Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mlipakodi alivyojichanganya treni ya SGR

Nimekaa zangu natafakari kodi ninazolipa kila siku zinakwenda wapi. Nikakumbuka maneno maarufu ya miaka ya hivi karibuni: ‘Miradi ya kimkakati’

Hiyo kwa miaka karibu 10 iliyopita ukiisikia maana yake ni reli ya kisasa (SGR), Mradi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na ununuzi wa ndege/kufufua shirika la ndege la Tanzania (ATCL).

Ndege hizo tangu mwaka 2016 nimezipanda na kupiga picha ndani yake na chakula chao ambacho huwezi kushiba, nimekula nikiwa angani.

Kwenye bwawa huko nako wanatuambia eti sehemu ya umeme tunaotumia nchini unatoka huko, hivyo kila muda huwa nawasha taa na kuzima ili kuhakikisha kodi zangu zinaleta umeme au ni ‘fiksi’ tu

Kuna wakati zinawaka kuna wakati nakuwa nimeishiwa luku zinagoma ila baadaye watu wakishangilia nje nikiwasha zinawaka.

Nikasikia treni ya kasi imefunguliwa, nikakumbuka kodi zangu tena. Nikasema lazima niipande hii ila nikaogopa nikasema acha kwanza izoee njia nisiwe chambo!

Mmhh ila mtandaoni picha za wanaopanda zikawa nyingi nikaitamani, nikasema acha niende Morogoro ‘nikale bata’ jioni nirudi nayo.

Juzi juzi hapa asubuhi kama saa 11 kasoro nikaomba gari kwa mtandao, ikaja IST  tukaanza kuelekea stesheni. Aaah yule dereva anapiga stori nyingi njiani, tukaanzia kwa RC wa Simiyu, tukaja kwa Mange, Komasava ya Diamond mpaka kwenye siasa tukafika.

Hanyamazi anasema yeye tu, kufika pale stesheni bado dakika 20 treni iondoke,  mzee akanikera  nikampa Sh15,000 nikasubiri buku yangu ya chenji mpaka ailete japo nilimuonea huruma maegesho yanavyosumbua nyakati za asubuhi.

Kufika pale wanaruhusiwa wenye tiketi tu nao wanaambiwa wawahi sisi tusionazo tukaanza kukaa  foleni kubwa na haiendi,  nikapata tiketi bado dakika 10, nikakaguliwa nikaanza kupanda ngazi.

Nakimbia nafika juu sehemu ya kupandia bado dakika saba nikaambiwa milango imefungwa nimechelewa, doh iliniuma nikaambiwa nyingine mpaka saa 10 jioni.

Najua wengi tuliozoea treni za kudandia, Hii ya SGR imetuacha sana. Mlango ukifungwa umefungwa basi, basi nikaenda nikashuka chini kinyonge nikaita gari, nikatafuta ‘indoo pabu’ moja Masaki nikaanza kushusha Yohana Mtembezi Lebo nyekundu ndiyo naweza kuimudu hiyo.

Baadaye nikaagiza na mishikaki kama 10 hivi huku nikiendelea kuagiza ‘aisi’ tu na coca kumpunguza nguvu yohana.

Ilipofika saa nane mchana nilikuwa siwezi kusimama kwa mguu mmoja, nikaita gari  huyo nikarudi stesheni, awamu hii nilifika saa moja kabla nikakata tiketi ya daraja la wananchi nimefika kwenye chuma  nikauchapa usingizi.

Baada ya saa moja na dakika 40, naambiwa tumefika muziki ukawa ni kutoka stesheni ya Morogoro mjini.

Kwanza usafiri wa shida, mie nikasaka boda Sh5, 000 ikanipeleka mjini ila nilikoma barabara mbovu mpaka kuiona Barabara ya Dodoma na pikipiki za Morogoro mkulima zile hadi maini yalitikisika.

Nikafika mjini nikatafuta sehemu ya kulala kisha nikaenda kiwanja kimoja karibu na Halmashauri ya Manispaa Morogoro nikaendelea Yohana mtembezi kama kawaida huku nikipata burudani ya muziki na kushuhudia michuano ya soka ya Euro 2024.

Karibu na asubuhi mie nikaenda zangu kulala peke yangu kabisa, nikachapa usingizi hadi saa saba mchana, nikaamka nikapata chakula kisha nikawa nasomasoma muswada wa bajeti na kupiga simu mbili tatu kwa familia na washikaji nikawaelezea safari yangu kwenye treni, inavyokimbia na kujali muda.

Kusema ukweli treni ni nzuri sana, mandhari safi kuanzia stesheni mpaka ndani ya treni kila kitu kinavutia hata wahudumu ni wa moto.

Nikasema sasa leo Yohana akae pembeni niishuhudie treni nikiwa ‘soba’, nikaingia kwenye simu yangu nikaunga bando la intaneti la wiki ambalo najua litaisha ndani ya siku moja nikaingia tovuti ya TRC ili kukata tiketi ya kurudi Dar saa moja  na nusu jioni.

Sistimu ikaniletea uzito lakini baadaye nikatoboa, nikasema zamu hii sikai kwa wananchi tena maana kule watu wananung'unika sana mara hii siti yangu mara ni yangu kunyanyuana kila saa, Nikasema sitaki uswahilini tena nitakaa daraja la juu (Business) kurudi Dar.

Nikachukua tiketi yangu ya Business behewa namba 2. Saa 11 hivi nikachukua bajaji kuelekea Airport. Nikamshukuru aliyenihudumia nilipolala na kumshukuru Mungu kuwa DC wa Morogoro mjini yeye hakuja kukatiza usingizi wangu usiku kufanya ukaguzi nimelala na nani.

Foleni ya kufika stesheni Kihonda inatia hasira, msongamano ni mkubwa na hamna utaratibu mzuri wa kuratibu magari basi nikashuka kwenye bajaji nikampa Sh7,000 yake nikaanza kuchapa mguu.

Nafika stesheni wananiambia licha ya kuwa nina tiketi ya kielektroniki, lazima nipate ya karatasi nikasema haya ni maajabu, karatasi tena ulimwengu wa digitali wakati tiketi zote zina QR code, nikatoa pole kwa miti inayotengeneza karatasi kisha nikaunga foleni ya kuchapisha tiketi.

Bana wewe kama una kitu chochote cha kunywa hakikatizi pale, sijui chakula inakuaje lakini hata maji hayaingii bila kujali ujazo, unaacha pale hata soda mpya labda baadaye na upya wake inatupwa mie sijui.

Nikafanikiwa bana nikapenya shwaa sehemu ya kusubiri kupanda, hapo wamerundikana watu kama 500 hivi halafu padogoo, ingekuwa wakati wa Uviko-19 sijui ingekuwaje.

Baadaye watu wa ‘business’ tukapata upendeleo tukaitwa sasa sisi hao, tukaawacha wananchi wa kawaida, tukapokelewa vizuri na kukagulia tiketi kisha kukaribishwa ndani.

Yale mambo ya hii ni siti yangu nikakutana nayo tena huku. Nimekaa mwenyewe wakaja wenye siti yao mhudumu akaniomba kwa kuwa wapo wawili kama nitaridhia anihamishe, maana hao ni washari kwa kuwa alitabasamu vizuri kabla ya kuniambia nikakubali wakakaa sijakaa sawa mwenye siti ya nilipohamishiwa akaja anataka siti yake.

Nikamwita mhudumu nikamwambia nirudishe kwangu haya ya kila saa kunyanyuliwa siyataki akaniambia tulia akaongea na aliyetaka kuninyanyua akamwambia nitayamaliza, kumbe bwana neno hilo wameambiwa wengi kesi zikawa nyingi.

Lakini baadaye tukapangwa upya bila kujali siti namba yako. Treni ilivyong'oa waliobakia wakapelekwa kule daraja la kwa wananchi, lakini hapana tofauti kubwa sana zaidi ya mpangilio wa siti na nafasi bila shaka walimaindi kidogo.

Nikajiuliza hawa TRC wanatumia mfumo gani, wao dijitali haijawasaidia mbona wanatoa uzoefu mbaya kwa watu mwanzoni ila nikakausha.

Alivyopita mhudumu nikatumia fursa hiyo kumsogelea nikamwambia samahani naomba nikuulize kitu sauti ya chini basi akaniinamia.

Nikamuuliza mbona hivi kila siku watu wanalalamika siti kugongana akajibu itakuwa tatizo la mfumo, nikamwambia sawa lakini unapaswa kufanyiwa kazi. Mpaka sasa nakumbuka namna yule binti alivyokuwa akinukia vizuri.

Basi nikajiegesha nipunguze usingizi ila nikaamshwa na kuzima na kuwaka kwa taa kila baada ya muda zinazima na kuwaka tena ndani ya muda mfupi.

 Mimi muoga nikaenda kwa msimamizi ya behewa letu nikamuuliza mbona taa zinazima na kuwaka akasema umeme unakuwa umebadilika, hali hiyo hutokea kila laini ya umeme inapobadilika.

Nilipotoka nikapita maliwatoni kidogo. Ni kubwa na safi kama hotelini nikasema hapa abiria tu wasije wakaharibu miundombinu hii, japo maelezo ya kuflashi inabidi uwe msafiri mzoefu kama mimi kuweza kuyaelewa la si hivyo unaweza kuacha mzigo juu.

Kwenye behewa hamna kelele za kuku wala harufu za mahindi kama kwenye treni itokayo kwa bibi yangu Kigoma lakini matangazo ya kwenye SGR ni vichekesho.

Wazungumzaji nafikiri ni wanafunzi wa lugha zote, Kiswahili na Kiingereza wanabagaza sana, yaani wanapiga kelele tu. Nafikiri tulipe kodi zaidi ili waajiri watangazaji wazuri wa kutoa taarifa za mara kwa mara kwenye safari au ATCL wawaazime hawa jamaa kupata uzoefu.

Kwa matangazo yanayofanana, nafikiri yangerekodiwa na watu wenye utaalamu na mambo hayo sio hawa wachekeshaji wa waliopo sasa.Hapana. Si kila mtu anaweza kuzungumza na umma kama hajanolewa vizuri.

Baada ya kukerwa na watangazaji wa ndani ya treni wasiojua lugha na matamshi nikapata kiu nikaagiza ka lite wakaniambia hakapo kuna bia aina mbili tu na wine aina moja doh zote situmii. Nikauliza iwapo kuna bar au mgahawa wakasema hamna basi nikaegeshwa kichwa.

Mhudumu akaniambia vitu vingi vilikuwepo lakini vimeisha. Moyoni nikajisemea wanaotoka Dar kuja Moro labda ni wanywaji sana wamemaliza stoku yote ya TRC, itabidi waongeze ukubwa wa stoo yao sasa.

Lakini chuma inatembea bana wakati najiandaa kuchukua namba mahali fulani ghafla tumefika, hawa jamaa hawana kuchelewa kama wale wenzao wa angani.

Niliposhuka Dar nikagundua SGR ikichanganya stesheni ya Dar haitoshi ni finyu labda ijengwe nyingine kubwa nje ya mji, ngazi mbili nyembamba ni kubanana kushuka, vyoo vichache nje ni kama soko.

Nikajisemea Serikali na TRC wote ni wasikivu haya ambayo wengi hawajayapenda juu ya huduma hii nzuri na muhimu kiuchumi, yatafanyiwa kazi.

Kwa sababu ya msongamano, nikatembea kwa mguu hadi mwendokasi ili nikabanane vizuri sasa nikielekea nyumbani.

Baada ya SGR, hapa nataka niangalie na miradi mingine, nione inavyokula kodi yangu. Nitaionja!