Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumaini kurejeshewa fedha, mali za Deci yazimika rasmi

Dar es Salaam. Matumaini ya viongozi wa kampuni ya upatu iitwayo Development Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), kukomboa na kurejesha mali zao zilizotaifishwa na Serikali kwa amri ya Mahakama, yamefutika rasmi baada ya rufaa yao kutupiliwa mbali.

Viongozi hao wa Deci, Jackson Sifael Mtares, Dominic Kigendi, Timotheo Saiguran Ole Loitg’nye na Samwel Sifael Mtares walifungua maombi ya marejeo wakiiomba Mahakama hiyo irejee na hatimaye kubadilisha hukumu ya rufaa yao waliyoikata wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyoamuru kutaifishwa mali hizo.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Stella Mugasha, Ignas Kitusi na Gerson Mdemu, Agosti 21, 2023 imetupilia mbali ombi hilo ikisema sababu zao za marejeo hazina mashiko. Hii ilikuwa ni mara ya tatu na hatua ya mwisho katika jitihada zao za kurejesha mali hizo kwa mkondo wa sheria na mjadala wa kutaifishwa mali hizo umefungwa. Hakuna hatua nyingine wanayoweza kuichukua iwe ni kufungua maombi mengine wala rufaa nyingine kwa kuwa Mahakama ya Rufani ndiyo ngazi ya juu kabisa na ya mwisho nchini katika muundo wa Mahakama.

Katika shauri hilo la maombi namba 608/01 la mwaka 2021 dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP), walikuwa walitoa sababu nne zenye jumla ya vipengele 13, wakidai lilikuwa na makosa ya dhahiri katika uso wa hukumu iliyoamuru kutaifishwa mali hizo na hivyo kusababisha haki kutokutendeka.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, waombaji waliwakilishwa na Wakili Francis Stolla, huku Serikali ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro na Wakili wa Serikali Mwandamizi Anita Sinare.

Hata hivyo, kabla ya kuanza usikilizwaji Mahakama ilitaka kujiridhisha uhalali wa shauri hilo.

Wakili Stolla alidai shauri hilo lilikuwa halali kwa kuwa lilikuwa linahitaji Mahakama kubatilisha uamuzi huo kwa madai kwamba DPP hakuwa na mamlaka kisheria kufungua shauri la maombi ya utaifishaji mali hizo.

Wakili Kimaro kwa upande wake, alidai shauri hilo halikustahili, kwani lilikuwa linalenga kufungua upya usikilizwaji wa rufaa kwa kuwa hakuna sababu kati ya zilizotolewa ambayo imekidhi vigezo kuifanya Mahakama ifanye marejeo ya uamuzi wake.

Badala yake alisema sababu hizo zilikwishatolewa awali katika rufaa yao na zikasikilizwa na kuamuriwa kwa ukamilifu katika uamuzi huo waliotaka ufanyiwe marejeo.

Pia wakili Kimaro alieleza kuwa shauri la maombi ya kutaifisha mali hizo lililofunguliwa na DPP Mahakama Kuu, mwaka 2019 lilikuwa sawasawa.

Alifafanua DPP ana mamlaka ya kufanya hivyo chini ya kifungu cha 9 cha Sheria ya Mali zitokanazo na Uhalifu (Poca) kama ilivyorekebishwa kupitia Sheria namba 7 ya mwaka 2018. Hivyo aliiomba Mahakama itupilie mbali shauri hilo.

Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kurejea sheria na kanuni zinazoipa mamlaka na kubainisha sababu na vigezo vya kufanya marejeo ya hukumu zake, imekubaliana na hoja za Kimaro kuwa shauri hilo halina nguvu ya kusimama mahakamani.

Imebainisha kifungu cha 4(4) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, kinaipa mamlaka ya kufanya marejeo ya hukumu zake ili kusahihisha makosa yanayokuwa yametokea katika hukumu zake na kusababisha haki kutokutendeka.

Hata hivyo, imesema kanuni ya 66(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani inabainisha sababu za kufanya marejeo, akisisitiza marejeo hayapaswi kuwa mlango wa nyuma wa rufaa ambayo ilishaamuriwa kwa sababu zilezile, jambo lisiloruhusiwa kwa kuwa ni suala la kisera kwamba mashauri lazima yafikie mwisho.

Katika uamuzi huo Mahakama hiyo ilisema hoja zao walalamikaji kulalamikia uamuzi wa awali kwamba wadaawa wenye masilahi wameporwa haki ya kusikilizwa.

Ilisema jambo hilo halina mashiko kwa kuwa hao wadaawa wenye masilahi hawahusiki katika shauri hilo, kwani mbali na kwamba katika hatua ya marejeo si jukwaa sahihi ambapo mdaawa mpya anaweza kudai haki, kwa kuwa ni nje ya matakwa ya Kanuni ya 66(1).

Pia imefafanua katika uamuzi unaopingwa Mahakama imeeleza bayana ingawa taarifa ya usikilizwaji wa shauri la maombi ya kutaifisha mali hizo ilitolewa kwa waombaji na umma kwa jumla kujitokeza Mahakama Kuu kusikilizwa, hakuna wengine waliojitokeza kusikilizwa kama wanahusika na mali hizo.

“Sababu ambazo marejeo yanatafutwa katika shauri hili zote zinazunguka katika sababu ya kwanza na ya tatu za rufaa ambayo ilishaamuriwa na Mahakama hii,” ilibainisha Mahakama hiyo katika uamuzi huo.

Hivyo ilisisitiza kuwa sababu walizozitoa hazikidhi matakwa ya kanuni hiyo ya 66(1) ya Kanuni za Mahakama inayobainisha sababu za mahakama kufanya marejeo ya uamuzi wake wa awali. “Hivyo baada ya kuzingatia sababu zilizotumiwa kuomba marejeo, tumejiridhisha hazikidhi sharti lililobainishwa chini ya Kanuni ya 66(1) kuwezesha Mahakama kutumia mamlaka yake ya kimarejeo. Kwa hiyo shauri hili halina ustahilifu na linatupiliwa mbali.”

Uamuzi wa kutaifishwa mali za Deci zikiwemo pesa taslimu Sh14.1 bilioni, zilizoko katika akaunti za benki mbalimbali jijini Dar es Salaam, majumba na viwanja katika mikoa mbalimbali na magari ya kifahari ulitolewa na Jaji Stephen Magoiga, Mahakama Kuu,

Jaji Magoiga alifikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za maombi ya DPP kuwa mali hizo zilitokana na kuendesha shughuli za upatu na kukusanya pesa kutoka kwa umma bila kuwa na leseni.

DPP alifungua maombi hayo Machi mwaka huu, miaka sita baada viongozi hao wa Deci kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2009, kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu, kinyume cha sheria.

Viongozi hao waliokuwa wachungaji, viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekosti, walitiwa hatiani kwa kosa hilo mwaka 2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya Sh21 milioni. Walilipa faini hiyo na kuepuka kifungo.