MAWAIDHA: Hukumu, adabu za safari kwa Muislamu
Muktasari:
- Allah Mtukufu amesema: “…tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha uumbaji (uumbaji ulivyokuwa) (29:20).
Allah Mtukufu aliamuru waja wake wasafiri katika ardhi, wachunguze na wazingatie neema Zake na ustadi wa uumbaji Wake.
Allah Mtukufu amesema: “…tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha uumbaji (uumbaji ulivyokuwa) (29:20).
Kadhalika amesema: Yeye ndiye aliyeidhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake. Na kwake Yeye ndio kufufuliwa. (67:15)
Safari inampa mtu fursa ya kujitenga na kazi za kila siku na changamoto za maisha, Imam Shafi Allah amrehemu alisema: “Safari ina faida tano: Hufariji huzuni, kupata kipato, elimu, adabu, na ushirikiano na watu waaminifu" Na ni wazi kuwa safari ni njia ya kuweza kutafakari maajabu ya dunia, na kujenga imani kubwa kwa Allah Mtukufu na kuthibitisha kwamba dunia hii ina Mfalme na Mtawala Mkuu anayestahili kuabudiwa pekee yake.
Allah amesema: “Na katika ardhi zipo ishara kwao wenye kuamini” (51:20) Na sababu za safari kwa Muislamu ni nyingi; anasafiri kwa ajili ya ibada ya Hijja au Umra, kutafuta elimu, kupata riziki, kutembelea jamaa au rafiki, n.k.
Adabu za safari
Mosi, kuwa na nia njema. Mtume wa Allah (Rehma na amani zimshukie) anasema: "Vitendo vyote vinategemea nia, na kila mtu atapata kwa mujibu wa kile alichokusudia..”
Ni vema mtu akazingatia madhumuni ya safari yake, iwe ni ya halali, hata kama ni kwa ajili ya kupumzika izingatie sharia na isiwe na upetukaji mipaka au ufujaji ndani yake. Pili: Kujiandaa kwa safari kwa kuwa na fedha za kutosha, usafiri bora, nyaraka zinazohitajika, chakula na kinywaji na kuzingatia muda wa sala.
Tatu: Mtume wa Allah kabla ya kuanza safari alikuwa akiwaaga waumini na familia yake kwa kusema: "Nawaacheni kwa ulinzi wa Allah, dini yenu, uaminifu wenu, na matendo yenu ya mwisho." (At-Tirmidhi). Nne: Kuteua kiongozi wa msafara wanapokuwa watu watatu au zaidi. M
tume wa Allah alisema: "Ikiwa watu watatu wanakwenda safari, wateue mmoja wao kuwa kiongozi." Tano: Katazo la wanawake kusafiri bila kuwa na maharimu, kwa sababu inaweza kuleta fitna kwao au kwa wanaume wanaomzunguka.
Mtume wa Allah alisema: "Hairuhusiwi mwanamke anayemwamini Allah na Siku ya Mwisho kusafiri umbali wa siku moja na usiku mmoja bila maharimu" Sita: Siku bora ya kuanza safari ni Alhamisi asubuhi, Mtume wa Allah alikuwa na tabia ya kupenda kusafiri Alhamisi asubuhi.
Saba: Kukithirisha kuleta dua na nyiradi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allah, mfano wa dua anapokuwa katika chombo cha safari: “Alhamdulillah, Subhanalladhi Sakhkhara lana hadha wa ma kunna lahu muqrinin, wa inna ila rabbina lamunqalibuun “Tasfiri:” Ametakasika aliye mfanya huyu (mnyama) atutumikie, na tusingeli weza kufanya haya wenyewe. Na hakika sisi tutarudi kwa Mola wetu Mlezi. (43:13-14): Ewe Allah, tunakuomba katika safari yetu hii baraka na ucha Mungu.
Kusema: “Allah Akbar” wakati wa kupanda mlima na “Subhanallah” wakati wa kushuka, dua wakati wa kuingia mji au kijiji”Audhu bikalimatillahi Attammaat min sharr maa khalaq” Najiweka chini ya ulinzi wa maneno ya Allah dhidi ya uovu wa kila alichoumba." (Muslim). “...
Allah, tunakuomba kheri ya mji huu na kheri ya watu wake. Na tunaomba kuepuka shari yake na shari ya watu wake." (An-Nasa'i). Nane: Kudumisha kuwa na udhu Mtume wa Allah alisistiza umuhimu wa kuwa na udhu wakati wote, hasa kwa waislamu wanaosafiri. Hii ni kwa sababu udhuna unazuia uchafu wa mwili na roho.
Tisa: Msafiri anapaswa kuwa na tabia nzuri na kuheshimu haki za wasafiri wenzake. Hii ni pamoja na kujipamba na sifa ya upole, ukarimu, kudhibiti macho na kuwa na unyenyekevu kwa wenzake, na kuwasaidia pale wanapohitaji.
Ikiwa wapo katika usafiri mmoja au wanakaa katika chumba kimoja, inapaswa kuwa na adabu ya kuomba ruhusa kabla ya kufungua dirisha au mlango. Kadhalika kufuata adabu za jamii na kutoharibu faraja ya wengine, kwa mfano, kuepuka kuvuta sigara au kusema kwa sauti kubwa kuhusu mambo binafsi, na pia kutokutupa takataka au mabaki ya chakula ili kuhifadhi heshima ya wengine na usafi wa vyombo vya usafiri.
Kumi: Ni sunna kwa msafiri kurudi haraka kwa familia yake baada ya kumaliza safari, na siyo kukaa zaidi ya muda unaohitajika. Mtume wa Allah amesema: "Safari ni kipengele (sehemu) cha adhabu: Inazuia chakula chako, kinywaji chako na usingizi wako.
Hivyo, akishaimaliza haja yake, na harakishe kurudi kwa familia yake." Vile vile ni Sunna kukumbatiana wakati wa kukutana au kurudi kutoka safari: Anas (Allah Amridhie) amesema: Masahaba wa Mtume wa Allah walikuwa wakikumbataiana pindi wanapokutana au wanaporudi safari.”
Kwa mawasiliano zaidi piga: 0744 300 572