Mke adaiwa kumuua mumewe kwa kumkata shoka kichwani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo
Muktasari:
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alifariki kutokana na majeraha makubwa ya kukatwa na shoka kichwani, ambayo yalisababisha kutokwa na damu nyingi. Hata hivyo, chanzo halisi cha tukio hilo bado hakijabainika na upelelezi unaendelea. Mtuhumiwa amekamatwa na atapelekwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Arumeru. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Sofia Ernest Kimaro (48) mkazi ya kijiji cha Ushili wilayani Arumeru kwa tuhuma za kumuua mumewe Estomii Nnko (59) kwa kumkata na shoka kichwani.
Akizungumzia tukio hilo leo Februari 8, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo amesema kuwa mauaji hayo yamefanyika jana alfajiri katika Kijiji cha Ushili kilichopo wilayani Arumeru.
Amesema kuwa wanamshikilia mke wa marehemu kwa tuhuma za kutekeleza mauaji hayo kwa upelelezi, kabla ya kumfikisha mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
"Uchunguzi wa awali unaonyesha marehemu amefariki kutokana na kutokwa damu nyingi baada ya kujeruhiwa kwa kukatwa na shoka eneo la kichwani.
"Hata hivyo, chanzo halisi cha utekelezaji wa tukio hilo haijafahamika na upelelezi wa jeshi letu unaendelea, baadaye mtuhumiwa atafikishwa mahakamani," amesema.
Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha, kwa ajili ya kusubiri taratibu za kifamilia kuuhifadhi.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ushili, Mathias Timothy amesema kuwa walipata taarifa asubuhi ya Februari 7, 2024 baada ya kusikia kelele za kilio cha mke wa marehemu baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Ameongeza kuwa kutokana na ujirani wao, aliwahi kufika na kushuhudia marehemu akiwa amelala sakafuni kwenye dimbwi la damu akiwa ameshafariki.
"Baada ya kuona hivyo nilipiga simu Polisi ambapo walikuja na kufanya mahojiano na mke pamoja na mtoto wa kiume wa marehemu anayesoma kidato cha pili na baadaye kuondoka nao wakituhumiwa kushirikiana kutekeleza mauaji hayo," amesema Timothy.
Akielezea tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Elirehema Swai, amesema kuwa mauaji hayo yametokana na ugomvi uliotokea siku moja kabla ya tukio hilo.
"Siku moja kabla walikuwa na ugomvi baada ya baba (marehemu) kumpiga mtoto wao mkubwa wa kiume akimtuhumu, kuiba mahindi mabichi shambani kwa watu na kwenda kuuza mjini.
"Baada ya kutokea kwa wizi huo, huyu baba aliitwa ofisi ya kijiji kama mzazi na kuelezwa juu ya wizi wa mazao shambani iliofanywa na mwanaye na kisha kupigwa faini," amesema.
Baada ya kupigwa faini hiyo, Swai amesema kuwa marehemu alikubali kubeba dhambi za mwanaye na kuahidi kulipa baada ya siku mbili.
"Jioni aliporudi nyumbani alimkuta mtoto aliyetuhumiwa kuiba mahindi na ndipo alianza kumpiga, jambo ambalo mkewe hakulifurahia hivyo kuzua ugomvi mkubwa na baadaye alienda kulala, kabla asubuhi kusikia tukio hilo," amesema Swai.