Prime
Meta yaboresha usiri wa mawasiliano WhatsApp
Muktasari:
- Watumiaji wa WhatsApp watakiwa kutumia vipengele vya usalama kulinda mazungumzo dhidi ya watu wasiostahili.
Dar es Salaam. Simu ya mkononi imekuwa sehemu ya kuhifadhi karibu kila jambo muhimu katika maisha ya kila siku, kuanzia mawasiliano ya familia, biashara, nyaraka za kazi hadi taarifa za benki.
Hata hivyo, wataalamu wa usalama wa mtandao wanaonya kuwa kuiacha WhatsApp bila ulinzi wa kutosha kunaweza kuwaweka watumiaji katika hatari ya kuvuja kwa taarifa binafsi.
Kwa kutambua changamoto hiyo, kampuni ya Meta inayomiliki WhatsApp imeendelea kuongeza vipengele vya usalama vinavyowaruhusu watumiaji kuficha mazungumzo muhimu na kuyafanya yasionekane kirahisi hata pale mtu anaposhika simu yako.
Mbali na mfumo wa end-to-end encryption, WhatsApp sasa ina vipengele vya Chat Lock na Secret Code vinavyolenga kuongeza ulinzi kwa mazungumzo nyeti.
Chat Lock ni nini?
Chat Lock ni kipengele kinachokuruhusu kufunga mazungumzo ya mtu mmoja au kundi kwa kutumia alama ya kidole (Fingerprint), utambuzi wa uso (Face ID) au namba ya siri ya simu.
Mazungumzo yaliyofungwa huondolewa kwenye orodha ya kawaida ya chats na kuhifadhiwa katika sehemu maalumu inayoweza kufunguliwa tu baada ya uthibitisho wa mmiliki wa simu.
Hii ina maana kuwa hata mtu akifungua simu yako kwa ruhusa au kwa bahati mbaya, hawezi kuona mazungumzo hayo bila idhini ya ziada.
Jinsi ya kuwasha Chat Lock
Kwa watumiaji wa Android na iPhone, hatua za kuwasha Chat Lock ni rahisi. Fungua WhatsApp, kisha chagua mazungumzo unayotaka kulinda. Bonyeza jina la mtu au kundi, tafuta sehemu ya Chat Lock na uwashe kipengele hicho. Baada ya hapo, thibitisha kwa kutumia Fingerprint, Face ID au Passcode. Ukikamilisha hatua hizo, mazungumzo hayo yatahamia kwenye sehemu maalumu ya Locked Chats.
Baada ya kufanya hivyo, mazungumzo hayo yatahamia kwenye sehemu maalumu ya Locked Chats.
Secret Code inaongeza usiri
Meta imeongeza pia kipengele kinachoitwa Secret Code, kinachoruhusu mtumiaji kuweka neno au namba ya siri tofauti na ile ya simu.
Ikumbukwe kuwa baada ya kuwasha Chat Lock, ipo alama juu ya WhatsApp itakayojitokeza kuonyesha kuna mazungumzo yaliyofungwa, lakini ukitengeneza Secret Code alama hiyo itaondoka kabisa.
Badala ya sehemu ya Locked Chats kuonekana moja kwa moja, mtumiaji atalazimika kuandika neno hilo la siri kwenye sehemu ya kutafuta (Search) ndipo mazungumzo yaliyofungwa yatajitokeza.
Kwa njia hiyo, hata mtu anayejua password ya simu yako hawezi kujua kama kuna mazungumzo yaliyofichwa.
Kwa nini ni muhimu?
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la visa vya simu kupotea, kuibwa au kukopeshwa kwa ndugu na marafiki.
Katika mazingira hayo, taarifa za biashara, picha binafsi, nyaraka za kazi au mazungumzo ya kifamilia yanaweza kuonekana na watu wasiostahili.
Wataalamu wa usalama wa mtandao wanasema kulinda simu pekee hakutoshi, bali pia ni muhimu kulinda programu zinazobeba taarifa nyeti.
Usalama unaanza na mtumiaji
Licha ya uwepo wa Chat Lock, wataalamu wanashauri watumiaji kuchukua hatua nyingine za kujilinda. Miongoni mwa hatua hizo ni kuwasha Two-Step Verification ya WhatsApp, kutotuma namba za siri, PIN za benki au OTP kupitia mazungumzo, kutotumia namba rahisi kama 123456 au tarehe ya kuzaliwa kama password, pamoja na kusasisha WhatsApp mara kwa mara ili kupata maboresho ya usalama. Hatua hizi husaidia kuongeza ulinzi wa taarifa binafsi na kupunguza uwezekano wa kuingiliwa na watu wasiostahili.
Unapaswa kutumia lini Chat Lock?
Kipengele hiki kinaweza kuwa muhimu kwa watu wanaohifadhi taarifa za kikazi, wanawasiliana na wateja, wanaendesha biashara kupitia WhatsApp au wanaotaka kulinda faragha ya mazungumzo yao binafsi.
Kadiri matumizi ya simu yanavyozidi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, wataalamu wanaamini kuwa watumiaji wanapaswa kuanza kuona usalama wa taarifa zao kama jukumu lao binafsi badala ya kutegemea teknolojia pekee.