Mchuano rasmi kuwania uongozi kanda nne Chadema

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Susan Kiwanga akiwasili makao makuu ya chama hicho, Mikocheni Dar es Salaam kwa ajili ya kikao kilichoanza leo. Kulia ni mmoja wa wahudumu wa mkutano huo. Picha na maktaba
Muktasari:
Hatua hiyo ni baada ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne Dar es Salaam kupitisha majina ya wagombea.
Dar es Salaam. Sasa ni rasmi mtifuano wa vigogo ndani ya Chadema wanaowania nafasi za uongozi wa kanda ambao wanaanza kusaka kura kwa wajumbe katika mikoa 14.
Hatua hiyo ni baada ya Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne Dar es Salaam kupitisha majina ya wagombea.
Kamati Kuu imeamua uchaguzi wa kanda hizo ufanyike Mei 29, 2024.
Miongoni mwa nafasi zinazowania katika kanda ni uenyekiti, makamu mwenyekiti, wahazini wa kanda na viongozi wa mabaraza ya wanawake, wazee na vijana ya Chadema ngazi ya mikoa.
Kanda zitakazofanya uchaguzi ni Serengeti yenye mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu, kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma), Nyasa (Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Rukwa) na Victoria (Mwanza, Kagera na Geita).
Jumla ya makada 135 walitia nia lakini 92 ndio waliopenya katika mchakato huo.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema leo Mei 17, 2024 ametoa orodha ya wagombea wa kanda hizo waliopenya katika usaili uliokuwa wa vute nikuvute.
Miongoni mwa wagombea waliokatwa ni Emmanuel Ntobi na James Mahangi waliokuwa wakiwania uenyekiti wa kanda ya Serengeti, na Daniel Mwambikile wa kanda ya Nyasa.
Kwa nafasi ya makamu walioachwa ni Alex Kimbe (Nyasa), Ester Jackson, Gango Kidera na Esther Nyaburiri (Serengeti) na wengine katika ngazi ya mabaraza na wahazini.
Kwa hatua hiyo, Gimbi Masaba ambaye ni makamu mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti atachuana na Lucas Ngoto. Nafasi ya makamu yupo, Jackson Scania akisimama pekee.
Waliopitishwa Kanda ya Nyasa ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Mchungaji Peter Msigwa kwenye nafasi ya uenyekiti. Upande wa makamu mwenyekiti waliopenya ni Frank Mwakajoka, Joseph Mjenda na Mbegese Mwalipani.
Kwa Kanda ya Magharibi waliopitishwa uenyekiti ni Dickson Matata, Mussa Martine, Ngassa Mboje na Gaston Garubindi anayetetea kiti hicho. Nafasi ya makamu wapo Massanja Katambi na Rhoda Kunchela.
Katika Kanda ya Victoria waliopenya ni Ezekia Wenje anayetetea na John Pambalu, wakati makamu mwenyekiti wamo Bazil Waziri, Khalid Hussein, Mbutusyo Mwakihaba na Sylivester Makanyaga.
Taarifa ambazo Mwananchi limefahamishwa sababu za kuweka siku moja ya uchaguzi huo ni kuondoa figisufisu zinazoweza kutokea na kuharibu mchakato.
Wakati wa mchakato wa usaili, mmoja wa wagombea aliidokeza Mwananchi kuwa “uchaguzi utakuwa siku moja ili kuondoa mamluki watakaoweza kutoka kanda moja kwenda nyingine, kwa lengo la kufanya figisu.”