Mdundo: Vazi la Taifa sasa kimeeleweka

Muktasari:

  • Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Dk Kedmond Mapana amesema Ijumaa Februari 3, watakabidhi ripoti ya mdundo na vazi la Taifa kwa Serikali baada ya mchakato huo kufanyika kwa miaka kadhaa sasa nchini.

Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Dk Kedmond Mapana amesema Ijumaa Februari 3, watakabidhi ripoti ya mdundo na vazi la Taifa kwa Serikali.

Amesema mbali na ripoti ya vazi na mdundo wa taifa, pia siku hiyo wasanii zaidi ya 31 watakabidhiwa mikopo isiyo na riba inayotolewa na Serikali ya awamu ya sita.

Akizungumza leo Januari 31 kwenye uzinduzi wa wiki ya sanaa inayoanza kesho, Dk Mapana amesema mbali na matukio hayo, wadau wa sanaa pia watakuwa na tukio jingine kubwa la ‘Tukutane Dar’ kwa siku tano mfululizo.

"Tukio hili litafanyika kuanzia kesho Februari Mosi hadi 5 kwenye maeneo tofauti saba ya sanaa na utamaduni jijini Dar es Salaam likitanguliwa na warsha na mijadara asubuhi na burudani ni jioni," amesema.

Maeneo hayo ni Nafasi Art Space Rangi Gallery, CDEA, Ajabu Ajabu, ASEDEVA, Chuo kikuu cha Dar es Salaam na MuDa Kona.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi wa Nafasi Art Space, Lilian Hipolyte Mushi amesema maonyesho yatakuwa na sanaa za uoni rangi gallery, filamu, ubunifu katika soko la sanaa nchini, wanunuzi na wakusanyaji wa sanaa na burudani ya jukwaa.

"Pia kutakuwa na warsha ya yoga na ngoma za asili Jumapili," amesema.

Amebainisha kwamba asubuhi kutakuwa na mijadala mbalimbali ya sanaa na jioni ni maonyesho ya wasanii.