Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MC GARA B: Ticha aliyetumia ujasiri kutoboa, kunasa mke

Gara B na mkewe

Muktasari:

  • Ikitokea imeandaliwa orodha ya washereheshaji mahiri watano wanaofanya vizuri kwa sasa nchini na Afrika Mashariki, basi ujue kabisa, jina la Gara B haliwezi kukosekana katika orodha hiyo.

Ikitokea imeandaliwa orodha ya washereheshaji mahiri watano wanaofanya vizuri kwa sasa nchini na Afrika Mashariki, basi ujue kabisa, jina la Gara B haliwezi kukosekana katika orodha hiyo.

Hii ni kutokana na umaarufu na uwezo wake wa kunogesha sherehe na kama hujui ni kwamba kwa mwaka huu pekee amepata tuzo mbili kubwa za ushereheshaji. Moja ya Mshereheshaji Bora Afrika Mashariki na ile ya Mshereheshaji Bora Afrika. Bado kuna maswali?

Tuzo hizi zimezidi kuongeza ukubwa wa jina la MC huyu ambaye historia ya maisha yake inaonyesha amepitia maeneo mengi tofauti kabla ya kutambulika kwenye ushereheshaji, fani ambayo hakuipata kwenye chuo au ngazi yoyote ya elimu.

Mshereheshaji huyu, ambaye jina lake halisi ni Godfrey Rugarabamu amefanya mahojiano maalumu na gazeti hili na kutupitisha katika safari ya maisha yake, ndoa na familia ikiwa ni siku chache baada ya kuadhimisha miaka sita ya ndoa yake.

Licha ya kazi hiyo kumuingizia kipato cha kuendesha maisha yake, kamwe hasahau namna ushereheshaji ulivyomkutanisha na mkewe, Norah Nchobe, ambaye kwa pamoja wametengeneza familia ya watoto watano.

Wawili hawa walikutana mwaka 2012 katika harusi, Gara B akiwa MC, wakati Norah akiwa miongoni mwa warembo wanaowasindikiza maharusi (bride maids).

“Nakumbuka ilikuwa klabu ya Gofu ya Lugalo, nikiwa naendesha harusi ya jamaa yangu mmoja aitwae Kelvin na mkewe Hellen, nilimuona bibie kipindi hicho akiwa miongoni mwa wale wadada wasimamizi. Kiukweli alikuwa amependeza na alinivutia ila sikuzungumza naye,” anasema Gara B na kuongeza;

“Niliendelea kufanya kazi yangu, harusi ilipoisha watu wametawanyika tukiwa tunafunga vifaa vya muziki nikamuona bado yupo, nikaanza kumuongelesha, akaniambia anamsubiri kaka yake amfuate. Nikamwambia nimpe lifti, wakati namwambia hivyo wala sikuwa na gari, nilikuwa nasubiri lile gari linalobeba vifaa vya muziki ndilo nami nipande.”

Pamoja na jitihada hizo, anasema hakufanikiwa kumshawishi wala kupata namba ya simu, kwani alipoomba tu akatolewa nje.

Hata hivyo, huenda ilipangwa wawili hawa wawe pamoja, kwani baada ya muda walikutana tena kwenye sherehe nyingine na wakati huu bahati ilikuwa upande wake, akafanikiwa kupata mawasiliano ya mwanamke huyo.

“Baada ya kupata namba ya simu mambo yalikuwa mteremko, tukaanzisha urafiki uliodumu kwa miezi miwili hadi mitatu. Si unajua yale mambo ya sitaki nataka, mwisho akaingia line tukaingia rasmi katika uhusiano uliozaa uchumba na hatimaye tukafunga ndoa Novemba 21, 2016,” anasema.

Muunganiko huo uliwawezesha kupata watoto watano, japo lengo lao lilikuwa wawili tu, kwa maana ya mmoja wa kike na mwingine wa kiume, ila wakati wao wanapanga hivyo, Mungu alikuwa na mipango mingine juu yao.

Hivyo walivyopata mtoto wa kwanza wa kiume wakaanza kutafuta wa pili wa kike, lakini kila mkewe alipobeba ujauzito walipata mtoto wa kiume.

“Mwendo ulikuwa hivyo hadi mtoto wa nne wote walikuwa wa kiume, tukasema tujaribu mara ya mwisho akiwa wa kiume basi tunaachana na habari hizo, bahati nzuri Mungu akatupatia mtoto wa kike ambaye ndiye kitinda mimba wetu. Ameleta furaha kubwa katika familia kwani tulimtafuta mtoto wa kike hatimaye tukampata.”

Licha ya muda mwingi kuwa kwenye majukumu ya kazi iwe ni ushereheshaji, uigizaji, utangazaji au uendeshaji wa lebo yake ya mavazi ya maharusi, muda mchache anaopata anautumia na familia yake.

“Ninapopata muda wa kupumzika, najitahidi niwe nyumbani, nipate wasaa wa kuwa na familia, hususan watoto maana wakati mwingine unaweza kumaliza wiki mnapishana tu. Inapotokea niko nyumbani napenda kuwa nao,” anasema Gara B na kuongeza:

“Mtoto wangu wa kwanza namuandaa kuwa nyota wa mpira wa kikapu na kufanikisha hilo, nimetengeneza mazingira nyumbani tunacheza pamoja. Pia napenda bustani hivyo wakati mwingine natumia muda wangu nikiwa nyumbani kushughulika na bustani kuhakikisha kila kitu kipo sawa”.

Tofauti na ilivyo kwa washereheshaji wengine, Gara B ameamua kuzingatia taratibu za ajira kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine, ikiwemo suala zima la likizo, kila ifikapo Machi huchukua likizo na kujikita zaidi na familia na kutembelea vivutio vya utalii.


KUMBE TICHA WA UNG’ENG’E

Kwa namna ambavyo anaonyesha umahiri katika ushereheshaji unaweza kufikiri kuwa aliingia darasani akapikwa na kubobea upande huo, la hasha, kitaaluma Gara B ni mwalimu wa Somo la Kiingereza, aliyehitimu Chuo cha Ualimu Kigurunyembe, mkoani Morogoro na kuajiriwa na Shule ya Sekondari Pendamoyo iliyopo Temeke, Dar es Salaam.

Gara B ameweka wazi kuwa ualimu ni kazi aliyoipenda na kuifanya kwa ufanisi mkubwa, ila harakati za maisha zilimfanya aangalie fursa nyingine mbele ya upeo wa macho yake.

“Kitaaluma mimi ni mwalimu, tena mwalimu mzuri wa Kiingereza, nilifurahia maisha yangu ya ualimu kwa kuwa wanafunzi walinipenda na kulipenda somo langu, hivyo hata ufundishaji haukuwa mgumu na walifanya vizuri,” anasema Gara B na kuongeza;

“Nakumbuka zile moments za wanafunzi kufanya vizuri kwenye somo langu na nilikuwa miongoni mwa walimu wanaopata zawadi mara kwa mara kutokana na kufaulisha, yaani A kwenye Kiingereza enzi zangu zilikuwa za kutosha.”

Kama alivyoangukia katika ushereheshaji, hata kwenye ualimu alikwenda ikiwa ni njia ya kujitafuta baada ya kushindwa kutimiza ndoto ya mama yake, aliyetamani aje kuwa padri wa Kanisa Katoliki baada ya kupelekwa Shule ya Seminari.

“Mama alitamani sana nimtumikie Mungu kwa kuwa padri, alinipeleka seminari akiamini huko ndipo mahali sahihi pa kunitengeneza anavyotaka. Kweli nilisoma hadi kidato cha sita na nilikwenda kabisa nyumba ya malezi, ila nafsi yangu iliniambia upande huo siuwezi, niangalie kwingine ndipo nikaibukia ualimu.

“Nikiwa shuleni nilipenda kujihusisha na sanaa, mara kadhaa nilitoroka kwenda nje ya shule kwenye masuala ya uimbaji, haikuwa rahisi kufanya hivyo ukiwa seminari, ila hata siku moja sikuwahi kugundulika hadi nilipomaliza shule,” anafafanua.

Aliendeleza harakati hizo akiwa chuo cha ualimu na hatimaye akakamilisha mwaka mmoja wa mafunzo ya darasani na kwenda kwenye vitendo ambako, huko ndiko matamanio yake ya kuingia katika sanaa yakaongezeka.

“Huku sasa mambo ya sanaa yakazidi kuniteka, nikaanza kushiriki mashindano ya kusaka vipaji, ikiwemo vya utangazaji na uimbaji, sikuwahi kushinda, ila mara zote nilivuka kwenye mchujo hadi kufikia 10 bora, hii ikanipa matumaini kuwa kuna kitu ndani yangu,” anasema na kuongeza:

“Nikiwa Morogoro kwenye mafunzo kwa vitendo nikapata fursa ya kutangaza Redio Abood, lakini kutokana na kubanwa na majukumu ya ualimu nikaipoteza nafasi ile, ila utangazaji ilikuwa ni miongoni mwa vitu nilivyovipenda.

“Nikatengeneza urafiki na wadau wa sanaa, uandaaji wa matamasha wakawa washkaji zangu, basi ikitokea matamasha au kuna wasanii wanakuja Morogoro jukumu langu lilikuwa kuzunguka kwenye gari la matangazo kutangaza kwa kipaza sauti au spika kuhusu ujio huo au tamasha. Kwa jinsi nilivyokuwa naifanya kwa moyo walinipenda nikawa napata kazi nyingi za utangazaji.”

Baada ya kumaliza mafunzo kwa vitendo akapangiwa kituo cha kazi Sekondari Pendamoyo, akiwa anatekeleza jukumu hilo alipata pia kazi ya muda wa jioni katika kampuni moja ya simu ambapo alikuwa akiifanya mara baada ya kumalizika saa za kufundisha.


KAZI YA U-MC

Kupenda kwake masuala ya burudani tangu akiwa sekondari, kulimfanya pia avutiwe na kazi ya ushereheshaji (MC), hivyo taratibu akawa anajifunza kuongoza sherehe na ili kujinoa zaidi alisimamia shoo za sherehe zote za familia.

“Ilikuwa ikitokea kipaimara sijui birthday jukumu la kuongoza sherehe nalichukua, hiyo niliendelea nayo hadi wakati nasoma, nilikuwa nikienda kwenye sherehe naangalia namna MC anavyoendesha, zaidi ya hilo kuna rafiki yangu alikuwa mpiga video kwenye sherehe nilikuwa naenda kwake nachukua CD za sherehe najifungia ndani kufuatilia kila anachokifanya MC,” anafichua na kuongeza:

“Hii iliniimarisha siku hadi siku, nikaendelea kuhudumia shughuli za kifamilia. Nakumbuka kazi yangu ya kwanza kama MC niliipata kutoka katika ile kampuni ya simu niliyokuwa nafanya part time, bosi wangu mmoja alikuwa na sherehe halafu MC akamuangusha dakika za majeruhi, lakini siku zote nilikuwa nawaambia naweza kufanya hivyo, hawakuwahi kuniamini ila lilipotokea hilo akanipa nafasi.”

Wazungu wana msemo ‘Golden chance never come twice’, Gara B alihakikisha anaitumia vyema fursa hiyo na wafanyakazi wenzie wakaonyesha kuvutiwa na huduma yake, kuanzia hapo milango ya ushereheshaji ikafunguka na huo ndio ukawa mwanzo wa safari yake. Aliendelea kutekeleza majukumu yake yote ya ualimu, kampuni ya simu na ushereheshaji hadi mwaka 2020 alipochukua likizo ya masomo kwa ajili ya kujiendeleza kielimu, lakini akajikuta anautumia muda huo kujijenga na kujiimarisha zaidi kwenye kazi hiyo ya ushereheshaji.

Nje ya kutoa huduma kama MC, Gara B ana kampuni ya utayarishaji picha na video za sherehe, anatengeneza na kuuza mavazi ya maharusi wa kiume, biashara ambayo ina uhusiano mkubwa na anachokifanya kwa sasa.

Kila kazi ina vitu vya kuzingatia ili uifanye kwa ubora, kwenye ushereheshaji pia iko hivyo, Gara B huwa na kikao maalumu na maharusi au binti anayefanyiwa sendoff kabla ya siku husika ambapo hutumia kupata taarifa za kina kuhusu maharusi, familia na vitu wanavyopenda ili kuongeza mzuka anapochagiza kwenye sherehe.

Kando na hilo suala la muonekano ni muhimu, hivyo hutumia pia muda mwingi kuandaa mavazi atakayovaa kwenye sherehe husika sambamba na kujiweka vizuri kimuonekano na hili ndilo lilimsukuma kuanzisha lebo ya mavazi.

“Kwangu muonekano ni kipaumbele, lazima nipendeze ndio sababu nina muda wa kujiweka sawa, kabla ya kuhudhuria sherehe. Nilianzisha lebo ya mavazi kwa sababu nilikuwa kila ninapohitaji nguo nakwenda kwa mbunifu, lakini maelekezo yote ya ile nguo nayatoa mimi, nikaona hivi kwanini nisijitengenezee mwenyewe,” anasema Gara B na kuongeza:

“Nikafanya uwekezaji eneo hilo, nina vijana wanaoshona na kubuni suti vizuri mno, natoa maelekezo kwa nguo za maharusi au pale inapobidi. Kutokana na hili naweza nisihudumu kwenye sherehe yako kama MC, lakini ukavalishwa na GaraBest Look.”


VANESSA NA ROTINI TU

Licha ya kuhudumu katika sherehe nyingi za watu wa kawaida na maarufu, kiu kubwa ya Gara B ni kushuhudia ndoa ya Vanessa Mdee na Rotimi, akitamani kuiongoza harusi yao kama mshereheshaji.

“Nawapenda Vanessa na Rotimi, natamani ifike siku wafunge ndoa, maana kwa muda ambao tumewaona wakiwa pamoja inatosha sasa dada yetu aolewe. Ikitokea hivyo natamani nipate bahati ya kusherehesha harusi yao. Nawapenda pia Jackline Wolper na Rich Mitindo ila kutokana na majukumu nilishindwa kuifanya kazi yao, nawapenda pia Nandy na Billnass hawa nilifanikiwa kusherehesha kwenye utoaji mahari na sendoff na wengine wengi nawapenda,” anasema Gara B na kuongeza:

“Nimesherehesha harusi nyingi, ila kiukweli harusi ya Petro Magoti ilikuwa kubwa mno kwangu, ilikuwa na watu wengi, ilifuatiliwa sana na imetembea mno kwenye mitandao ndani na nje ya Tanzania. Hadi sasa naona video za harusi ile zikijadiliwa katika nchi mbalimbali. Kwangu ni mafanikio makubwa na imezidi kukuza jina langu.”


CHANGAMOTO

Kama zilivyo kazi nyingine, Gara B anasema hata kwenye shughuli zake amekuwa anakumbana na changamoto. Anasema licha ya furaha, lakini zipo kumbukumbu mbaya kwenye kazi yake na katika hili anasema: “Siwezi kusahau siku niliyoendesha harusi kwa dakika 40. Hiyo sherehe ilikuwa inafanyika kwenye ukumbi mmoja maarufu uliopo ghorofani, hata siku moja jengo hilo halijawahi kukatika umeme, lakini siku hiyo ulikatika.

“Nilifika pale mapema umeme hamna tukakaa hadi saa nne haujarudi, shughuli nyingine mfano chakula ilibidi ziendelee. Umeme ulipokaa sawa muda ulikuwa umeshaenda sana, hivyo nikalazimika kumaliza shughuli ndani ya dakika 40 na watu wote walifurahi utafikiri hakuna kilichotokea.”