Mitaro ya maji taka kero katikati ya jiji Dar

Muktasari:
- Jiji la Dar es Salaam licha ya kuwa maarufu lakini lina changamoto zake katika baadhi ya maeneo ambazo zimekuwa kero kubwa kwa wakazi wake.
Dar es Salaam. Achana na maeneo kama Buguruni, Manzese na mengineyo ambayo miaka ya nyuma yalikuwa yamezoeleka kwa uchafu wa mazingira na kusababisha harufu mbaya.
Kwa sasa baadhi ya mitaa iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam nako kumeibuka kero ya harufu mbaya ya kinyesi inayosababishwa na kuziba kwa chemba za maji taka ambayo ni kero kubwa kwa wananchi.
Hii inatokana na kuwepo kwa miundombinu isiyokidhi mahitaji ya jiji hilo, moja ya chemba ya majitaka katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Bibi Titi, Dar es Salaam ambayo imefurika na kuwa kero kwa watumiaji wa maeneo hayo kwa zaidi ya wiki mbili mfululizo.

Uwepo na chemba hiyo ya majitaka pamoja na mvua zinazoendelea kwa sasa jijini Dar es Salaam, zimechangia kufurika kwa chemba hiyo hivyo majitaka kuchanganyika na ya mvua, na kusababisha maji machafu kuenea barabarani yakiambatana na harufu mbaya.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Everlasting Lyaro, amesema anafuatilia jambo hilo.
“Naomba nilifuatilie jambo hili kwa eneo ambalo umenitajia,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi, leo Aprili 23, 2025 Vicent Haule ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE), amesema hali hiyo ni ya muda hivyo inawalazimu wakati mwingine kupita kwenye jengo la biashara la City Mall lililopo jirani na barabara hiyo.
“Ufinyu wa njia hatuwezi kupishana sehemu moja inabidi kusubiriana kuondoa kero hiyo mtu inabidi apite ndani ya jengo hili, na hapo inakuwa mzunguko hadi kufikia geti lilipo,” amesema Haule.

Naye, Shamimu Nundu, mkazi wa Keko amesema kufurika kwa chemba hizo na kutiririsha maji machafu licha ya kuwa kero, lakini ni hatari kwa magonjwa ya milipuko. Amesema watembea kwa miguu wamekuwa kwenye hatari kubwa wanapopita eneo hilo huku magari yakirusha maji bila kujali watembea kwa miguu.
“Nilimwagiwa maji eneo hili kitendo kile kiliniuma kwa sababu nilikuwa nakwenda kazini kila nikijiangalia najiskia vibaya kwa sababu haya maji ni machafu kutoka vyooni, mamlaka husika zichukue hatua,” amesema Shamimu.
Shukuru Ally, dereva wa bodaboda amesema kutokana na hali hiyo ya kutiririka kwa maji machafu, wameingiwa hofu ya kupita kwenye eneo hilo.
“Bora kupita pembeni ya barabara na hata foleni inayotokea watu wanaohofia kuingia kwenye mashimo yenye maji machafu yanatoka kwenye chemba za vyoo,” amesema Ally.

Awali, kero za kutiririka kwa maji machafu ilikuwa kwenye mitaa ya Kariakoo ambayo ilikuwa ikifurika mara kwa mara na kuwa kero kwa wafanyabiashara na wateja wanaofika katika eneo hilo.
Hata hivyo, Mwananchi ilipita katika mtaa wa Mchikichi ambao unafahamika kwa kero ya kujaa maji na chemba kutoa maji na kukuta kukiwa salama.