Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mjamzito asimulia ‘malaika’ mwokoaji alivyomnusuru na kifo

Muktasari:

Grace Elisha (27), mkazi wa Kijiji cha Bwisya, kisiwa cha Ukara ameeleza jinsi alivyonusirika katika ajali ya kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere katika mazingira ambayo binafsi mpaka sasa anaona ni kama muujizi umetendeka wa mungu kumshushia ‘malaika’ aliyemwokoa kwenye ajali hiyo ambapo ni watu 41 tu ndio waliookolewa huku wengine 230 wakipoteza maisha majini.

 


Kuna sababu nyingi zinazodaiwa huenda zilikuwa chanzo cha ajali ya Mv Nyerere iliyopinduka Septermba 20, mwaka huu ikiwa hatua chache kutia nanga katika gati ya Kijiji cha Bwisya kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe.

Baadhi wanadai kitendo cha aliyekuwa nahodha wa meli hiyo, marehemu Constatine Mahatane kutumia muda mwingi kuzungumza na simu yake ya kiganjani ni moja ya sababu.

Wapo pia wanaodai naodha huyo hakuwa amefuzu mafunzo ya uendeshaji chombo cha majini, kukosa uzoefu au hakuwa na sifa za kuongoza chombo bila ya usimamizi.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali ya Mv Nyerere, wanadai kivuko hicho kilipinduka baada ya kukosa uwiano kutokana na nahodha kukata kona ya ghafla alipogundua chombo chake kilikuwa kimeacha uelekeo wa gati ya Bwisya.

Nahodha angeweza kuepusha ajali

Akizungumzia kivuko kukata kona ghafla, Nahodha wa meli ya Mv Nyehunge, Mabula Luchanganya anasema iwapo nahodha aliyekuwa akikiongoza chombo angekuwa makini kwa kiasi kidogo tu kwa kuepuka kukata kona ghafla, chombo hicho kisingepinduka.

“Nahodha makini hawezi kukata kona ghafla, kwa kasi anapoongoza

chombo kilichojaza abiria na mizigo. Hata baada ya kugundua ametoka

kwenye uelekeo wa gati, angeweza kukata kona taratibu na kuruhusu chombo kutia nanga salama pembezoni mwa gati,” anasema.

Akifafanua, Kapteni Luchanganya anasema kutokana na ufinyu wa eneo la gati ya Bwisya na Bugorola, nahodha anatakiwa kuwa makini kwa kuanza kuelekeza chombo kwenye uelekeo sahihi kuanzia umbali wa kilomita mbili kabla ya kutia nanga.

“Baada ya kugundua kosa hilo, nahodha alitakiwa kuwa mtulivu kwa kuruhusu chombo kutia nanga hata nje ya gati kwa sababu pwani ya kijiji cha Bwisya imekaa vema kiasi cha kuruhusu kivuko kutia nanga nje ya gati. Chombo na abiria wangebaki salama,” anasema Luchanganya.

Sababu za meli, kivuko kupinduka

“Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuchangia ajali ya chombo ndani ya maji. Uwiano hasi unaotokana na

kujaza abiria, mizigo na upangaji usiaozingatia kanuni ya usalama ni kati ya sababu zinazoweza kupindua chombo,” anasema Luchanganya.

Anasema ili kuweka uwiano sawa, nahodha na wasaidizi wake ndani ya meli au kivuko wanapaswa kuhakikisha uzito wa mizigo unakuwa chini ya chombo kabla ya kujaza maeneo mengine ya juu.

“Nahodha makini unatakiwa kuhakikisha abiria kwanza wanajaa kwenye eneo la chini ya chombo tena wakiwa wameketi vitini. Uzito mkubwa unapokuwa eneo la chini huongeza usalama wa chombo majini,” anasema.

Akitoa maoni yake kuhusu sababu za kupinduka kwa kivuko cha Mv

Nyerere, Kapteni Luchanganya alitaja mambo mawili. Mosi ni kujaza

abiria na mizigo kupita kiasi na nahodha kukosa umakini.

Sababu nyingine inayoweza kusababisha meli au chombo cha majini kupinduka au kuzama ni hitilafu ya kiufundi pamoja na chombo kutoboka.

Mkanganyiko uwezo, ujuzi wa nahodha

Kati ya mambo ambayo hadi sasa yameibua sintofahamu ambayo huenda jibu likapatikana baada ya uchunguzi wa vyombo vya dola na kamati maalumu iliyoundwa na Serikali ni uwezo kiutendaji, elimu na ujuzi wa aliyekuwa nahodha wa Mv Nyerere Constantine Mahatane wakati kivuko kikipinduka.

Wakati anayetakiwa kuongoza kivuko au meli yenye hadhi kama Mv Nyerere anatakiwa kuwa na kiwango mahususi cha elimu ya masuala ya unahodha na ubaharia kuanzia (Master Near Coast Deck Officer Class 4) marehemu Mahatane alikuwa na elimu ya (Deck ratings).

Elimu hiyo aliipata mwaka 2014 kutoka Chuo cha Ubaharia cha Dar es Salaam Maritime Institute (DMI), jinini Dar es Salaam.

Mmoja wa waliosoma naye kozi hiyo, Salum Adam anathithibisha kuwa licha ya kuwa na uwezo wa kuongoza chombo, kiwango chao cha elimu na majukumu ya wenye elimu ya ubaharia Deck ratings

hayawaruhusu kuongoza chombo bila uangalizi na usimamizi wa nahodha.

“Nimesoma kozi moja na Mahatane pale DMI, mwaka 2014. Kwa elimu hiyo tunaruhusiwa kuongoza chombo lakini chini ya uangalizi na usimamizi wa nahodha ambaye ni lazima awepo ndani ya chombo wakati,” anasema Adam.

Adam ambaye ni baharia katika meli ya Mv Nyehunge inayosafirisha abiria na mizigo kati ya Nansio, Ukerewe na jiji la Mwanza anasema mwenye alimu kama yake na Mahatane anaruhusiwa kuongoza chombo baada ya kujiendeleza na kupata uzoefu wa kutosha.

“Hatua ya elimu tuliyofikia inafikiwa baada ya mafunzo

mengine ya awali ya ubaharia. Kwa kiwango hicho cha elimu na

mafunzo, baharia anaweza kuendesha chombo lakini chini ya uangalizi

wa nahodha ambaye sharti awemo ndani ya chombo wakati wa safari,” anafafanua.

Hata hivyo, akizungumzia elimu na uwezo wa nahodha huyo, Jumapili iliyopita Mhandisi wa Mv Nyerere, Alphonce Charahani alisema Mahatane alihitimu kozi ya unahodha na alikuwa amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 10, hivyo hakuwa ‘deiwaka’ kama inavyodaiwa na kwamba siku ajali ilipotokea alikuwa zamu.

Aina za ajali

Kwa mujibu wa Timothy Hosea ambaye ni Nahodha Msaidizi wa Meli ya Mv Nyehunge, kuna aina mbili za kuzama kwa meli. Kwanza ni kupinduka kwa kulala ubavu au juu chini kutokana na kukosa uwiano na pili ni kuzama kunakosababsihwa na chombo kutoboka kwenye kitako, hivyo kuruhusu maji kuingia ndani ya meli kupita kiwango kinachoweza kuhimilika.

Kwa upande wake Mhandisi wa Meli ya Mv Nyehunge, Said Mohammed mbali na sababu zilizotajwa aliongeza ya tatu inayoweza kusababisha chombo cha majini kupata ajali ni kugongwa na kitu chochote kutokea nje.

Ukara wataka gati ipanuliwe

Akizunguma katika mahojiano maalumu kijijini Bwisya, mmoja wa wananchi, Teokeles Majura aliiomba Serikali kujenga upya na kuipanua gati ya Bwisya ambayo udogo wake unadaiwa kuwa chanzo cha ajali.

“Kwa mujibu wa mashuhuda, miongoni mwa sababu za ajali ni nahodha kukata kona kwa kasi na ghafla baada ya kuona chombo kinaacha uelekeo. Gati ingekuwa kubwa nahodha asingelazimika kukata kona ghafla,” anasema Majura.

Mjamzito aliyeponea tundu la sindano

Kama kuna watu wanaweza kusimulia miujiza na kumshukuru Mungu kuhusiana na tukio la ajali ya kivuko cha Mv Nyerere basi Grace Elisha (27), mkazi wa Kijiji cha Bwisya, kisiwa cha Ukara atakuwa mmoja wao. Huyu ni kati ya watu 41 pekee waliokolewa wakiwa hai katika ajali hiyo.

Akizungumza alipohojiwa na Mwananchi, Grace ambaye ni mama wa watoto wawili, Jenipher Madaraka (3) na Catherine Madaraka (2) anasema bila muujiza wa Mungu, angekuwa miongoni mwa marehemu.

“Nilitoka nyumbani kwangu asubuhi ya Septemba 20, kwenda Bugorola kuhemea mahitaji ya nyumbani. Nikiwa njia kurejea nyumbani ndipo janga hili lilipotokea na kuangamiza watu wengi,” anasema Grace.

Akisimulia, manusura huyo anasema “Ikiwa inakaribia kutia nanga katika gati ya Bwisya huku baadhi ya watu wakijiandaa kuteremka, ghafla meli (kivuko) iliyumba na nikajikuta nimetumbukia ndani ya maji”.

Anasema akiwa majini huku akijitahidi kujiokoa kwa kuogelea, alibamizwa mgongoni na pikipiki iliyorushwa kutoka ndani ya kivuko, hali iliyomsababishia maumivu na kupoteza nguvu na uwezo wa kujiokoa.

Kutokana na kutapatapa huku akipiga kelele za kuomba msaada, mmoja wa abiria wa kiume ambaye naye muda huo alikuwa kwenye hekaheka za kujiokoa aliogelea hadi alipo na kumwelekeza amshikilie mguu ili wajiokoe pamoja.

“Kutokana na hofu ya kifo iliyoniingia, nilijikuta nikimshika mguu kwa nguvu kiasi cha yeye kushindwa kuogelea. Kitendo hicho kilimfanya anipige teke kujiokoa asizame pamoja nami,” anasema na kuongeza

“Baada ya kuogelea na kusogea mbali kidogo kutoka nilipokuwa, mwanaume yule aliingiwa imani jinsi nilivyokuwa natapatapa majini nikiomba msaada, alirejea nilipo na kunisihi nijikaze kusubiri waokoaji (wavuvi) ambao tayari walikuwa wameshaingia majini kukielekea kivuko”.

‘Malaika mwakoaji’

“Nikiwa nimechoka na kuishiwa nguvu huku mawazo na hofu ya kifo ikianza kunijaa, ghafla nilimwona kaka Bishompa Sendema akiwa anatumia boya kuogelea kujiokoa. Nilipiga kelele nikimwita jina ndipo alipogeuka na kuniona natapatapa majini,” anasimulia Grace mwenye ujauzito wa miezi saba.

Anasema kelele hizo zilimfanya Bishompa Sendema (36) kugeuza boya na kuogelea kumfuata ambapo baada ya kumfikia alimtaka kujishikilia kwenye boya hilo.

“Baadaye alianza kuogelea kumfuata binti mwingine ambaye pia alikuwa akitapatapa majini na kumtaka pia ashikilie boya kwa nguvu. Tukiwa watatu kwenye boya, Bishompa akaogelea kumfuata mwananume mwingine aliyekuwa akizama na kwa pamoja akatutaka kushikilia boya kwa nguvu,” anasema.

Kutokana na kushikilia boya hilo, Bishompa alifanikiwa kuogelea hadi ufukweni na kuwaokoa wote watatu “Nilimuona ni kama malaika aliyetumwa aje kuniokoa kwa kweli sikuamini”.

“Kutokana na kazi kubwa ya kuokoa watu watatu, Bishompa alianza kuishiwa nguvu naye kuokolewa na boti za wavuvi waliokuwa wamefika tayari kutoa msaada,” anasema.

Anasema “Wakati natapatapa huku nguvu zikiniishia, hofu ya kifo iliniingia nikaanza kuwaza jinsi ninavyowaacha watoto wangu ambao bado ni wadogo, mume wangu na mama yangu mzazi,” anafichua Grace.

Anaongeza; “Hata suala la kufa na mtoto wangu mwenye umri wa miezi saba tumboni pia liliniumiza sana moyoni wakati naanza kuishiwa nguvu za kujiokoa”.

Hata hivyo usemi usemao kila mmoja na siku yake ya kufa imetimia katika familia ya Grace ambaye licha ya kuponea tundu la sindano, lakini amejikuta akipoteza shemeji zake watatu aliokuwa nao ndani ya kivuko cha Mv Nyerere.

“Ndani ya meli (kivuko) tulikuwa ndugu watano. Mimi, mama yangu mzazi pamoja na shemeji zangu watatu. Mama amepona lakini shemeji zangu wote wamekufa kwenye ajali,” anasimulia.