Prime
Miezi sita kitanzi kwa bosi mpya Tanesco

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Gisima Nyamohanga.
Dar es Salaam. Miezi sita aliyopewa bosi mpya wa Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco) kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme nchini ni kama kitanzi kwake, kutokana na hali iliyopo sasa.
Rais Samia Suluhu Hassan amemwambia bosi huyo wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga kuwa baada ya miezi sita hataki kusikia kelele za kukatika kwa umeme.
Amemtaka kusimamia mchakato wa ukarabati wa mitambo unaoendelea hivi sasa, akisema ndilo jukumu lake la kwanza ndani ya shirika hilo.
Katika hotuba yake aliyoitoa jana Ikulu jijini hapa, baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali, Rais Samia alisisitiza ana imani Nyamo-Hanga, aliyewahi kuwa mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) anaiweza kazi hiyo kwa kuwa alikuwa huko awali.
“Nyamo-Hanga una miezi sita, nisisikie kelele za kukatika kwa umeme… Maharage yupo hapo akwambie walikuwa wanafanyaje wanapenya wapi.
“Najua utaweza, nakupa miezi sita, nakuangalia pale Tanesco, kazi yako ya kwanza ni kusimamia ukarabati wa mitambo, lakini baada ya miezi sita, nisisikie kelele za kukatika kwa umeme, tutasaidiana, nenda najua utaweza,” alisisitiza.
Hata hivyo, Rais Samia alikiri uwepo wa changamoto ya umeme hivi sasa, akisema janga hilo si la mtu, bali ni la Taifa.
Alisema hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabianchi na mchakato wa matengenezo ya mitambo.
“Nyamo-Hanga unakwenda Tanesco nikijua wewe si mgeni, unaijua vema, utakwenda kuongeza pale Maharage alipofikia. Tuna ‘crisis’ (janga) kama Taifa siyo mtu, bali mitambo haikufanyiwa matengenezo kwa muda mrefu, sasa inakwenda kufanyiwa kazi ambapo lazima kwingine kuzimwe na kuwasha kwa hiyo kuna upungufu wa umeme," alisema Samia.
Alisema Serikali imejipanga kukabiliana na suala hilo, ikiwemo kufanya ukarabati wa mashine, kujenga vituo vya kupoza umeme na kuunganisha mikoa katika gridi ya Taifa.
Wakati Rais Samia akisema hayo, hivi karibuni Naibu Mkurugenzi wa Uwekezaji Tanesco, Declan Mhaiki alisema sababu ya kukatika umeme kwa baadhi ya maeneo nchini ni upungufu wa maji na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati hiyo kutokana na uwekezaji.
Kibarua kigumu
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi alizungumzia maagizo hayo ya Rais akisema, “sijui kama itawezekana au haiwezekani, kwa kuwa upungufu wa umeme unatokana na vitu vingi, ikiwemo ukame na uchakavu wa mitambo na mfumo mzima wa umeme.
“Sijui kwa kiasi gani hayo matengenezo yamefanyika hadi hivi sasa, inawezekana Rais Samia anajua ndiyo maana amempa muda wa ukomo. Natamani itokee kama ambavyo Rais amesema ili kupunguza shida za umeme nchini,” alisema.
Alisema endapo muda huo wa ukarabati ukikamilika na mvua zikanyesha za kutosha na mabwawa yakajaa maji, mambo yatakuwa mazuri na huenda umeme ukapatikana wa kutosha, lakini ikiwa tofauti na hapo hali itabaki kama ilivyo sasa.
Naye mchambuzi wa siasa na uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema sababu alizozitoa Rais Samia, ikiwemo ya ukarabati wa mitambo inayosababisha upungufu wa umeme, inaweza kushughulikiwa ndani ya muda aliompa Nyamo-Hanga.
“Kama ni sababu hiyo, basi ni rahisi kwa bosi mpya, inaweza isifike hata miezi sita, hata miezi mitatu inaweza isifike tukarudi kwenye hali ya kawaida. Miezi sita ni mingi kama sababu ni ukarabati wa mitambo.
“Ingekuwa kama tunataka tuongeze uzalishaji, hapo ingekuwa suala lingine, mfano tuna megawati 600 halafu tuongeze nyingine, hii ingekuwa kazi nyingine, lakini ukarabati hauchukui muda,” alisema.
Sababu uteuzi wa Ulanga, Yakubu
Katika hotuba yake, Rais Samia aligusia uamuzi wake wa kuwateua John Ulanga na Said Yakub kuwa mabalozi, akisema anataka kukiimarisha kitengo cha diplomasia ya uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kabla ya uteuzi huo, Ulanga alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), nafasi aliyohudumu kuanzia Agosti 7 mwaka huu, huku Yakub alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Rais Samia alisema hivi sasa Serikali ipo katika mchakato wa kuijenga upya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akisema ndani yake kuna kitengo cha diplomasia ya uchumi ambacho hakina nguvu.
“Tumeangalia wasifu wa watu mbalimbali, tumeona wa Ulanga na Yakubu wanaweza kuweka nguvu katika eneo hili, sambamba na uzoefu mliopitia katika sekta za umma na binafsi,” alisema.
Pia, alisema hivi sasa Serikali ipo katika hatua ya kutengeneza sera ya uchumi ya mambo ya nje na mchakato huo umefika mbali, hivyo aliwataka Ulanga na Yakubu kuangalia zaidi eneo la uchumi kwa kuboresha na kuongeza vitu vilivyokosekana.
Rais Samia alisema anafahamu TPSF wana ya kwao na huenda uhamisho wake kuna watu wataufurahia na wengine kusikitika na hivyo akampa Ulanga jukumu la kuhakikisha anasimamia upatikanaji wa mtu sahihi kama yeye wa kushika wadhifa aliouacha.
“Balozi Said tumekutoa ukatibu mkuu, unaweza kudhani ni kushushwa cheo, lakini si hivyo, bali nataka mkakijenge kitengo kwa nguvu zote halafu mbele tutaangalia mengine ya kufanya.
Awali, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka mabalozi hao kwenda kuimarisha diplomasia ya uchumi, kisiasa na kiutamaduni ili kuendeleza mahusiano kati Tanzania na mataifa mengine.
Majaliwa alisema Rais Samia amewekeza nguvu zaidi katika diplomasia ya uchumi akitaka kutumika kwa fursa za uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine kuimarisha uchumi wa Taifa.