Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mstaafu anapoishia kujiuliza ashike lipi, aache lipi!



Majuzi hiki chama kisemekanacho kuwa ni cha kuwatetea na kuwasemea waajiriwa kuhusu matatizo yao, kimefanya jambo moja kubwa ambalo hakijawahi kulifanya kwa huyu mstaafu wetu na wenzake wote kwa miaka 40 waliyokuwa waajiriwa wakiijenga nchi hii.

Chama kisemekanacho kuwa ni cha kuwatetea wafanyakazi, kimefanya jambo jema la kumpa pole mwajiri mkuu wa nchi kwa maswaibu yaliyompata ya kuiongoza nchi kwenye uchaguzi mkuu wa Taifa na yaliyofuata. Hakikutoa pole kwa wafanyakazi kwa kukosa nyongeza ya mishahara ya kuboresha maisha yao ili wakabiliane na hali ngumu ya maisha inayomkabili kila mtegemea mwisho wa mwezi... na petroli!

Mstaafu wetu anajua kuwa mheshimiwa mwajiri mkuu wa nchi alikuwa kwanza mfanyakazi aliyekuwa mwanachama wa hiki chama cha kuwatetea wafanyakazi, na ninaamini alikuwa akilipa ada yake vyema tu ya kila mwezi ili uanachama wake chamani uwe hai.

Mstaafu anatatizika kidogo anapojiuliza iwapo uanachama wake chamani ulikoma mara tu pale Katiba yetu ilipomteua kuwa mwajiri nambari moja wa Taifa letu na uanachama wake kwenye kile chama cha kutetea wafanyakazi ukaishia hapo.

 Naam, anatoka kuwa mwanachama mwajiriwa na kuwa mheshimiwa mwajjiri mkuu wa Taifa! Uzuri wa Katiba yetu, japo inahitaji ‘viraka’ viwili vitatu, kama si vinne vitano vya ziada ili kuwa bora zaidi!

Pamoja na hilo, mstaafu wetu alitegemea kuwa chama kijitokeze na kuwaeleza wanachama wake wengi wa kutosha wanaolipa ada inayoeleweka kila mwezi kuwa chama chao kitapambana ‘juu chini’ ili wafanyakazi wapate nyongeza ya mishahara ili waweze kukabiliana vyema na kupanda kwa bei ya mafuta, kunakomaanisha kupanda kwa bei za vitu vyote muhimu kwa binadamu!

Kuhusu hilo, mheshimiwa mwajiri mkuu akatoa maelezo kuwa chama kilimpa pole kwa mishughuliko na hela kubwa iliyotumika kuendesha uchaguzi mkuu wa Taifa uliogharimu Shilingi trilioni moja, na kwa maana hiyo masuala ya nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi mwaka huu yamewekwa ‘pending’ (Kimbugu kwa msisitizo!) hadi May Day mwakani!

Ndoto ya mstaafu ya kupokea pensheni ya Shilingi laki tano kwa mwezi ikaanza kuota mbawa, huku Kinondoni ikimkonyeza fasta, maana alikuwa na matumaini makubwa kwamba wafanyakazi wakiongezwa mishahara, panga pangua na wao wastaafu wa kima cha chini wataponea humo. Kumbe imekuwa maweee!

Maana nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi waliopo kazini ilikuwa na maana kuwa hata wastaafu wa kima cha chini wangekumbukwa, japokuwa si lazima iwe hivyo, maana kama wastaafu hawatambuliki kuwa wastaafu, sembuse wale wa kima cha chini ambao ndio wa mwisho kabisa kwenye mlolongo wa wastaafu!

Mambo haya ndiyo maana husababisha hata kuhakikiwa tu, wastaafu huwabidi wengine kulazimika kupanda magorofa ili kufika kwenye baadhi ya ofisi za kuhakiki.

Wazee hawa walio na miaka 70 mpaka 80 na... tuoneeni huruma jamani, maana hata kama tunaweza kujikongoja wenyewe kupanda hiyo ‘milima’ ndani ya magorofa yenu, bado tu uzee, magonjwa yetu ya uzee na tabu nyingine, lakini kuhakiki bado kunatuhusu! Tutafutieni utaratibu mwingine ili tule laki mbili na nusu zetu kwa amani!

Kwa waajiriwa wale wengine ambao huona ni usumbufu kuwahudumia wastaafu wazee, heri yao, maana hata hawakumbuki kuwa muda mfupi tu ujao, ustaafu utawahusu, na kikokotoo ambacho hiki chama kinachopaswa kuwatetea kweli wafanyakazi kimekubali kukipitisha kirahisi rahisi na kusahau kuwa kitawabamiza, kama wastaafu wanavyobamizwa na riba na tozo za mikopo! Pole zao.

Inasikitisha sana kuwa wastaafu hawajawahi kupokea ‘pole’ kutoka kwa Serikali yao, kutoka kwenye chama kinachopaswa kuwatetea wafanyakazi na kutoka kwenye kibubu cha akiba ya uzeeni, pamoja na kutumia hela ya wastaafu kujenga magorofa ya kukodisha na kuuza. Si neno. Hata ‘pole’ tu ya pensheni ya Shilingi laki tano kwa mwezi itatutosha!

Inawezekana. Ni utashi tu, kama ule ulioamua baadhi ya watu katika nchi yenye vyanzo tele vya kupata mshiko tulivyotengeneza, wapate mshahara wa Shilingi milioni... mama wee!... 14 na marupurupu yake mengine, huku tulioijenga na kuilinda nchi kwa jasho na damu yetu kwa miaka 40 ya ajira tukiishia kulipwa pensheni ya tushilingi laki mbili na nusu tu kwa mwezi! Ni utashi unaoshangaza.


0754 340606 / 0784 340606