Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mnyukano Waziri Gwajima, Askofu Gwajima washika kasi

Mnyukano Waziri Gwajima, Askofu Gwajima washika kasi

Muktasari:

  • Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ameagiza kuitwa na kuhojiwa kwa Askofu Josephat Gwajima, huku akitaja sababu kuwa ni kuivuruga wizara na Serikali hasa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.


Dar/Butiama. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ameagiza kuitwa na kuhojiwa kwa Askofu Josephat Gwajima, huku akitaja sababu kuwa ni kuivuruga wizara na Serikali hasa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko-19.

Pia amemtuhumu kiongozi huyo wa kanisa la Ufufuo na Uzima na mbunge wa Kawe kutoa taarifa za uongo kwa viongozi wa Serikali kuhusu chanjo hiyo.

Hata hivyo, Mwananchi ilipowatafuta msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni wote walieleza kutofahamu taarifa hizo.

Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai alipoulizwa kwa simu alisema: “Sina taarifa, hivyo siwezi kutoa maoni kwa chochote.”

Katika siku za hivi karibuni, Askofu Gwajima amekuwa akisisitiza kuwa hatakubali kupatiwa chanjo ya Uviko-19 na kuwataka waumini wake kutojitokeza kwenda kuchanja.

Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Askofu Gwajima alijibu kwa ujumbe mfupi kwamba asingeweza kulizungumzia kwa sasa.

Wakati Askofu Gwajima akitoa kauli hiyo, Spika Ndugai amewaasa wabunge kujitokeza kuchanja na kwamba japo ni hiari, lakini hakuna hiari ya kuwaambukiza wengine ugonjwa huo.

Jana akizungumza katika kijiji cha Kyatunge wilayani Butiama, Waziri Gwajima alisema mara kadhaa Askofu Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha juu ya chanjo hiyo na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake, jambo ambalo limekuwa likileta mkanganyiko katika jamii.

“Gwajima ni ndugu yangu, ni shemeji yangu kabisa, lakini mimi ni waziri wa wananchi, nimekula kiapo cha kutumikia nchi yangu sio kumtumikia shemeji. Mimi ndiye msemaji wa masuala ya afya nchini si msemaji wa shemeji yangu, sasa nimechoka kuvurugwa, naelekeza majeshiyote, polisi na Takukuru waende wakatumie sheria zao wamuite, awaeleze maana amesema pesa, pesa, pesa,” alisema.

Dk Gwajima alifafanua kuwa sekta ya afya si ya kuchezewa, yeyote atakayejaribu kupotosha au kuvuruga mipango ya Serikali kupitia sekta hiyo lazima hatua kali zitachukuliwa bila kujali nafasi yake au uhusiano wake na mtu yeyote.

Pia, aligusia madai ya askofu huyo kuwa chanjo zilizoletwa nchini ni feki, hivyo kuagiza akamatwe ili aeleze zinakopatikana chanjo hizo.

Alisema yeye kama waziri yupo tayari kwenda kwa mkemia mkuu au maabara yoyote ya nchi jirani, ili kupima chanjo hizo zitakazoonyeshwa na askofu huyo.

“Mambo ya sayansi yanapingwa na sayansi, hivyo Askofu Gwajima anatakiwa kutoa uthibitisho wa kisayansi juu ya madai yake hayo, la sivyo hatua za kisheria lazima zichukuliwe,” alisema.

Waziri huyo aliwahimiza Watanzania kukubali kuchanjwa, kwani kupatikana kwa chanjo ya Uviko-19 mapema ni neema za Mungu.

“Watu wanasema mbona chanjo imepatikana haraka, wanasahau kuwa haya mambo ni ya kisayansi.

“Nawaomba tuukatae ugonjwa huu katika jamii kwa kukubali kuchanja wakati wataalamu hao wakiendelea na tafiti kwa ajili ya chanjo ya magonjwa mengine, lakini ikumbukwe ni sayansi ndiyo inayoongea, hakuna wa kupingana nayo,” alisema.

Alieleza kuwa Serikali haimuogopi mtu yeyote, bali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuongeza kuwa kabla ya kuanza kuruhusu Watanzania kuchanjwa, ulifanyika utafiti ili kujua usalama wa chanjo hiyo.

“Mnakumbuka chanjo ilianza kutolewa Desemba mwaka jana, lakini Tanzania hatukukimbilia kuchanja, tulikuwa bado tunataka kujiridhisha na baada ya kuridhika ndipo tukaanza kutoa chanjo mwezi uliopita. Tumejiridhisha kuwa huko kwa wenzetu hakuna mtu aliyebadilika kuwa zombi kama wasomi wa kwenye mitandao wanavyotuaminisha,” alisema.

Mpaka sasa Tanzania imepokea dozi milioni 1.05 za chanjo huku waliochanja hadi kufikia Agosti 14 ni watu 207,391.