Msongamano ‘baibai’ daraja la Kintinku, madereva waonywa

Baadhi ya magari makubwa yake, yakipita juu ya daraja la Kintinku mkoani Singida
Muktasari:
- Madereva wa mabasi na magari makubwa wameondokana na adha ya msongamano na uharibifu wa vyombo vyao baada ya ujenzi wa barabara ya lami katika daraja la juu la Reli ya Kisasa (SGR) kukamilika.
Singida. Changamoto ya uharibifu na msongamano wa magari katika daraja la juu ya Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Kintiku wilaya ya Manyoni mkoani Singida, umemalizika baada ya ujenzi wa barabara ya lami katika eneo hilo kukamilika.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 24, 2025 baada ya kutembelea ujenzi wa barabara hiyo.

Ujenzi wa daraja hilo umetekelezwa kwa ushirikiano wa Tanroads na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambapo Besta amewaonya madereva wafuate alama za barabarani ili kuepusha ajali katika eneo hilo.
“Nimeridhishwa na ukamilishaji wa kazi ya ujenzi wa barabara ya lami eneo la Kintinku Overpass ya SGR. Kazi iliyofanyika kati ya Tanroads na TRC ni nzuri na sasa msongamano wa magari umepungua kabisa,” amesema.
Amesema barabara hiyo inayotoka Dodoma kuelekea Singida, ni muhimu kwa uchumi wa wananchi na amewaomba radhi kwa usumbufu walioupata wakati wa ujenzi.
Mkurugenzi huyo amesema barabara hiyo imekamilika tangu Machi, mwaka 2025 na hivyo kuwarahisishia wananchi wanaoitumia.
Naye Mkuu wa Kitengo cha matengenezo wa Tanroads, Mkoa wa Dodoma, Elisony Mweladzi amesema ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 100 na ametoa wito kwa madereva kuhakikisha wanaitunza.

“Tunawaomba madereva, hasa wa magari makubwa kuzingatia sheria za barabarani kuepuka kutupa taka ovyo, kumwaga mafuta na kutengeneza magari yao barabarani mara yanapoharibika,” amesema Mweladzi.
Mmoja wa madereva wanaoitumia barabara hiyo, Hassan Hamis amesema kukamilika kwa barabara hiyo kumepunguza kero ya msongamano na uharibifu wa magari yao.
“Hiki kipande kilikuwa na changamoto kubwa kwetu, magari yalikuwa yanashindwa kupanda kilima na mengine kuharibika mara kwa mara. Lakini sasa hali ni nzuri, tunashukuru sana Serikali kwa maboresho haya,” amesema dereva wa lori, Hassan Hamis.