Mkakati kusaidia watumiaji wa ARVs

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCop) Dk Anath Rwebembera akizungumza katika kikao cha kuelezea mradi wa Afya Thabiti unaotekelezwa na Shirika la Amref Health Afrika.
Muktasari:
Shirika la Amref Health Africa, Tanzania limekuja na mradi wa Afya Thabiti ambao pamoja na mambo mengine, unalenga kuwafuatilia watu walioacha dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARVs) ili waendelee kupata huduma hizo.
Dodoma. Utaratibu wa kutoa dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) kwa kipindi cha kati ya miezi mitatu hadi sita, umechangia kupunguza changamoto ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) wanaoacha kwenda katika vituo vya afya kuchukua dawa hizo.
Mkurugenzi wa Mradi wa Huduma na Matibabu ya VVU (Afya Thabiti), unaotekelezwa na Shirika la Amref Health Africa, Tanzania, Dk Edwin Kilimba ameyasema hayo katika mazungumzo ya heshima na utambulisho wa mradi huo kwa Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Amesema changamoto ya walio katika matibabu ya VVU, kuacha kwenda katika vituo vya kutolea huduma ni kubwa na inaendelea nchini.
Amesema changamoto hiyo inatokea kwa sababu ya unyanyapaa ambapo mtu huogopa ndugu pamoja na marafiki zake kujua hali yake ya kiafya.
“Kazi kubwa ya mradi ni kufuatilia walipo vijijini, majumbani kwao na kuhakikisha kuwa wanaendelea kupata huduma hizo. Ni ile elimu inayowafanya watambue wasipotumia dawa ama wasipofuatilia huduma wanajiumiza wenyewe wala hawamuumizi ndugu wala mtu mwingine,” amesema.
Amesema wapo baadhi ambao wanawapa namba ama anuani ambazo haziko sahihi ili wasiweze kupatikana wanapowatafuta.
Dk Kilimba amesema kwa sababu wanafanya kazi na wenyeji na vijiji wanapotoka watu hao, wakipata elimu na kuelewa wanarudi katika matibabu.
Amesema sasa hivi kuna mbinu mbalimbali zinazoruhusu wateja kutofika kliniki kwa miezi mitatu hadi sita iwapo mteja anaendelea kiafya na ikitokea katikati akaugua basi hurejea hospitali.
Hata hivyo wanaopata huduma hiyo ni wale ambao wataalam wa afya wamehakikisha hawana magonjwa nyemelezi na kiwango vya VVU kimepungua kwa kiasi kikubwa.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCop), Dk Anath Rwebembera amesema Serikali imeendelea kufanya kazi na wadau kutekeleza afua mbalimbali za kiafya, kuboresha miundombinu na kutoa huduma za afya kwa walengwa.
Amesema ingawa tafiti zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi mapya kwa vijana kinashuka, lakini bado wanapokea wagonjwa wapya na kuwataka Amref wanapokwenda katika mikoa hiyo kulitazama kundi hilo pia.
Mradi huo wa miaka mitano ulioanza Oktoba mwaka jana na kutarajiwa kumalizika mwaka 2028, unafanyika katika mikoa ya Simiyu, Mara kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Lengo la mradi huo ni kuimarisha utoaji wa huduma na matibabu ya kufubaza VVU katika kliniki za VVU/Ukimwi za Serikali na za hospitali teule ili kuongeza kasi ya kufikia malengo ya 95-95-95 ya kudhibiti Ukimwi nchini.