Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh174.98 bilioni kutekeleza vipaumbele vinane sekta madini

Waziri wa Madini, Anthony wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo, Jumatatu Aprili 27, 2026 bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Serikali imesema katika mwaka wa fedha 2026/27 imeweka kipaumbele katika kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa

Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameliomba Bunge kumuidhinishia Sh174.98 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya utekelezaji wa vipaumbele vinane vya wizara hiyo.

Vipaumbele hivyo ni kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa na kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati.

Vingine ni kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani wa madini, kuimarisha uendeshaji minada na maonesho ya vito, kuongeza uwekezaji kwenye tafiti, kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara.

Kati ya fedha hizo, amesema Sh71.5 bilioni sawa na asilimia 40.87 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh103.47 bilioni sawa na asilimia 59.13 kwa matumizi ya kawaida.

Mavunde amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Aprili 27, 2026 aliposoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa wizara hiyo.

Akifafanua kipaumbele cha kwanza, Mavunde amesema wizara itaweka nguvu katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuimarisha usimamizi wa rasilimali madini.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza mapato ya ndani yanayotokana na sekta ya madini na kuboresha mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Katika kipaumbele kingine, amesema wizara inalenga kuendeleza kasi ya ukuaji wa sekta hiyo ili mchango wake kwa uchumi uendelee kuongezeka.

“Hilo linaenda sambamba na mkakati wa kuendeleza mnyororo wa thamani katika rasilimali zenye ushindani mkubwa duniani,” amesema Mavunde.

Waziri huyo, amesema Serikali pia imeweka mkazo katika kuhamasisha uwekezaji na kuongeza thamani ya madini nchini, sambamba na kuimarisha minada na maonesho ya madini ya vito ili kuongeza ushindani wa soko na fursa za biashara.

Kwa upande wa tafiti, amesema bajeti hiyo inalenga kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za kina za madini ili kufungua maeneo mapya ya uchimbaji na kuongeza taarifa za kijiofizikia na kijiolojia zitakazochochea uwekezaji.

Kwa wachimbaji wadogo, amesema Serikali itaendelea kuweka mkazo kwenye urasimishaji na maendeleo yao ili kuongeza tija na kuwajumuisha zaidi katika uchumi rasmi.

“Tunalenga kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara,” amesema.