Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maofisa wa ulinzi kutoka nchi 17 watua nchini kujifunza utalii katika usalama wa Taifa

Muktasari:

  • Maofisa hao kupitia Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), wametua jijini Arusha jana Novemba 10, 2025 na watakamilisha mafunzo Novemba 15, 2025 kwa kutembelea hifadhi mbalimbali za Taifa na bonde la Ngorongoro.

Arusha. Zaidi ya maofisa 72 wa ulinzi na usalama kutoka nchi 17, ndani na nje ya Afrika, wametua jijini Arusha kwa ziara ya siku tano kujifunza kwa vitendo namna sekta ya utalii inavyochangia ustawi wa uchumi na usalama wa Taifa.

Maofisa hao kupitia Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), wametua jijini Arusha jana Novemba 10, 2025 na watakamilisha Novemba 15, 2025 kwa kutembelea hifadhi mbalimbali za Taifa na Bonde la Ngorongoro.

Akizungumzia ujio wa maofisa hao, Mkuu wa Chuo cha NDC, Meja Jenerali Wilbert Ibuge amesema katika msafara huo wameambatana na wakufunzi waandamizi elekezi pamoja na washiriki wa kozi ya 14 ya mafunzo ya muda mrefu, iliyoanza Septemba 2025 na itahitimishwa Julai 2026.

Mkuu wa chuo cha taifa cha ulinzi (NDC) balozi meja jenerali Wilbert Augustine Ibuge akizungumza kwenye mafunzo hayo

Amesema lengo la kutembelea Mkoa wa Arusha ni kwa ajili kupata mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi hao wanaojifunza usalama wa taifa na mikakati.

“Unajua usalama wa Taifa unajumuisha sekta zote zinazohusika na maendeleo ya nchi, ndio maana tuko hapa kwenye eneo la kitovu cha utalii kuona na kujifunza kwa vitendo jinsi utalii unavyochangia katika usalama wa Taifa,” amesema.

Amesema ziara hiyo ni utaratibu wa NDC kutembelea Arusha kila mwaka kutokana na nafasi yake kama kitovu cha utalii nchini na eneo muhimu katika mifumo ya kiulinzi, kiuchumi na kimkakati.

“Chuo hiki ni cha kimataifa na mwaka huu tuna washiriki kutoka nchi rafiki 17 ambao wanajifunza kwa undani mikakati ya utalii, uendelevu na mchango wake kwa usalama wa Taifa,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amewakaribisha washiriki hao na kusema mkoa huo ni kitovu cha utalii nchini na unaendelea kuimarika kiuchumi kwa kasi, hasa katika maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ikiwemo kubuni mazao mapya ya utalii.

Washiriki hao ni kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi, Namibia, Botswana, Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Sierra Leone, Ethiopia, India, Misri, Bangladesh na Nigeria.

Katika kipindi cha siku tano, watatembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii na maeneo ya kitamaduni jijini Arusha ili kupata uelewa wa kina kuhusu usimamizi na mchango wa utalii kwa Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Kanali Bhekisile Audrey Mathonsi kutoka Afrika Kusini amesema wanashiriki programu maalumu ya ‘Tentative Programme for Economy in Tourism’, inayolenga kuchunguza mchango wa utalii katika kukuza uchumi, kudumisha diplomasia na kuimarisha usalama wa Taifa.

“Tuone jinsi Tanzania ilivyojipanga na namna jamii inavyonufaika na utalii shirikishi, lakini pia jinsi imeweka mikakati thabiti kuhakikisha sekta hii inaendelea kuimarisha uchumi na usalama wa nchi.” amesema.

Naye Frank Mbando, mshiriki wa kozi ya 14 kutoka Tanzania, amesema ziara hiyo itawasaidia kuona kwa vitendo yale wanayofundishwa darasani kuhusu usalama wa nchi na mikakati ya kiuchumi kupitia utalii.

“Tumejionea jinsi utalii unavyochangia zaidi ya asilimia 25 ya Pato la Taifa (GDP) na ziara hii inatuwezesha kuelewa uhalisia wa changamoto na fursa zilizopo kwenye sekta hii muhimu.” amesema.