Mifuko zaidi ya 600 mbolea ya ruzuku yamuweka matatani Maneno

Muktasari:
- Maneno Yusuph, Mkazi wa Ilula wilayani Kilolo anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Iringa kwa tuhuma za kujipatia zaidi ya mifuko 600 ya mbolea ya ruzuku kinyume cha sheria na hatimaye kuuza kwa wakulima kwa bei ya juu ambayo ni tofauti na ile inayoelekezwa na Serikali.
Iringa. Jeshi la Polisi Mkoani Iringa linamshikilia Maneno Yusuph, Mkazi wa Ilula wilayani Kilolo kwa tuhuma za kujipatia zaidi ya mifuko 600 ya mbolea ya ruzuku kinyume cha sheria na hatimaye kuuza kwa wakulima kwa bei ya juu tofauti na bei elekezi ya Serikali.
Inadaiwa kuwa Maneno, alijisajili majina tofauti tofauti kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea na kujizolea mifuko hiyo ambayo aliiuza kwa wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akinunua mbolea kutoka kwa kampuni mbalimbali na kuuza kwa bei ya juu.
Kulingana na Dendego, Maneno alikuwa akiwauzia wakulima mfuko wa kilo 50 kwa bei ya Sh82, 000 hadi 87,000.
Dendego amesema mtuhumiwa huyo alifanya udanganyifu katika manunuzi yake ya mbolea kwa kutumia namba ya mkulima 81140702890 ambayo ilikuwa imeandikishwa katika mfumo wa ruzuku kwa jina la Sudiana J. Mwakalinga wa mkoani Morogoro.
Mtuhumiwa alifuatiliwa kwenye mfumo na kubainika kuwa alifanya udanganyifu katika kujiandikisha na kupata namba tatu za ruzuku ambazo ni 84050311708 ambazo zilikua kwa ajili ta ekari saba, namba 84050327582 za ekari 80 na 84050328057 za ekari 120.
Mara kadhaa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA), Dk Stephen Ngailo amenukulia akisema sheria kali itamkumba yeyote atakaye bainika kufanya wizi wa mbolea ya ruzuku.
"Wito wangu kwa wafanyabiashara na mawakala wote wa mbolea nchini, hakuna mtu anaye ruhusiwa kuuza mbolea zaidi ya bei elekezi tulizotoa, atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Ngailo.
Michael Sanga ni Meneja wa Kanda wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni juhudi za ofisi yake pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa za kudhiiti vitendo vya aina hiyo.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema wanaendelea na uchunguzi zaidi kwa kuwa wanadhani tukio hilo linahusisha zaidi ya mtu mmoja.