Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MSD, hospitali watafuta suluhisho la madeni

Muktasari:

  • Serikali kupitia Wizara ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na hospitali wameanza mkakati wa pamoja kudhibiti madeni ili kuimarisha upatikanaji endelevu wa dawa nchini.

Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD), imeanza hatua mpya ya kuimarisha usalama wa kifedha wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini. Hatua hiyo imekuwa kufuatia ongezeko la madeni kutoka kwa taasisi mbalimbali zinazohudumiwa na MSD.

Wakati mjadala huo ukifanyika, Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, iliyotolewa bungeni Mei 11, 2026 ilionyesha kuwa MSD inaidai Serikali Sh302.2 bilioni zinazotokana na usambazaji wa dawa na vifaatiba katika vituo vya afya pamoja na miradi misonge.

Makubaliano hayo yameazimiwa katika kikao kazi kilichofanyika jana Mei 13, 2026 jijini Dodoma, kikihusisha viongozi wa Wizara ya Afya, MSD pamoja na wawakilishi wa taasisi na hospitali zaidi ya 45 nchini.

Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa kujadili mikakati ya kudhibiti na kuondoa madeni yanayoikabili MSD ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa, vifaatiba na vitendanishi katika vituo vya afya.

Baadhi ya Wakurugenzi wa Hospitali mbalimbali nchini.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Serikali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Emmanuel Tayari alisema Serikali imekusudia kuona taasisi zote zinazohudumiwa na MSD zinashiriki kikamilifu katika kujenga mfumo endelevu wa kifedha utakaoihakikishia bohari hiyo uwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kuyumba.

Alisema changamoto ya madeni imekuwa mzigo mkubwa kwa MSD hivyo,  ipo haja ya wadau wote kukaa pamoja na kuweka mpango wa pamoja wa kuyamaliza huku wakidhibiti yasijitokeze tena siku zijazo.

“Tunapaswa kuwa na mfumo wa pamoja utakaoifanya MSD kuwa imara kifedha. Kila taasisi ina wajibu wa kuhakikisha inalipa madeni yake kwa wakati ili kuimarisha huduma za afya kwa wananchi,” alisema Tayari.

Kwa upande wake, Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi alisema kuna umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa usimamizi wa madeni katika hospitali zote zinazohudumiwa na MSD.

Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea.

Alisema baadhi ya taasisi zimekuwa zikichukua bidhaa za afya kwa mikopo inayozidi uwezo wao wa kulipa, hali inayochangia kuongezeka kwa mzigo wa madeni ndani ya bohari hiyo.

“Ni muhimu sasa kuweka ukomo wa madeni kwa taasisi zinazopokea huduma za MSD pamoja na kuwa na ratiba maalumu za malipo ili kuzuia mrundikano wa madeni mapya,” alisema Msasi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai alisema hali ya madeni imeendelea kuathiri uwezo wa taasisi hiyo kufanya manunuzi ya dawa na vifaa tiba kwa wakati pamoja na kuwalipa wazabuni wake.

Alifafanua kuwa changamoto hiyo pia imeathiri uwezo wa MSD kujenga akiba ya kimkakati ya bidhaa muhimu za afya, jambo linaloweza kuhatarisha utoaji wa huduma wakati wa dharura au milipuko ya magonjwa.

“MSD ina jukumu kubwa la kuhakikisha dawa zinapatikana katika hospitali zote nchini. Hata hivyo, mtiririko hafifu wa fedha kutokana na madeni unaathiri utekelezaji wa jukumu hilo,” alisema.

Akichangia mjadala huo, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi alisema changamoto ya madeni haiwezi kutatuliwa kwa kuiangalia MSD pekee bali inahitaji tathmini ya mfumo mzima wa kifedha wa sekta ya afya.

Alisema gharama kubwa za uendeshaji wa hospitali zimekuwa zikichangia taasisi nyingi kushindwa kulipa madeni yao kwa wakati, hivyo kuhitaji mkakati wa pamoja unaoshirikisha serikali na wadau wote wa sekta hiyo.

Baadhi ya washiriki wa kikao hicho walikiri kuwa pamoja na dhamira ya taasisi nyingi kutaka kulipa madeni, changamoto za kifedha zimeendelea kuathiri uwezo wao wa kufanya hivyo.

Hata hivyo, kwa pamoja walionesha dhamira ya kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa suluhisho la kudumu ili kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Kikao hicho ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa Aprili 2, 2026 na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, wakati wa ziara yake katika makao makuu ya MSD, Keko Mwanga jijini Dar es Salaam, ambapo alizitaka hospitali na taasisi zote zinazodaiwa na MSD kuwasilisha mpango wa kulipa madeni yao ndani ya miezi miwili.