Prime
Mawakili walivyochuana kesi ya mkataba wa bandari-3

Mbeya. Sehemu ya pili ya uchambuzi huu wa kesi ya Mkataba wa IGA, maarufu mkataba wa bandari, tuliona jinsi wakili wa wadai, Mpale Mpoki alivyochambua hoja ya kwanza kama wananchi walishirikishwa ipasavyo kutoa maoni kabla ya kuridhiwa na Bunge.
Leo tunaendelea na wakili wa upande wa walalamikaji, Boniface Mwabukusi. Fuatilia sehemu hii.
Wakili Mwabukusi: Waheshimiwa majaji mimi nitawasilisha (hoja) katika kiini namba moja; halafu nitazungumzia namba nne na tano kwa pamoja.
Kwa kuanza nitaongozwa na Sheria ya Tafsiri ya Sheria Kifungu cha 25 (1) (2) (marekebisho ya mwaka 2019).
Kifungu (1), kinaeleza utangulizi katika sheria ni sehemu ya sheria husika na unapaswa kutafsiriwa kama sheria yenyewe kwa madhumuni ya kusaidia kutoa ufafanuzi na madhumuni ya sheria hiyo.
Kifungu kidogo cha pili kinasema kiambatanisho, jedwali au orodha katika sheria pamoja na maelezo mafupi vitakuwa ni sehemu ya sheria hiyo.
Hoja namba moja; kama kusaini, kuwasilisha na kuridhiwa bungeni mkataba wa IGA kulikiuka Sheria namba 5 na namba 6 za mwaka 2017 za Ulinzi wa Rasilimali na Maliasili za Taifa.
Waheshimiwa majaji kwanza ninaomba Mahakama tukufu wakati ikiangalia maelezo yetu katika kiini (hoja) hiki iende kwenye preamble ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki Rasilimali na Maliasili, namba 5 ya mwaka 2017, hasa aya ya kwanza na ya pili za preamble (dibaji).
Aya ya kwanza kwa tafsiri yangu inahusu msingi mkuu wa malengo na maelekezo ya kisera kama inavyobainishwa katika Ibara ya 1, 8 na 9(f) za Katiba ya Tanzania zinazotambua nchi yetu ni ya kidemokrasia na itapata nguvu na mamlaka yake kutoka kwa watu, huku msingi mkuu ukiwa maslahi ya watu.
Aya ya pili inaeleza sheria za kimataifa zinatambua haki yetu ya jamhuri katika permanent sovereignty (umiliki wa kudumu) ya kufaidi, kutumia na kusimamia maliasili zake.
Vilevile aya ya nne ya preamble inaeleza kuhusu mamlaka, nguvu na haki ya kuhakikisha kwamba mipango na makubaliano yote, yanalinda masilahi ya watu na jamhuri yetu.
Aya ya tano, inaeleza kusudi la kuweka sheria mahsusi ili kuhakikisha umiliki udhibiti maliasili na kulinda ukuu wa Taifa kuhusiana na maliasili zake.
Kifungu cha 11(1) na (2) cha sheria hiyo, kinasema kwa mujibu wa Ibara 27(1) ya Katiba, umiliki wa kudumu wa maliasili zake utahakikisha migogoro ya rasilimali na maliasili hayapelekwi kwenye mabaraza ya nje.
Kifungu (2) kinaeleza kuwa migogoro inayotokana na masuala ya urithi wetu wa asili na maliasili zetu lazima itatuliwe na Mahakama zetu au taasisi nyingine husika ndani ya jamhuri yetu kwa mujibu wa sheria za Tanzania.
Kifungu hicho kinakataza kabisa masuala yote yanayohusu maliasili zetu kwenda kusikilizwa na kuamuriwa na Mahakama za kigeni.
Wakati mkitafakari kuhusu sovereignty kwa mujibu wa sheria hii, naomba mwende kwenye Jedwali la Pili Sura ya Pili, ibara ya 2 (1), (2) (a) na (b) ambayo ime-asset (imetangaza) mamlaka ya nchi kuhusu usimamizi, uratibu na haki ya nchi kutokulazimishwa au kulazimika kupitia mkataba kufanya jambo linaloathiri sovereignty yake.
Sehemu nyingine kwenye hiyo ‘issue’ tunaipata kwenye sheria namba 6 ya mwaka 2017 (Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika mikataba inayohusu Rasilimali na Maliasili za Nchi).
Kifungu cha 5(1) kinaeleza bayana mipango au makubaliano yote kuhusu maliasili na rasilimali yanayofanywa na Serikali katika kipindi cha siku sita za vikao vya Bunge yatapaswa kuripotiwa bungeni.
Kifungu 6(2) kinabainisha ni mambo gani yanaufanya mkataba ujulikane kama una changamoto, ambayo ni kama unaiondolea nchi haki yake ya ukuu katika udhibiti wa maliasili na shughuli za kiuchumi.
Kama unaidhibiti nchi kutumia mamlaka yake kudhibiti wawekezaji kwa kutumia sheria za nchi, kama unatoa upendeleo kwa mwekezaji mmoja baina ya mwingine, kama unaiweka nchi chini ya mamlaka ya kigeni.
Katika ukurasa wa 5 preamble j (IGA- mkataba huo) ikisomwa pamoja na Article (ibara) 2(1) hii inayoitwa IGA was to make a binding agreement and not otherwise (ni makubaliano yanayofunga na si vinginevyo).
Ibara nyingine ya IGA inayo-shake (zinazotikisa) sovereignty (ukuu) ya Taifa hili ni 4(2) inayolifanya Taifa kuwa messenger (tarishi) wa Dubai.
Ni kwamba, Tanzania itawajibika kuwajulisha Dubai kuwepo kwa fursa nyingine za bandari na miundombinu ili kumruhusu Dubai kueleza masilahi yake.
Ibara hii inaondoa sovereignty ya nchi kutumia rasilimali yetu lakini sheria nilizozieleza (za ulinzi wa maliasili) zinazuia nchi kuwekwa chini ya mamlaka ya nchi au mtu mwingine.
Ibara hii pia inainyima nchi yetu uhuru wa kutafuta fursa kwa haki na kutoa upendeleo kwa Dubai au kampuni ya Dubai kinyume na sheria nilizozitaja.
Jambo lingine ambalo naomba Mahakama hii ione kwamba linakinzana na sovereignty ya nchi yetu ni Ibara ya 19 ya IGA. Waheshimiwa majaji ukiisoma Ibara ya 19 inasema …
Edson Mweyunge (Wakili wa Serikali Mkuu anaweka pingamizi)
Waheshimiwa majaji, tunaomba mwongozo wa Mahakama. Msomi wakili Mwabukusi amesema ana-submit (anawasilisha hoja) kwenye issue namba moja. Ili nasi tupate kuelewa namna ya kujibu sijui kama bado yuko kwenye issue hiyo au amekwenda nyingine?
Halafu alieleza ibara za mkataba ambazo ana matatizo nazo. Ibara 19 haipo (kwenye hoja ya kwanza) kama hilo tatizo limeibuka sasa hivi basi afute kesi yake airekebishe ndipo ailete.
Wakili Mwabukusi: Waheshimiwa majaji ninachozungumzia ni kwamba ni namna gani ilivyo illegal (isivyo halali).
Wakili Mweyunge: Waheshimiwa majaji kama anaongelea issue namba moja basi hiyo haina kifungu namba 19. Kwa hiyo tunaomba ajikite kwenye vifungu vilivyo kwenye hiyo hoja tu.
Jaji Mustafa Ismail: Mimi nadhani tuendelee (baada ya kujadilina na wenzake).
Wakili Mwabukusi: Waheshimiwa majaji, nimesema sheria zetu zinataka migogoro ya umiliki wa rasilimali zetu tutumie sheria za ndani, lakini ibara hii imeondoa mamlaka hayo.
Ibara 23(4) ya IGA inafunga na kuondoa kabisa sovereignty ya nchi yetu katika haki yake ya kujiondoa, kuamua kusitisha au kufanya ushirikiano na watu wengine.
Kiini namba nne na tano: Waheshimiwa majaji, katika eneo hili swali la kwanza ni kujiuliza je, IGA ni mkataba au mazungumzo ya kawaida. Kwa kile kilichojiri katika mkutano wa 11 kikao cha 45 cha Juni 10, 2023, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi aliwasilisha bungeni azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa mkataba.
Eneo la kwanza ni kifungu cha 25 cha Sheria ya Mikataba. Mkataba huu unahusu uwekezaji, lakini haujaambatanishwa na nyaraka yoyote au kifungu chochote kinachoonesha huyu mwekezaji DP World au Emirate of Dubai anawekeza kiasi gani.
Hata kwenye appendix za IGA (viambatanisho vya mkataba huo) namba 1 katika phase one (awamu ya kwanza) ya projects (miradi) hakuna kinachoonesha anawekeza nini au kiasi gani zaidi ya kueleza tu vitu anavyopewa kinyume cha cha masharti ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mikataba.
Sehemu nyingine ya changamoto ni capacity (nguvu) maana wameuita mkataba.
Sheria ya Mikataba kifungu cha 11(1) (kinaeleza sifa za mtu mwenye nguvu ya kuingia mkataba, ambazo ni pamoja na mtu ameondolewa nguvu na sheria husika na (2) kinaeleza kuwa mkataba unaoingiwa na mtu asiye na nguvu hiyo ni batili.
Ibara ya 123 ya Katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) inaeleza bayana katika aya ya kwanza kwamba member of Emirates (mwanachama wa umoja huo) anaweza kukamilisha makubaliano na nchi mwanachama.
Tunachokizungumza hapa ni kwamba Dubai hana capacity ya kufanya inter-government agreement (makubaliano na nchi nyingine) katika hii nature (asili) na hakuna instrument (hati rasmi) inayompa mamlaka hayo.
Ibara ya 1 ya Montevideo Convention inatoa sifa ili nchi iweze kutambulika kimataifa katika suala la mikataba mbali na kuwa na watu, mipaka inayotambulika, Serikali lazima iwe na capacity to contract (nguvu ya kuingia mikataba) na nchi nyingine.