Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu za jamii kukwepa sheria ndoa za utotoni-2

Msichana ambaye aliolewa kabla ya miaka 18  katika kijiji cha Nyanza wilayani Meatu mkoani Simiyu alipokuwa akifanya mahojiano na Mwananchi Gazeti

Muktasari:

  • Wadau Halmashauri ya Meatu waeleza mikakati inayotekelezwa kukabiliana na mimba na ndoa za utotoni.

Meatu. Licha ya Tanzania kuwa na sheria zinazozuia ndoa na mimba za utotoni, jamii inatumia usiri na uongo kama mbinu ya kuepuka mkono wa sheria.

Mbali ya hayo, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inatajwa kuchochea hali hiyo kwa kuwa inaruhusu wasichana kuolewa wakiwa na miaka 14 kwa idhini ya mahakama na miaka 15 kwa ridhaa ya mzazi.

Katika Kijiji cha Nyanza wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu, mwenyekiti wa kijiji, Msafiri Bushiya anasema baadhi ya wazazi hudanganya umri wa watoto wanapokwenda hospitali kufanya vipimo kabla ya ndoa.

“Wazazi wanafanya udanyanyifu ili kuhalalisha ndoa, mtu anakuja kufanya vipimo akiona mwanaye umri wa ndoa bado na daktari hawezi kukubali anadanganya,” anasema.

Bushiya anasema hilo hutokea kwa watoto wasioendelea na masomo ya sekondari baada ya kufeli mtihani wa darasa la saba au kidato cha pili.

“Akiacha tu shule anaangukia katika ndoa za utotoni, wazazi nao wanaridhia kwa sababu hata wao mwamko wa elimu hawana, wengi wameishia darasa la saba kwa hiyo hawajui hata umuhimu wa elimu,” anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyanza, Makoye Machayi anasema umaskini huchochea wazazi kuruhusu watoto wao kuolewa pasipo kujali umri kwa kuangalia ng’ombe watakazopata.

“Katika jamii hii ya wafugaji si wote wana ng’ombe, sasa akipata nafasi anaona kipato kimeingia na kama anazo anajiongezea bila kujua baada ya muda ng’ombe huisha. Hili linafanyika bila kujali binti anaweza kwenda kuteseka kwa sababu bado mdogo na hawezi kumudu majukumu,” anasema.

Anasema jambo hilo linachochewa na mwamko mdogo wa elimu uliopo kwa jamii ya wafugaji.

“Huwa tunafuatilia wanafunzi wetu, sijawahi kupata kesi kama hizi ila wakimaliza utasikia wamekubaliana huko wamemaliza, au labda hili lifanyike kwa wazazi kusingizia kuhama,” anasema.

Anasema baadhi ya wananchi wamekuwa wakihama kutoka eneo moja kwenda lingine kwa shughuli mbalimbali.

Ofisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mwamvita Juma, anasema mahari inayolipwa ni moja ya vitu vinavyowazuzua wazazi.

Kutokana na umaskini uliopo anasema baadhi ya wazazi wanaona kumruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa mdogo ni kupunguza mzigo ndani ya familia.

“Sababu nyingine ni shinikizo la jamii na utamaduni, mila na desturi hasa za makabila ya wafugaji walioko mkoani hapa zinachangia ndoa na mimba za utotoni kwa kuhimiza wasichana kuolewa mapema,” anasema.

Anasema ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia huchangia pia, akieleza kuna wasichana hupata mimba kutokana na ukatili wa kijinsia.

Anasema ikitokea binti kabakwa wakati mwingine pande mbili hukaa pamoja na kuridhiana kwa sababu tayari binti ana mimba.


Kuhusu sheria, mikataba

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, anasema ndoa za utotoni ni moja ya sababu zinazokwamisha kufikia usawa wa kijinsia hasa katika upande wa elimu.

Anasema takwimu zinaonyesha chini ya theluthi moja ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi hawamalizi ya sekondari kutokana na vikwazo kadhaa zikiwamo ndoa na mimba za utotoni.

"Msichana mmoja kati ya watatu, anaolewa kabla ya kutimiza miaka 18 na mmoja kati ya wanne tayari ni mama kabla ya kufikisha miaka 18. Wasichana kuacha shule, kupata mimba na ndoa za utotoni vina uhusiano wa moja kwa moja. Pindi msichana anapopata mimba, ni vigumu kwake kuendelea na masomo na mara nyingi huishia kuolewa akiwa bado mdogo,” anasema.

Rebeca alifungua kesi akiiomba Mahakama Kuu itoe amri ya kufanyiwa marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kuhusu umri wa kuolewa mtoto wa kike.

Hata hivyo, tangu hukumu ya mahakama itolewe Julai 8, 2016 zaidi ya miaka minane sasa bado hakuna mabadiliko yaliyofanyika.

Mkataba wa kupinga aina zote za ukatili dhidi ya wanawake wa mwaka 1979, Ibara ya 16 unataka wanawake wapatiwe haki sawa na wanaume katika masuala ya ndoa na familia.

Pia, unataja wanawake kuwa na haki ya kuingia kwenye ndoa kwa hiari pasipo kulazimishwa au kupunguzwa uhuru wao.

Mkataba wa Haki za Mtoto wa 1989 unaotafsiri mtoto kama mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, unataka apatiwe haki zikiwamo za kujieleza na kusikilizwa, kupata elimu, kulindwa dhidi ya aina zote za unyanyasaji au kudhalilishwa, ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda haki za watoto katika Ibara ya 12 (haki ya usawa) na Ibara ya 13 (haki ya kibinadamu) ambayo inahusisha haki za mtoto.

“Kitu ambacho natamani sasa ni kuona viongozi kabla ya kampeni waone mabadiliko ya sheria ya ndoa ni suala la kufanyiwa kazi au limeshafanyiwa kazi, Tanzania ina nafasi kubwa ya kuimarisha ulinzi wa watoto hasa wa kike.

“Tunahitaji kuona uwajibikaji katika sheria hii ya ndoa, maana inakuwa kama mbuyu ambao unashindikana kukatwa, sitaki kuamini kuwa viongozi huu mbuyu umewashinda naamini kuwa wanaweza kama wakiamua hivyo. Ni vyema waone umuhimu wa kulifanyia kazi,” amesema.


Nini kifanyike

Mwenyekiti wa Kijiji, Bushiya anasema kwa sababu elimu ndiyo silaha muhimu kwao, kama serikali ya kijiji walikaa na kuweka mikakati kuhakikisha wanafunzi wote wanaotakiwa kwenda shule hawakosi fursa hiyo.

“Tunajitahidi mtoto asome, tumekaa na serikali ya kijiji kuhamasisha kufuatilia watoro na kuwarudisha shuleni kwa sababu tunaamini akimaliza kidato cha nne anakuwa mtu mzima anayeweza kuolewa na anakuwa na elimu sahihi,” amesema.

Amesema ni vyema vyuo vya ufundi vifike hadi ngazi ya vijiji ili kuvuta watoto wengi kusoma fani mbalimbali kuwawezesha kupata ujuzi wa kujitegemea.

“Sheria ziwe kali hasa zinazowabana wazazi ili waweze kutekeleza wajibu wao, hili litasaidia kukomesha ndoa za utotoni,” anasema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mwamvita anasema juhudi zinafanyika kupambana na tatizo hilo.

Anasema wamewatwisha viongozi wa makundi ya kijamii wakiwamo wa dini, jeshi la jadi (sungusungu), vyama vya michezo, wakulima na wafugaji jukumu la kuhamasisha jamii kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike.

“Tuliona katika mapambano haya tuwashirikishe viongozi wetu wa makundi mbalimbali wakiwamo wa dini, watumie majukwaa yao kukemea vitendo hivyo na kusisitiza haki ya kila mtoto wa kike kulindwa dhidi ya ndoa za utotoni,” amesema.

Amesema wamekuwa wakitumia mikutano, warsha na makongamano kutoa elimu juu ya kuzuia ndoa za utotoni kwa kuwalinda zaidi watoto wa kike ambao ndiyo waathirika wakuu.

Amesema wanaisimamia vizuri Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 na marekebisho yake yaliyofanywa na Bunge yanayoweka adhabu kali kwa wanaohusika na ndoa za wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Kifungu cha 60A (4) (Sheria ya Elimu ya mwaka 1978) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh5 milioni kwa mtu yeyote anayesaidia kufungwa ndoa ya aina hiyo na sisi tukishawabaini tunahakikisha tunasimamia suala hili katika vyombo vya sheria,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura anasema ili kupambana na suala hilo wanatoa elimu kwa jamii ili kuona umuhimu wa kuwalea watoto na kuacha tamaa ya kupokea ng'ombe kama mahari kwa watoto wenye umri mdogo.

“Kwa kutumia Jeshi la Polisi tunachukua hatua za kisheria kwa wanaoozesha watoto wakiwa na umri mdogo au kuwapa mimba watoto wadogo kila tunaposikia kuna binti ana mimba,” anasema.

Amesema kampeni ya kitaifa ya kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili kwa watoto nchini Tanzania (Smaujata) wanaitumia katika kupata habari za watoto wanaoozeshwa au waliopata mimba.

“Tumeanzisha klabu za wanafunzi shuleni na kuwapa elimu za mimba za utotoni ili wawe mabalozi wazuri kwa wazazi na jamii wanayoishi,” anasema.

Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Prisca Kayombo anasema mbali na kampeni yenye kaulimbiu: “Mahari kwa mzazi kwa ndoa za utotoni si utajiri” inayotekelezwa kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania, pia wanalitumia Jeshi la Polisi kuhamasisha jamii kuhusu madhara ya ndoa za utotoni na kuchukua hatua dhidi ya wanaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

“Hata hivyo, pamoja na jitihada hizi, bado kuna changamoto katika kutokomeza kabisa ndoa za utotoni katika mkoa huu,” amesema.

Amesema unahitajika ushirikiano zaidi kati ya Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla ili kubadili mitazamo na desturi zinazochangia kuendelea kwa tatizo hilo.