Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KONA YA MSTAAFU: Mstaafu anapotamani kumpiga kofi au kumpigia makofi mtu!

Ni Mitihani. Mstaafu sasa anafikishwa mahali pa kuwaza na kutamani, achague ama ampige kofi au ampigie makofi mtu, kutokana na haya yanayoendelea kumhusu yeye mstaafu wa kima cha chini aliyeijenga nchi hii kwa jasho na damu yake. Ni Mitihani!

Anasikitika sana kwamba wapo watu wachache sana, rudia wachache sana, kama wapo, kwenye suala la kumjali na kumwezesha mstaafu wa kima cha chini kukabiliana kweli na hali ngumu ya kustaafu kwake, wanaostahili kupigiwa makofi kwa kumjali mstaafu aliyeijenga nchi hii ambayo sasa inaliwa na wenye meno tu na sio wenye moyo, kama walivyokuwa yeye na kima cha chizi wenzake.

Ndiyo, Mstaafu sasa anasikitika sana kuona kuna rundo la watu ambalo wanadai kuwa wanaongoza vyama vinavyosemekana vya kuwasemea na kuwaongoza wafanyakazi ambao hawajafanya wala kutamka lolote wala chochote kuhudu Mstaafu huyu kuongezwa pensheni yake, ili aweze kukabiliana kweli na hali ngumu ya maisha Inayoelekea sasa inataka sasa 'kumstaafisha' kweli mstaafu kumpeleka Kinondoni!

Mstaafu amefanya kazi kwa miaka 40 na amekatwa mshahara wake kwa miaka hiyo 40 kwa kile alichoaminishwa kuwa ni kwa ajili ya kumsaidia atakapostaafu na alipostaafu akaambiwa anastahili kupata shilingi elfu 50 tu kutokana na michango yake kwenye mshahara wake wa miaka 40, huku akiona kibubu chake kikigeukia kujenga na kukodisha magorofa kutokana na hela zilizotoka kwenye michango ya mshahara wake wa miaka 40.

Kibubu kinafanya hivyo lakini kodi na mauzo ya majengo hayo inaelekea hazimhusu mstaafu, wala hajui nani anayezipokea na anapata mshahara wa Shilingi milioni ngapi kwa mwezi wakati yeye mstaafu akipokea pensheni ya shilingi laki mbili unusu kwa mwezi, huku kibubu kinachosemekana kumtetea mfanyakazi ghafla kikiwa bubu! Kuna mtu kofi lisilo la kushangilia linamhusu!

Hivi ni vile vyama ambayo vinapopata bahati ya kuonana na mheshimiwa yoyote, vinakuwa na wazo tu la kumzawadia mheshimiwa picha yake au kinyago lakini havimbani kwa kumuuliza lini atawapandishia pensheni wastaafu wa nchi wa kima cha chini ili wapambane kweli na hali ngumu ya kustaafu.

Tukumbuke kwamba kuna vyama vya wafanyakazi nchi nyingine vinavyoweza hata kushika madaraka ya kuongoza nchi na kuiambia siri-kali ichape lapa, lakini hivi vya kwetu viko kutafuna vitamu tamu kwa waheshimiwa badala ya kuwabana ili kujua ni lini watampandishia pensheni yake mstaafu wa kima cha chini aweze kupata japo Shilingi laki tano kwa mwezi.  

Ndiyo maana kikokotoo kiliweza hata kupitishwa na kutumiwa pamoja na kelele za waajiriwa za kukipinga. Kikokotoo kikapita salamaa, kama vile hakuna vyama vya kuwasaidia waajiriwa. Dhahiri hapa mstaafu anaona kofi la kumpiga mtu badala ya makofi ya kumshangilia mtu, yanawahusu viongozi wa vyama vya waajiriwa.

Wako wengi. Kuna yule aliyemshtua sana nusura kumpeleka Kinondoni, aliyesema mstaafu anastahili kupata Shilingi milioni tano na laki tano, na kumfanya mstaafu kuona kuwa angalau bado kuna watu wanaostahili kupigiwa makofi kushinda hata yale wanayopigiana wale wa Domdom...

...Maawee, hata kabla wino wa maandishi hayo haujakauka, mheshimiwa akamalizia kuwa mstaafu atapata Shilingi milioni tano na laki tano hizo akiwa amekufa sio akiwa hai, ili familia yake igawane kile alichochuma kwa miaka 40 aliyofanya kazi ya kuijenga nchi. Mstaafu ameishia kuona dhahiri kuwa kuna mtu kofi lisilo la kushangilia linamhusu.

Na Shida zote hizi unampaje mstaafu shilingi milioni tano na laki tano akiwa maiti, na sio akiwa hai ili ajipongeze kwa kazi nzito aliyofanya kwa Taifa kwa miaka 40 kwa usalama! Mpeni Shilingi milioni tano zake mstaafu akiwa hai, maana mkono wake wa miaka 67 sasa hauwezi hata kuumba tonge vizuri la ugali wake, sembuse kupiga kofi shavu la mtu.