Mambo haya kuongeza wanawake kwenye sayansi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira,Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Muktasari:
- Ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati bado ni mdogo licha ya juhudi za wadau katika eneo hilo.
Dodoma. Serikali imetaja mambo manne yatakaosaidia ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi ikiwemo kuanzisha mifumo rafiki ya kumotisha kwa wanaoshiriki na kufanya vizuri katika sayansi, teknolojia, uhandisi, hisabati (Stem).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira,Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete leo Jumanne, Februari 11, 2025 wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Wanawake na Wasichana katika Sanyasi yanayofanyika jijini Dodoma.
Amesema Serikali na wadau wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kuongeza michango na ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, kiuchumi na kijamii.
Ridhiwani amesema mikakati ya kuimarisha, kuratibu na ufugamanishaji mipango, programu na juhudi nyingine zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati na nyanja nyingine za kisayansi.
Pia amesema jingine ni kufanyika kwa tafiti mahususi zinazolenga kubainisha hali halisi ya idadi ya wanawake na wasichana wanaojiunga katika ngazi mbalimbali za elimu nchini katika kipindi kizichozidi miaka 10.
Amesema kuendesha programu kabambe baina ya sekta za umma na sekta binafasi zinazolenga kuleta mapunduzi katika ushiriki na mchango wa wanawake na wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (stem).
Aidha, Ridhiwani ametaja jambo la nne ni kuanzisha mfumo rafiki wa utoaji wa motisha kwa wanawake na wasichana wanaoshiriki na kufanya vizuri katika sayansi, tafiti na ubunifu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, anaeshughulikia Elimu Msingi, Dk Charles Mahera amesema Serikali itaendelea kuandaa walimu wazuri wa masomo ya sayansi kwa lengo la kuwasaidia wanawake na wasichana wapende kusoma masomo ya sayansi.
"Kwa kuzingatia wanawake na wasichana ni asilimia 51.7 tukihakikisha wanasoma masomo haya tutaongeza ubunifu katika teknolojia na katika masomo ya Sayansi. Tuna na mshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzidi kuwekeza katika elimu pamoja na kujenga shule za wasichana katika mikoa yote Tanzania,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anaeshughulikia vyuo vikuu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi amesema maadhimisho hayo yanalenga kuhamasisha na kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika nyanja za sayansi, uhandisi na hisabati ili kupata wataalamu wengi katika siku za usoni.
Amesema Tanzania tangu mwaka 2021 imeungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku hiyo ili kuchagiza ushiriki na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mussa Sima amesema kamati inafurahi kwa jinsi ambavyo Serikali inahakikisha wanafunzi wa vyuo vya kati wanapata mikopo.
Amesema zaidi ya vijana 250 wa vyuo vya kati wamepatiwa mikopo na 700 wanatarajiwa kupatiwa kwa mwaka huu.