Mama aliyeporwa mtoto mwenye ualbino ahama kijiji, akata tamaa

Picha ya mtoto Asimwe Novath (2).
Muktasari:
- Asimwe aliibwa mbele ya mama yake na watu wasiojulikana, kisha kutoweka naye kusikojulikana Mei 30, 2024.
Muleba. Zikiwa zimepita siku 14 bila kupatikana kwa mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) aliyeibwa na watu wasiojulikana, mama wa mtoto huyo, Judith Richard (20), amesema amekata tamaa na kuamua kuhama makazi akisema hawezi kuishi tena eneo hilo bila mwanawe.
Asimwe aliporwa akiwa amepakatwa na mama yake aliyekuwa amekaa sebuleni ndani ya nyumba yao na watu wasiojulikana Mei 30, 2024.
Mama huyo aliyekuwa akiishi na mume na mtoto huyo katika Kitongoji cha Mbale kijiji cha Bulamula Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, amehamia nyumbani kwa mama yake mzazi, Odina Richard (40) katika kijiji cha Kanoni, Kata ya Kamachumu wilayani humo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 12, 2024, Judith amesema sababu za kuhama kijijini hapo alipozaliwa ni upweke wa kumkosa mtoto wake aliyeporwa mbele yake, huku mumewe akiendelea kushikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
“Nimeshindwa kuishi bila mwanangu Asimwe kwenye nyumba yetu kwa sababu nilikuwa nimezoea kumuona kila siku, siwezi kuishi bila yeye. Pia siwezi kuishi bila mume wangu ambaye ameshikwa na polisi mpaka sasa, nasikia na vikundi vya ulinzi shirikishi vimezuiliwa kumtafuta sijajua tatizo nini,” amedai mama huyo.
“Siku 14 zimepita bila kupata majibu ya wapi alipo mtoto wangu, kama mume wangu anahusika polisi si waseme kuwa anahusika, maana nasikia kuna watu wa Kemondo (Bukoba) na Geita wanahusishwa pia, kwanini Polisi wasitoe majibu? Mimi sipo kijijni hapo nimeenda nyumbani kwetu naishi na mama kwa sasa,” amesema Judith alipozungumza na Mwananchi kwa simu.
Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga kuzungumzia suala hilo amesema mtoto huyo bado hajapatikana, licha ya kasi ya kumtafuta kuongezwa.
“Bado hatujakata tamaa tunaendelea kumtafuta mtoto, juhudi zipo zinaendelea licha ya mimi kwenda likizo. Kuhusu vikundi hivyo, sina taarifa kamili kama Jeshi la Polisi limevisitisha,” amesema Dk Nyamahanga.
Mwananchi Digital liliutafuta uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera bila mafanikio.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Yusuph Daniel alipoulizwa na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Juni 11, 2024 kuhusu utafutaji wa mtoto huyo ulipofikia alisema jeshi hilo litatoa taarifa kamili wiki ijayo.
“Nahisi tutazungumza next week (wiki ijayo) kuhusu mtoto huyo tulipofikia katika uchunguzi wa shauri hilo,” alisema Kamanda Daniel.
Mpaka sasa watu wanne bado wanashikiliwa na jeshi hilo kuhusiana na kuibiwa mtoto huyo, akiwemo baba yake mzazi, Novath Venant (24).
Kuhusu zilipofikia jitihada za vikundi vinne vya ulinzi shirikishi vilivyoundwa kumsaka mtoto huyo, kikiwemo cha wawindaji na mbwa, Diwani wa Kamachumu, Lodigard Chonde ambaye pia ni kiongozi wa vikundi hivyo alipotafutwa azungumzie hilo amesema hayuko sehemu yenye utulivu, hivyo hawezi kuzungumza.
Hata hivyo, Juni 8, 2024, Chonde alisema zaidi ya wiki imepita wakimtafuta mtoto huyo na hakuna walichokibaini na walipanga mikakati mipya ya kuendelea na msako huo.