Mkandarasi apewa siku 36 kukamilisha Daraja la Mkuyuni
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa daraja la Mkuyuni jijini Mwanza.
Muktasari:
- Daraja hilo lililopo katikati ya barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga limekuwa kero kwa watumiaji wa barabara hiyo pindi linapofurika mvua zinaponyesha na kusababisha msongamano wa magari na wakati mwingine watu kulazimika kupita ndani ya maji machafu.
Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amempa siku 36 mkandarasi Jasco Co. Ltd anayejenga Daraja la Mkuyuni lililopo mkoani Mwanza kumaliza ujenzi huo kuanzia leo Desemba 11, 2025 hadi Januari 15 mwakani atakaporudi kulizindua.
Maagizo ya Ulega yamekuja zikiwa zimepita siku chache tangu Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kumuelekeza kukutana na kumuuliza mkandarasi huyo anamaliza lini ujenzi wa daraja hilo wakati akizungumza na wakazi wa Jiji la Mwanza Uwanja wa Nyamagana, Desemba 5, 2025.
Daraja hilo limekuwa kero kwa watumiaji wa Barabara Kuu ya Mwanza-Shinyanga ambao wakati mwingine wanalazimika kupita ndani ya maji machafu mvua zinaponyesha na maji kufurika.
Hata hivyo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) iliamua kulibomoa na kulijenga upya ili kumaliza tatizo la mafuriko yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kulikagua, Ulega amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha ujenzi hadi Januari 15, 2026 baada ya kumuuliza atakamlisha lini na mkandarasi kutaja tarehe hiyo.
“Kwanza nimetumwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mlimsikia alipopita aliniagiza nije na mimi nimetii maelekezo ya kwamba nije kusukuma Daraja la Mkuyuni…nimeona hii kazi nataka nisikie kwa mkandarasi ni lini unakamilisha mradi huu?" alihoji Ulega.
Akijibu swali hilo Meneja wa Jasco, Sundeep Bachu amesema mpaka sasa mradi huo upo asilimia 75 na kuahidi kuwa itakapofika tarehe hiyo ujenzi utakuwa umekamilika kwakuwa wapo nyuma kwenye utekelezaji kwa asilimia 14 pekee.
“Tumekuwa nyuma ya muda kutokana na changamoto ya ucheleweshaji wa kuondolewa kwa miundombinu ya maji, umeme, mawasiliano pamoja na udhaifu wa tabaka la chini la msingi wa daraja kupelekea kuongezeka kwa kina cha daraja,” amesema.
Nakuongeza, “Pamoja na changamoto hizo mpaka sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kuanza uwekaji wa tabaka la lami kwenye barabara, nguzo za daraja. Tunatarajia ifikapo Januari 15, 2026 daraja hili litakamilika,”.
Diwani wa Kata ya Mkuyuni, Richard Daraja hili amesema daraja hilo lipo katikati ya njia inayoingia na kutoka jijini Mwanza na kwamba maji yakifurika yanasimamisha uchumi wa wakazi wa maeneo hayo pamoja na kusababisha foleni za magari kwa wanaoingia na kutoka katikati ya jiji hilo.
“Daraja hili limechangia mdororo wa kiuchumi katika maeneo haya hususani wafanyabiashara kama unavyoona kuna benki hapa, kituo cha mafuta na soko,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema pamoja na changamoto zilizosababisha ujenzi huo kuchelewa, lakini wananchi wananchotaka ni daraja hilo kukamilika ili waendelee na shughuli zao ikiwemo biashara ndogo ndogo.
“Changamoto tunazijua sisi viongozi lakini hawa wananchi wa mkuyuni na wananchi wengine wanaotumia barabara hii hao wenyewe hawayajui wanachohitaji ni barabara ikamilike uchumi wa hapa ufunguliwe na wananchi waweze kupita kwa amani,”amesema Makilagi.
Mkazi wa Mkuyuni, Issa Shija ametaja baadhi ya madhara ya maji kufurika eneo hilo ni maduka kujaa maji, bidhaa za wafanyabiashara kuharibika na wengine kukimbia maeneo ya biashara kutokana na hasara wanayoipata.
“Wangetengeneza hata mifereji kwakuwa watu wanapata adha sokoni, biashara zao haziendi maduka yanajaa maji..kuna wengine hata biashara zao wamekimbia maji yanatwama hadi kwenye viuno,”amesema
Mkazi mwingine, Shabani Kassimu amesema wamefrahi daraja hilo kujengwa akitaka mkandarasi atatue kero ya vumbi katika barabara inayotumika kwenye ujenzi pamoja na barabara ya muda inayotumiwa na wakazi wa jijni humo wakati ujenzi ukiendelea.
Awali, akitoa taarifa kwa Ulega, Meneja wa Tanroads mkoani Mwanza, Paschal Ambrose amesema daraja hilo linalojengwa upana wa mita 15 na njia sita (nne za magari na mbili za watembea kwa miguu) kwa zaidi ya Sh5 bilioni, ujenzi ulianza Novemba 13, 2024 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 13, 2025 lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza wamemuongezea mkandarasi muda.
Hatahivyo, Waziri Ulege amemtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha ujenzi huo pamoja na kuondoa changamoto za vumbi wakati akitekeleza mradi huo kwa kumwagia maji barabara za muda zinazotumika mara kwa mara.
“Hakikisheni hayo maji yanayolalamikiwa yanakwenda katika miundombinu ya watu ikiwa pamoja na masoko mnatengenezea njia yake, lazima yale maji yapate muelekeo wa kwenda kwenye njia yake badala ya kwenda kwenye shuguli za watu kujitafutia ridhiki zao,”amesema.