Mkuu wa Operesheni Jeshi la Polisi Mtwara afariki dunia

Mkuu wa Operesheni Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, Emmanuel Garuyamoshi enzi za uhai wake
Mtwara. Mkuu wa Operesheni Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara, Emmanuel Garuyamoshi amefariki dunia Aprili 9,2025 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni Ndanda.
Taarifa za kifo chake zimetolewa leo Aprili 10, 2025 na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Camillius Wambura katika kurasa za mitandao ya kijamii ya jeshi hilo.
“Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura anasikitika kutangaza kifo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Emmanuel Christian Gariyamoshi, Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Mtwara kilichotokea Aprili 09, 2025 saa 11:00 asubuhi katika Hospitali ya Misheni Ndanda Wilaya ya Masasi alikokuwa akipatiwa matibabu,”imeeleza taarifa hiyo.
Kabla ya kupangiwa kazi mkoani Mtwara, ACP Gariyamoshi aliwahi kuwa Oparesheni Ofisa wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, na pia alitumikia kama Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa taratibu na ratiba ya mazishi zitatolewa baadaye.