Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yalenga kushindana uwekezaji wa madini duniani

Waziri wa Madini, Anthony wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo, Jumatatu Aprili 27, 2026 bungeni jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Wizara ya Madini, imesema dhamira yake ni kuifanya Tanzania kuwa na ushindani katika uwekezaji wa madini duniani.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inalenga kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza ushindani wa nchi katika sekta ya madini duniani na kuvutia mitaji zaidi kupitia mageuzi ya kisera, tafiti za madini na maendeleo ya miradi ya kimkakati.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameeleza malengo hayo akiwa ameoliomba Bunge, limuidhinishie bajeti ya Sh224.98 bilioni kwa ajili ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Waziri huyo ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu Aprili 27,2026 aliposoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema hatua zinazopangwa kutekelezwa zinalenga kujenga mazingira yanayoifanya Tanzania kuendelea kuonekana eneo lenye mvuto wa uwekezaji katika sekta ya madini.

Amesema miongoni mwa viashiria vinavyoonesha mwelekeo huo ni kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika viwango vya kimataifa vya kuvutia uwekezaji.

“Katika kiashiria cha kuvutia uwekezaji, Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 73 mwaka 2023 hadi nafasi ya 52 mwaka 2024. Aidha, katika kipengele cha sera, Tanzania imepanda kutoka nafasi ya 81 mwaka 2023 hadi nafasi ya 59 mwaka 2024,” amesema.

Amesema maboresho hayo yanakwenda sambamba na hatua za wizara kuongeza uwekezaji katika tafiti za kina za madini, jambo alilosema linaongeza uhakika kwa wawekezaji na kufungua maeneo mapya ya uchimbaji.

Katika hotuba hiyo, Mavunde amesema Serikali itaendelea kusukuma mbele utafiti wa madini muhimu na madini mkakati yanayoongeza ushindani wa nchi kwenye uchumi wa kimataifa, hususan katika kipindi ambacho dunia inaelekea zaidi kwenye mahitaji ya madini ya teknolojia na nishati safi.

“Tunalenga kuendeleza mnyororo wa thamani katika madini muhimu na madini mkakati, kuhamasisha uwekezaji na uongezaji thamani ya madini na kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za madini za kina,” amesema.

Amesema mwelekeo huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuongeza imani ya wawekezaji katika sekta hiyo.

Mavunde, amesema moja ya maeneo yanayopewa uzito ni maendeleo ya mradi wa Liganga na Mchuchuma pamoja na miradi ya madini muhimu, ambayo inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji na thamani ya sekta hiyo kwa muda mrefu.

“Wizara itaendelea kuratibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya madini, kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje, pamoja na kuimarisha mazingira ya biashara na ushindani katika sekta ya madini,” amesema.

Katika hotuba hiyo amesema uwekezaji hautajengwa tu kwa leseni na mitaji, bali pia kwa kuimarisha mifumo ya biashara ya madini, masoko, minada na miundombinu ya taarifa za kijiofizikia na kijiolojia.

Amesema hatua hizo zitasaidia kupunguza hatari kwa wawekezaji na kuongeza uaminifu wa soko la Tanzania.

Mavunde, amesema Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na rasilimali zake bila kupunguza mvuto kwa wawekezaji.

“Kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye ukuaji wa Pato la Taifa na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini,” amesema.

Mwelekeo wa Serikali, amesema ni kuifanya Tanzania siyo tu kuwa nchi yenye rasilimali, bali pia eneo lenye ushindani, uhakika wa sera na mazingira rafiki kwa mitaji ya muda mrefu katika sekta ya madini.