutokana na janga la moto. Ni hali ya kutisha isiyostahimilika. Wafu ni lazima waheshimiwe.”
Mwaikambo alikiri makosa ya kutuma mara mbili picha zisizopendeza kwa umma katika mitandao ya kijamii.
Gazeti la Telegraph liliandika kuwa Mwaikambo anaishi hatua chache kutoka lilipo jengo la Grenfell akifanya shughuli za upishi, na alishuhudia jinsi jengo hilo lilivyoungua usiku na alikuwa ni miongoni mwa wapishi waliowapikia chai maofisa wa uokoaji waliokuwa wakizima moto huo.
“Lakini Jumatano asubuhi, alipoona miili hiyo nje ya nyumba yake, alichukua picha kwa kutumia simu yake aina ya iPad na kuzituma kwenye ukurasa wake wa Facebook,” limeandika gazeti hilo.
Mwaikambo aliandika: “Kuna mtu anaujua mwili huu uliolala nje ya jengo kwa saa mbili?”
Jaji Ikram alisema ni dhahiri kitendo cha kutuma picha hizo Facebook hakijaonyesha heshima kwa waathirika wa tukio hilo na kuonyesha uso wa maiti hadharani ni kosa ambalo halielezeki.
Mpaka sasa watu zaidi ya 17 wanasadikiwa kufariki dunia kutokana na moto uliounguza jengo hilo refu na maarufu lililo magharibi mwa Uingereza.
Kaimu meneja wa mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakanjala alisema hapa nchini mtu anapotenda kosa hilo na akaripotiwa, hukamatwa kwa Sheria ya Makosa ya Kimitandao (Cybercrime Act) chini ya kifungu cha matumizi mabaya ya mitandao.
“Makosa kama haya ni uhalifu na yanashughulikiwa na kitengo cha uhalifu wa mtandaoni cha Jeshi la Polisi. Sisi tunawapa msaada wa kitaalamu, lakini pia huwa tunawakumbusha wananchi juu ya matumizi sahihi ya mitandao,” alisema Mwakanjala.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye mafanikio makubwa katika masuala ya kimtandao, lakini wananchi hawaioni fursa hiyo ya kimaendeleo na badala yake wanaitumia kwa ajili ya mambo yasiyo na tija.
Kwa upande wake, Ismail Njoka ambaye ni mkazi wa Mwenge jijini hapa, alisema tabia ya Watanzania kusambaza picha zisizo na maadili katika mitandao ya kijamii, limekuwa sugu na linahitaji mkazo wa kisheria na elimu kwa wananchi.