Migogoro ya ardhi, mirathi yakithiri kliniki ya Makonda Arusha

Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha wakiwa katika Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha leo Alhamisi Mei 9, 2024 ikiwa ni siku ya pili ya kliniki ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili

Muktasari:

  • Kliniki hiyo ya siku tatu ilianza jana ambapo akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi 9, 2024, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria  wa Tanganyika (TLS), Kanda ya Arusha, George Njooka, ametaja maeneo makubwa mawili yaliyoonekana kuwa na changamoto ni ardhi pamoja na mirathi.

Arusha. Changamoto za migogoro ya ardhi na mirathi imetajwa kushamiri kwenye kliniki ya haki katika Mkoa wa Arusha iliyoratibiwa na mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 9, 2024, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria  wa Tanganyika (TLS), Kanda ya Arusha, George Njooka amesema katika siku mbili za kusikiliza wananchi na maeneo makubwa mawili yaliyoonekana kuwa na changamoto ni ardhi pamoja na mirathi.

Leo ikiwa ni siku ya pili tangu kliniki hiyo ianze kusikiliza kero hizo, amesema eneo la ardhi limeonekana kuwa na changamoto kubwa ambapo baadhi ya wananchi wanadhulumiana wao kwa wao.

Wakili Njooka amesema moja ya vitu vitakavyosaidia kupunguza migogoro hiyo ni pamoja na wananchi kutumia wanasheria kwani baadhi yao wamenunua ardhi na kuandikiwa mikataba na wauzaji, hivyo kukosa ushauri wa kisheria wakati wa ununuzi jambo linalochangia ongezeko la  migogoro hiyo.

“Unaponunua ardhi lazima uangalie mmiliki, huyu mtu ameupataje umiliki lakini ukitoka kwenye umiliki angalia pia barabara za kuingia eneo lako, wengine wana migogoro ya barabara kumbe wamenunua maeneo yasiyo na barabara,” amesema.

Ametaja changamoto ya pili waliyokutana nayo kwa ukubwa ni eneo la mirathi ambalo limeonekana kuwa shida kubwa kwa watu wengi ambapo baadhi yao wamefungua mirathi bila kufuata utaratibu au kutokujua muda maalumu wa kufanya hivyo.

 “Niwashauri  wananchi wenzangu, tujitahidi kuandika wosia, watu tuna imani nikiandika wosia unatafsiri kufa lakini unapoondoka duniani na ukaacha mali bila kuandika na kurithisha unaacha shida kubwa ulimwenguni na wale ambao ulikuwa unawatafutia mali zinaishia kupotea.”

Ameongeza: “Wasikimbilie kwa mkuu wa mkoa, waje wapate ushauri kwenye ofisi na tunakuwa na nyakati tofauti tunatoa huduma za kisheria mwanzoni mwa mwaka wa Mahakama na tunapoenda mwisho wa mwaka ili wafanye mambo sahihi kwa mujibu wa sharia,” amesema.

Mmoja wa wananchi waliojitokeza katika kliniki hiyo ni mjane, Honoratha Temu ambaye amesema alifiwa na mume wake tangu mwaka 1984 lakini hadi sasa hajapata haki yake.

“Mume wangu alikuwa akifanya kazi serikalini na alifariki kwa ajali, nimefuata kwa taratibu zote za kisheria lakini sijapata haki yangu, ni Mungu amemleta Makonda asikilize shida zetu, hii fursa ya kusikilizwa na mawakili, naamini watatusaidia,” amesema.