Serikali na jumuiya ya wafanyabiashara walivyokubaliana kumaliza mgomo

Msemaji wa Serikali, Thobias Makoba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea nchini.

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Wafanyabiashara wamekubaliana kumaliza mgomo kwa maazimio 15, ikiwemo kusitisha kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za EFD, kuongeza elimu ya kodi na kuboresha mfumo wa TANCIS na bandari kavu.

Dodoma. Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) wamefikia makubaliano ya kumaliza mgomo wa wafanyabiashara uliokuwa ukiendelea nchini baada ya kuweka maazimio 15. Makubaliano hayo yametangazwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 27, 2024.

Mgomo huo ulianza Juni 24, 2024, katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, kisha kusambaa katika mikoa mingine kama Arusha, Morogoro, Kagera, Dodoma, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mwanza na Mtwara.

Miongoni mwa maazimio hayo ni kusitisha mara moja kamatakamata na ufuatiliaji wa risiti za EFD katika maeneo yote nchini hadi Agosti, 2024.

Wafanyabiashara wamehimizwa kuendelea kutoa risiti za mauzo huku TRA ikitakiwa kuweka mfumo mzuri utakaowezesha utoaji wa nyaraka muhimu za manunuzi wakati wa uingizaji wa bidhaa kuanzia Julai, 2024.

Aidha, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeagizwa kuongeza haraka bandari kavu kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa mizigo kupitia utaratibu wa de-consolidation.

Kwa upande wake TRA imeelekezwa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kodi na maboresho yanayofanyika ili kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara.

Pia, inatakiwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika. Bidhaa hizo ni vitenge, mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti.

Serikali itaendelea kufanya mapitio ya viwango vya kodi ili kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa haki na amani. Aidha, TRA inatakiwa ikamilishe maboresho ya mfumo wa TANCIS ambao utajumuisha moduli ya Auto Valuation kufikia Januari 2025.

TBS na TRA wameelekezwa kukamilisha marekebisho ya mfumo wa Tehama ili mizigo inayoingia nchini kwa njia ya uchangiaji makasha iweze kukombolewa kwa namba ya usajili ya mlipakodi (TIN) ya mwenye mzigo bila gharama za ziada.

Wizara ya Fedha imetakiwa kufanya uchambuzi na tathmini ya mfumo mzima wa utozaji na ukusanyaji wa ushuru wa huduma na kushauri njia mbadala rafiki kwa wafanyabiashara.

Aidha, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuimarisha ukaguzi wa vibali vya kazi kwa wageni na kuchukua hatua kali kwa wanaokiuka sheria.

Mawaziri wanaohusika na sekta ya biashara watakutana na wafanyabiashara kusikiliza changamoto na kupokea maoni ya kuboresha mazingira ya biashara.


Wataalamu wa forodha nao wameguswa wakitakiwa wakutane na Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini kujadiliana kuhusu taratibu za kiforodha na uthaminishaji wa mizigo ifikapo Julai 10, 2024.

Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuratibu utoaji wa mrejesho kwa wafanyabiashara kila robo mwaka kuhusu utekelezaji wa maazimio baina ya wafanyabiashara na Serikali.

Kutokana na maazimio hayo, pande zote mbili zimekubaliana hali ya biashara kote nchini kuendelea kama kawaida ili kuwapa Watanzania huduma wanazostahili.