Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkakati kunufaisha wakulima wa Pareto waja

Musa Malubalo ,Ofisa  Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) mikoa ya Mbeya na Songwe  akielekeza namna bora ya uchumaji wa maua kwa wakulima wa zao hilo Wilaya ya Mbeya vijijini .Picha na Hawa Mathias.

Muktasari:

  • Miradi hiyo itajengwa  katika Mikoa ya Mbeya na Songwe kwenye Wilaya za Ileje na Mbeya vijiji kupitia  Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) na mashirika binafsi baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto ya ukaushaji  wa maua ya pareto na  kusababisha kupata unyevu na kupunguza ubora.

Mbeya. Wakulima wa Pareto  13,000 Wilaya za Mbeya na Ileje mkoani Mbeya na Songwe, watanufaika na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kukausha maua itakayojengwa na kampuni ya Pareto Tanzania (PCT), kwa kushirikiana na wadau ili kusaidia kuzalisha kwa ubora unaoendana na masoko.

Akizungumza na Mwananchi digital leo Jumanne, Mei 16 ofisini kwake, Ofisa Pareto mikoa hiyo, Mussa Malubalo; amesema hatua hiyo imekuja baada ya kubaini wakulima kuchuma maua na kukosa vifaa vyenye teknolojia za ukaushaji, vinavyosababisha unyevu, unaopunguza ubora.

“Unajua zao la Pareto linahitaji kiwango kizuri cha utunzaji kwenye joto na ukaushaji, tumebaini changamoto inayosababisha wakulima kuzalisha chini ya kiwango, ni ukosefu wa vifaa; ikiwepo miundombinu ya kuanikia na kukaushia maua. Sasa tumekuja na na mwarobaini huo,” amesema.

“Ukaushaji usiozingatia kanuni umekuwa mwiba mkali kwetu, kwani asilimia kubwa ya Pareto inaharibika na unyevu, ili tusiharibu masoko tunalazimika kuboresha na kutumia gharama kubwa na ndipo tunaingiza sokoni,” amesema.

Amesema zao la Pareto kwa bara la Afrika, Tanzania inashika nafasi ya kwanza huku likishika nafasi ya pili kwa uzalishaji kidunia. Kwamba zao hilo kwa Tanzania hutegemea masoko nchini Marekani kupitia kampuni ya MGK na ndio sababu kuhakikisha zao hilo linaboreshwa kwa lengo la kulitangaza zaidi.

“Kila mwaka tunasafirisha tani 3,000  kwenda katika soko nchini Marekani wakati  mahitaji ni tani 3,500  ili kuwezesha wakulima kuzalisha kwa tija, tunawasaidia kuondoa vikwazo kwa kufanyia maboresho changamoto zao sambamba na kuwaeleza madhara ya kuuza maua mabichi kupitia kwa mawakala,” amesema.

Msimamizi na mdhibiti wa mazao mikoa ya nyanda za juu kusini kutoka Bodi ya Pareto Tanzania, (TPB) Edwin Margwe amesema kuwa Serikali imepiga marufuku makampuni kununua Pareto mbichi na watakaobainika awamu ya kwanza wataonywa na wakirudia watafutiwa leseni na kulipa faini ya Sh1 milioni au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja.

“Tayari zipo sheria na kanuni ambazo zinaelekeza endapo kampuni ikakiuka mkataba hatua zinachukuliwa sambamba na wakulima kuwajibishwa endapo watabainika kuuza maua mabichi,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo Wilaya ya Mbeya, Gidion Mapunda, amesema ili kufikia malengo wameweka mikakati ya kuendelea kutoa elimu na kupiga marufuku uuzaji holela wa maua ambayo hayajakomaa.

Mkulima wa Pareto Wilaya ya Mbeya, Noel Bukuku amesema changamoto kubwa ni uchumi duni miongoni mwao na hivyo kujikuta wakichuma maua ambayo hayana ubora na kuuza kwa wanunuzi wanaofuata mashambani.

“Kimsingi tunashukuru sana kampuni ya pareto imekuwa mstari wa mbele kutupatia elimu ya namna bora ya kuandaa na kukausha kwa ubora na kupata masoko   ya uhakika,” amesema.