Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Niliona wakimpiga risasi, kutoroka na bodaboda-2

Moshi. Agosti 7, 2013 jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa kwa risasi, mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, tukio lililotokea wilayani Hai.

Wauaji wa mfanyabiashara huyo waliokuwa na pikipiki walitumia mbinu ya kumshawishi kumuuzia madini ya Tanzanite na kumvuta hadi eneo la Orkolili Mijorohoni, ambapo walimminia risasi 22 kwa kutumia bunduki aina ya SMG.

Mwili wake ulikutwa na matundu 26 ya risasi, madogo 13 yakiwa ya sehemu ambayo risasi ziliingia na 13 zilipotokea zikiwa zimechakaza utumbo mwembamba, kuharibu figo, mishipa ya damu na bandama.

Katika toleo la jana, tulikuletea ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, Mrakibu wa Polisi (SP), Joash Yohana, aliyekuwa mkuu wa upelelezi (OC-CID) wilaya ya Hai, alieleza namna walivyoukuta mwili wa marehemu na hali yake.

Leo tunakulete ushahidi wa shahdi wa pili wa Jamhuri, Noel Thomas (19) ambaye ni kijana wa kimasai ambaye siku ya tukio, alishuhudia mauaji hayo katika Kijiji cha Orkalili, Wilaya ya Hai, pembezoni ya barabara kuu ya Moshi-Arusha. Endelea ...


Aliyoyashuhudia

Akitoa ushahidi wake Oktoba 6, 2015 kwa kuongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Stella Majaliwa, shahidi wa pili, Noel Thomas alisema siku ya tukio asubuhi alitoka kijijini na kupeleka mifugo malishoni Barabara ya Moshi-Arusha.

“Nikiwa njiani nikitokea kijijini Orkalili kwenda barabara ya Moshi-Arusha, nilikutana na watu wawili waliokuwa na pikipiki pembeni ya barabara ya lami (eneo la mijohorni). Mmoja alikuwa amekaa kwenye kiti cha pikipiki,” alisema.

“Baadaye ikaja gari ikitokea uelekeo wa Bomang’ombe kwenda KIA, ikasimama na kupiga honi. Huyo mtu aliyekuwa ndani ya gari akapungiwa mkono wa ishara na wale waliokuwa na pikipiki. Hapo akaendesha gari lake kuwafuata walipo,” alisema.

“Mmoja kati ya wale watu alimfuata mwenye lile gari na mwingine alisimama nyuma ya ile gari. Kwa wakati huo nilikuwa nimesimama umbali wa hatua 30 kutoka mahali walipokuwa hao watu na lile gari,” alieleza Thomas.

“Nikaona yule mtu akishuka kwenye gari lake na hapo nikamuona yule mtu aliyekuwa upande wa nyuma wa gari akimpiga risasi yule mwenye gari. Alijaribu kukimbia kuelekea barabarani akipiga kelele kuomba msaada lakini akaanguka.

“Baadaye hao watu (wauaji) walirudi kwenye pikipiki yao na kuondoka nayo kwa spidi kuelekea Kijiji cha Olmelili. Kabla hawajaenda mbali ikaja pikipiki nyingine ya pili wakaungana pamoja na kuondoka pamoja,” alieleza Thomas.

Thomas alisema pikipiki hiyo ya pili ilitokea barabara ya vumbi ya Boma-KIA.


Nguo walizovaa wauaji

Akiendelea kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alisema anayakumbuka mavazi waliyokuwa wamevaa wale waliokuwa na pikipiki na kwamba yule aliyeenda kuongea na mwenye gari (Bilionea Msuya) alikuwa amevaa koti jeusi.

“Yule aliyekuwa amesimama nyuma ya lile gari (aliyemshambulia kwa risasi bilionea Msuya) alikuwa amevaa jaketi la rangi ya udongo. Nakumbuka pia rangi ya ile pikipiki yao ilikuwa nyekundu. Sikuona vizuri sura za hao watu,” alisema.

Akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili Emmanuel Safari aliyemtetea mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu, shahidi huyo alisema watu waliokuwa na pikipiki walikuwa upande wa kulia wa barabara ila hakukariri namba ya pikipiki.

“Gari (ya bilionea Msuya) ilitokea uelekeo wa Boma kuelekea KIA ndio likasimama. Mtu akatoka ndani ya gari. Sikufahamu walikuwa watu wangapi kwenye gari ila nilimuona mmoja tu ambaye ndiye alikuwa akiendesha,” alieleza.

“Mmiliki wa hiyo gari aliitwa na hao waliokuwa na pikipiki. Alipewa ishara ya kuwafuata. Gari ilikuwa ya rangi ya udongo. Nafahamu ziko rangi tofauti tofauti za udongo. Sijawahi kuwaona wale watu waliokuwa na pikipiki,” alimaliza ushahidi.


Pikipiki ilivyopata pancha

Kwa upande wake, shahidi wa tatu, Raphael Karoli (58) mkazi wa Embukoi wilayani Siha katika ushahidi wake alisema Agosti 7, 2013, alikuwa nyumbani kwake na kulikuwa na sherehe na siku hiyo walikuwa wamechinja mbuzi kwa ajii ya sherehe.

Kwa sababu lilikuwa ni eneo la wazi, aliona watu wawili wakija na pikipiki na walipopita na kukaribia korongo, pikipiki yao ilipata pancha gurudumu la mbele, ndipo walishuka na kuvuka mto usio na maji na kwenda upande wa pili.

“Walitaka kwenda msituni na hii ilitushtua, tukawa tunajiuliza hawa ni akina nani. Tulikuwa kundi la watu 10. Tulienda mbele yao na kuwazuia tukitaka kujua wao ni nani. Badala ya kutujibu wakaondoka na kuingia kwenye lile korongo,” alisema.

“Mmoja alivuka korongo na kutoroka. Mwingine akaenda upande wa pili. Huyu alikuwa amevaa jaketi kubwa la kaki kama la polisi. Alikuwa na kitu kizito pia amekivingirisha mkononi. Tulipiga kelele ili waliopo upande wa pili wasikie.”


Muuaji awatawanya kwa SMG

(Baada ya kupiga kelele) “Huyo mtu akatoa bunduki akafyatua risasi hewani. Baadhi yetu tulianguka na wengine wakakimbia. Wakati huyo mtu anakimbia alidondosha jaketi lake na hakuweza kuliokota kwa sababu tayari tulikuwa tumefika karibu naye,” alieleza.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, hakuweza kumtambua mtu huyo aliyefyatua risasi hewani ila waliwasiliana na Polisi Sanyajuu nao waliwashauri wawapigie polisi wa Bomang’ombe wilayani Hai, na walipofika ndio wakasema (wale watu) wameua mtu.

Shahidi huyo alisema akiliona jaketi ambalo lilitelekezwa mbele yake anaweza kulitambua na akasema anaweza pia kutambua pikipiki na alitaka kutoa pikipiki kama kielelezo lakini wakili Emmanuel Safari akawasilisha pingamizi.

Wakili huyo alisema shahidi huyo hajaweza kuitambua vizuri pikipiki hiyo na hajui kusoma wala kuandika na kwamba upande wa mashtaka ulipaswa uwe umeleta pikipiki tofauti tofauti zinazofanana muundo, ili shahidi aweze kuitambua.

Akijibu hoja hiyo, Wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula alisema shahidi wao alisisitiza anaweza kutambua namba ya pikipiki lakini kama suala ni kuwa na pikipiki zaidi, akaomba ahirisho fupi ili kuwewezesha kutafuta pikipiki hizo.

Katika uamuzi wake, Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo alisema pingamizi la Wakili Safari linakubaliwa na kuwa mahakama hairuhusu shahidi aitambue pikipiki aliyoitaja kama nyekundu, bali angeeleza taarifa zaidi kuhusu pikipiki hiyo.

Akijibu maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili Hudson Ndusyepo aliyetaka kufahamu ni nani hasa aliyeokota lile jaketi, shahidi huyo alisema walikuwa zaidi ya watu 10 na ni wao wote waliokota isipokuwa ni ‘kijana mmoja’ ndiye aliyelichukua.

Kwa upande wake, Wakili Majura Magafu alitaka kufahamu shahidi anajuaje ana umri wa miaka 58 na kama umeongezeka wakati hajui kusoma wala kuandika, naye akasema hajui kama umeongezeka ila ni umri huo huo ambao aliwatajia polisi.

“Ninachojua nina miaka 58, basi. Siwezi kusema kwa uhakika muonekano wa wale watu waliokuwa na pikipiki kwa sababu sikuwa karibu yao. Sikusema kuwa mmoja wa hao watu alikuwa mnene na mrefu. Ninachokumbuka mmoja alivaa jaketi.”

Usikose kusoma mwendelezo wa kesi hii kesho