Msongamano wa magari wakithiri Moshi

Muktasari:

Mji wa Moshi umekumbwa na msongamano mkubwa wa watu pamoja na magari kufuatia idadi kubwa ya wageni wanaoingia mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mapumziko ya Sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.

Moshi. Mji wa  Moshi umekumbwa na msongamano mkubwa wa magari na watu  kufuatia idadi kubwa ya wananchi wa mkoa huo wanaoishi nje ya mji huo kuwasili kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu za mwishoni mwa mwaka.

Hali hiyo imewalazimu askari wa kikosi cha usalama barabarani kuingia katikati ya barabara za mjini hapa ili kuongoza magari na kukabiliana na msongamano uliopo  barabarani ambao unasababisha foleni kubwa.

Aidha, msongamano huo umesababisha adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa mji huo wanaokwenda maeneo tofauti tofauti, kama vile Kiboriloni, Himo na maeneo mengine jirani na mji huo wakikaa barabarani kwa muda mrefu.

Pia, Mwananchi limetembelea maeneo mbalimbali ikiwemo sokoni, kwenye maduka makubwa na kujionea msongamano mkubwa wa watu.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Desemba 24, 2018, wakazi wa mji wa Moshi, wameeleza kushangazwa na idadi kubwa ya wageni waliopo kwa sasa na kusema hali hiyo imewafanya kukaa barabarani muda mrefu kutokana na foleni ya magari iliyopo.

Mary Shayo ambaye ni mkazi wa Moshi ameelezea kukerwa na msongamano huo mkubwa wa watu katika barabara ya Mbuyuni na barabara za katikakati ya mji.

"Nimetoka sokoni kununua vitu vya kupika kwa ajili ya sikukuu, yaani njia hazipitiki msongamano wa watu na magari ni mkubwa, hata kama una usafiri wako unaweza simama barabarani zaidi ya saa mbili," amesema Mary.

"Tumeona maeneo mengi trafiki wanaongoza magari lakini msongamano uko palepale, watu ni wengi mno sasa, kesho sikukuu sijui itakuaje kama hapa Soko la Mbuyuni watu ni wengi hakuna pa kukanyaga," amesema.

Mmoja wa madereva wa daladala za Kiboriloni, Hashimu Issah amesema msongamano huo wa magari umempelekea kusimama barabarani zaidi ya saa moja jambo ambalo halijawahi kutokea.

"Yaani leo hapa mjini msongamano wa magari ni mkubwa mno, mtu unakaa barabarani zaidi ya saa moja, hii ni hatari maana unakuta mtu mwingine anamuwahi mgonjwa hospitali,” amesema Issah.