Matumizi ya 5G Tanzania yatakavyonoga

Dar es Salaam. Kampuni ya YAS Tanzania imetangaza ushirikiano na Samsung Electronics East Africa kwa kuzindua simu mpya za Samsung Galaxy S25 Series, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya teknolojia ya 5G nchini.
Ushirikiano huu unalenga kuimarisha upatikanaji wa mtandao wa kasi wa 5G na kuwezesha wateja kufurahia huduma bora za kidijitali.
Kwa maboresho ya mtandao wake, YAS imefanikisha upanuzi wa 5G katika Dar es Salaam, Zanzibar, na Dodoma, ikiwezesha kasi ya hadi 1Gbps na kuiweka Tanzania katika ramani ya teknolojia ya kisasa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ikunda Ngowi, Meneja wa Wateja wa Kati na Vijana wa YAS, amesema ushirikiano huu utaongeza kasi ya upatikanaji wa 5G na kuboresha matumizi ya intaneti kwa wateja wa Tanzania.
"Ushirikiano huu ni hatua muhimu kwa ukuaji wa teknolojia ya 5G nchini. Tumeboresha mtandao wetu kuhakikisha wateja wanapata kasi na ufanisi wa hali ya juu katika matumizi ya intaneti," amesema Ngowi.
Meneja wa Samsung Electronics East Africa Tanzania, Manish Jangra, amesema simu mpya za Samsung Galaxy S25 Series zimeundwa kwa teknolojia ya kisasa ili kufanikisha matumizi bora ya 5G.
"Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata fursa ya kufurahia faida za 5G kupitia vifaa vya hali ya juu," amesema Jangra.
Faida kwa wateja wa YAS
Ili kuwahamasisha wateja wake kutumia 5G, YAS inatoa GB 96 za intaneti bure kwa mwaka mzima kwa kila mteja atakayenunua moja ya simu mpya za Samsung katika maduka yake.
Ushirikiano huu unaweka Tanzania kwenye mwelekeo wa mapinduzi ya kidijitali, huku YAS ikiendelea kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha wateja wake wanapata huduma bora zaidi za mtandao wa kasi.