Makonda ampa siku tatu RC Mtanda kumaliza migogoro ardhi

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Tarime katika Uwanja wa Shamba la Bibi.
Muktasari:
- Akizungumza kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Bunda na Butiama za mkoani humo, Makonda amesema amebaini kuna migogoro mikubwa ya ardhi inayowatesa wananchi wa mkoa huo.
Tarime. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amempa siku tatu Mkuu wa Mkoa wa Mara Said Mtanda kuja na mpango wa utatuzi wa migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara ndani ya mkoa huo.
Ameeleza hayo leo Novemba 14 wakati akihutubia wananchi wa Tarime katika uwanja wa Shamba la Bibi, akiwa katika ziara ya kutoa shukrani kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika Wilaya za Bunda na Butiama za mkoani humo, Makonda amesema amebaini kuna migogoro mikubwa ya ardhi inayowatesa wananchi wa mkoa huo.
"Furaha niliyonayo Mkuu wa Mkoa (Said Mtanda) amenieleza alivyojipanga sasa nampa siku tatu awe amekamilisha mpango wake. Chama hakitaki kusikia migogoro ya ardhi katika mkoa wa Mara.
"CCM inamwamini Mtanda kwa sababu ni kiongozi shupavu, lakini ndani ya siku tatu akamilishe mpango wa kutatua na kuondoa migogoro ya ardhi. Yaani mwananchi ananua ardhi anapewa na hati, lakini akitaka kibali cha ujenzi aambiwa ardhi yake haitambuliwi, sasa wanaikataaje? alihoji.
Kwa upande wake, Mtanda amepokea maelekezo ya chama kwa unyenyekevu na kuahidi kuyafanyia kazi huku akimwakikishia Makonda wakati wowote wakipewa maagizo na chama hicho tawala watayatii na kuyatekeleza.
"Ni wajibu kwa hiyo Novemba 21 wataalamu wameshajipanga kuanza kliniki ya utatuzi wa migogoro ya ardhi Musoma.Lakini hapa kuna wakuu wa wilaya wangu wote nimewaelekeza kutenga siku mbili kwa wiki kusikiliza migogoro ya ardhi wakiwa na wataalamu," amesema Mtanda.
Katika hatua nyingine, Makonda amemwagiza Mtanda kuhakikisha bodaboda zote zilizokamatwa katika mpaka wa Sirari kuachiwa.
"Ninazo taarifa zipo bodaboda zilizotumia fursa ya mpaka wa Sirari kufanya biashara ya magendo hilo halipingiki. Lakini wapo wananchi ambao majirani wanaoendelea kufanya shughuli zao, sasa maelekezo ya CCM kuanzia leo pikipiki zote zilizokamatwa Sirari ziachiwe.
"Pikipiki zilizokamatwa warudishiwe, kama kuna mali zilizokamatwa kodi na kurudishiwa mali na fedha ziende hazina.Wapeni fursa watu wafanye biashara kama ni bodaboda alipe ushuru na kodi ili achukue bidhaa auze," amesema Makonda.
Uamuzi huo wa Makonda umekuja baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kusema pamoja na mambo mazuri vijana wa bodaboda wanakamatwa sana.
“Eneo la Sirari (mpakani), sasa hivi saruji ya Tanzania inauzwa Sh25, 000 bei lakini ya kutoka Kenya Sh 15,000 kwa mfuko mmoja hata ungekuwa wewe lazima ungepita chocho ili uipate ili kujenga
"Ukizungumza vijana wa Sirari wamekamatwa na kutaifishwa mali zao, kuna vijana wana shahada hawana ajira lakini pikipiki zao zimejaa pale Sirari.
Natamani vijana wakabidhiwe pikipiki zao ili kazi iendelee," amesema Waitara.
Naye Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki amesema changamoto kubwa ilikuwa soko ambapo wananchi na wafanyabiadhara walikuwa wakipata adha kubwa ya kufanya shughuli zao, lakini Srrikali imetoa Sh9 bilioni za ujenzi uliofikia hatua ya kumalizia.
"Tarime kulikuwa na tatizo la maji lakini Serikali imetoa Sh100 bilioni kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maji kutoka ziwa Victoria na mwakani mambo yatakuwa mazuri. Tarime kulikuwa na hospitali moja hivi sasa tuna vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali," amesema Kembaki.