Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mavunde asimamisha uchimbaji madini kwenye mito Katavi

Kufuatia ukaguzi uliofanywa kwa wamiliki wa leseni wanaofanya uchimbaji kwenye mto na kuathiri mazingira, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji madini kwenye mito ya Mtisi na Ibindi mkoani Katavi.

Ametoa kauli hiyo Jumatano Mei 13, 2026 wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za uchimbaji madini katika Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Nsimbo Mkoani Katavi.

"Rais Samia Suluhu Hassan ametupa maelekezo mahususi kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa mujibu wa Sheria na zisilete athari kwenye mazingira. Tumeshuhudia sote kinachofanyika hapa ni kinyume na matakwa ya Sheria yetu ya Madini Sura 123.

"Hivyo, naelekeza kuanzia leo shughuli zote za uchimbaji zisimame mpaka pale mtakapotekeleza wajibu wenu kama mlivyoelekezwa na Afisa Madini Mkazi wa Katavi kupitia barua aliyowaandikia. Pia, wamiliki wa leseni wasilisheni mpango wa kuhifadhi mazingira kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji tena", amesisitiza Waziri Mavunde.

Vilevile, Waziri Mavunde amefanya ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi (TSA) waliyoingia wachimbaji wadogo wa kitanzania na wawekezaji wa nje na kubaini mapungufu ambayo yalipelekea kuagiza Ofisi za Afisa Madini Wakazi wa Mikoa ya kimadini kufanya ukaguzi wa mikataba ya TSA nchi nzima ili kubaini iwapo inawanufaisha watanzania na inazingatia matakwa yaliyowekwa kisheria.

Akieleza utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maeneo ya uchimbaji, Mavunde alitoa maelekezo kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kutoa Hati ya Makosa (Default Notice) kwa wamiliki wote wa leseni za utafiti wasioendeleza na kufuata masharti ya leseni hizo.

"Lengo ni kuyafuta maeneo yote ya leseni za utafiti yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo kupitia vikundi vyao. Aidha, maeneo mengine yatatumika kugawa maeneo kwa wachimbaji wadogo vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia programu ya Mining for A Brighter Tommorow (MBT)" amebainisha Waziri Mavunde.

Akibainisha juu ya leseni alizozifuta mwezi uliopita, Waziri Mavunde alitangaza kutenga leseni 3 za utafiti ili zigawiwe kwa wachimbaji wadogo Mkoani Katavi, ambapo wachimbaji wadogo walishukuru na kupongeza jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kuwasikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa wakati.

Awali, Waziri Mavunde alieleza kuwa amefika kufanya ziara mkoani Katavi kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba aliyoyatoa alipofanya ziara ya kikazi mkoani Katavi.

Akitoa maelezo ya Mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu ameishukuru Serikali kwa hatua za utatuzi wa changamoto za wachimbaji mkoani Katavi na kuahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mavunde yanakwenda kusimamiwa ipasavyo ili yalete tija na kuimarisha shughuli za uchimbaji.

Kwa upande wake wabunge Haidary Sumry (Mpanda Mjini) na Anna Lupembe (Nsimbo) walimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuisimamia ipasavyo Serikali ambayo imekuwa ni mhimili imara katika kutatua changamoto za wananchi wa majimbo yao.