Fursa mpya za kiuchumi, ajira kwa wakazi wa Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera akiwa katika picha ya pamoja na walimu wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari visiwani Zanzibar waliofika mkoani humo kwa ajili ya ziara maalumu ya kutalii na kujifunza mambo mbalimbali ikiwamo masuala ya elimu.
Muktasari:
- Mradi huo unatarajia kukamilika Mei mwaka huu, ambapo utaufanya Mkoa wa Mbeya kuwa wa kisasa katika Wilaya za Mbeya Vijijini na Mjini na kuchochea fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi. Mradi wa upimaji ardhi waiva, kuibadili Mbeya kuwa ya kisasa, kiuchumi na ajira
Mbeya. Mradi wa upimaji ardhi katika maeneo ya Utengule na Nsalala uliokuwa chini ya Tanganyika Packers na TBC Iwambi mkoani Mbeya ambao ulianza Juni, 2024, unatarajia kukamilika Mei mwaka huu, huku ukitajwa kufungua fursa nyingi za kiuchumi na ajira.
Pia kukamilika kwa mradi huo utafanya Mkoa wa Mbeya haswa Wilaya za Mbeya Vijijini na Mbeya Mjini kuwa za kisasa, huku zikifunguliwa fursa mbalimbali ikiwamo viwanda, Ofisi za Serikali, kumbi za starehe, viwanja vya michezo, hospitali na chuo kikuu.
Pia kutakuwapo makazi bora ya watu, mashamba ya mjini ‘Urban Farms’, Maghala, stendi ya daladala, vituo vya afya, shule, machinjio na maduka ya biashara ‘Shopping More’ kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza leo Aprili 14,2025 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kukamilika kwa mradi huo kutaufanya mkoa huo kuwa wa kisasa zaidi akiwaomba wawekezaji wa ndani na nje kujitokeza kwa wingi kuichangamkia.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera akizungumza na waandishi wa habari kuelezea utekelezaji wa mradi wa upimaji ardhi unaoendelea mkoani humo ikitarajia kukamilika Mei mwaka huu.
Amesema utekelezaji huo ni hatua za makusudi kwa Serikali ya awamu ya sita kuupanua mkoa huo kimaendeleo na kuwafikishia wananchi huduma bora, akiomba wananchi walio karibu na mradi huo kutoa ushirikiano.
“Mbeya inaendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ina miji inayokua kwa kasi hivyo kuhitaji mipango ya ardhi na miundombinu bora”
“Mradi huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali kuimarisha mipango miji na matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ambapo Mbeya tunashiriki ikiwa ni sehemu ya juhudi za maendeleo ya kisasa” amesema Homera.
Ameongeza kuwa fursa hiyo ya kipekee inaiwezesha Mbeya kuwa ya mfano kwenye upimaji ardhi akieleza kuwa matarajio ya Serikali ni kuona Mkoa huo ukiwa kisasa zaidi kwa huduma bora.
Mmoja wa wadau wa maendeleo jijini Mbeya, Aurea Mwankota amesema mkoa huo ulichelewa kuwa na mazingira bora.
“Jiji la Mbeya ni tofauti na majiji mengine, huenda huo mradi ukaibadilisha na kuwa rasmi tunayoitaka, ila kwa ujumla ramani yake haikuwa na sifa za kuitwa Jiji kwa kuwa miundombinu yake bado hairidhishi” amesema Aurea.
Naye Benson Marcel amesema kila mwaka mkoa huo umekuwa na mabadiliko makubwa akieleza kuwa ni hatua chache ambazo zikiongezwa unaweza kuwa kivutio zaidi nchini.
“Kwanza Mbeya ipo karibu na nchi kama Zambia na Malawi hata DR Congo, hii hali yake ya hewa, milima ni vivutio vinavyoweza kuutangaza zaidi, mradi huo ukikamilika wawekezaji wakatumia fursa hiyo na utapiga hatua kubwa” amesema Marcel.