Malima awaonya watumishi Malinyi, Ifakara kuendeleza misuguano

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima  Mwenye Maikrofoni Nyekundu  akiendesha Kikao maalumi cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Ifakara kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG. Picha na Johnson James

Muktasari:

  • Katika halmashauri za Malinyi na Ifakara, kumebainika kuwapo migogoro baina ya wakurugenzi na madiwani au watumishi wengine, jambo linalosababisha kukwama kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Morogoro. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewataka watumishi wa Halmashauri za Malinyi na Ifakara kufanya kazi kwa ushirikiano, ili kuleta maendeleo kwenye halmashauri zao badala ya kuendeleza misuguano inayokwamisha miradi ya Serikali.

Malima amesema hayo leo Jumatano Juni 26, 2024 wakati wa ziara yake kwenye wilaya hizo, kuendesha vikao vya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Ushirikiano kwenye ufanyaji kazi kwenye wilaya ya Malinyi ni mbaya sana, hamfanyi kazi za Serikali inavyotakiwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwenye maeneo yenu, badala yake kila mtumishi akiletwa hapa anaonekana kaonewa.

“Sasa mimi ndiye mkuu wa mkoa wa Morogoro, ninamwakilisha Rais, kama kuna mtumishi anajiskia hawezi kuishi hapa Malinyi kuwatumikia wananchi, aniandikie barua ya kutaka kuhama, nami nitamhamisha ili tupate mtumishi atakayekuja kufanya kazi kwa maendeleo ya halmashauri hii ya Malinyi,” amesema Malima.

Akizungumzia changamoto ya kutokamilika kwa miradi ya Serikali kwa wakati katika halmashauri ya Ifakara, Malima amesema hatakuwa tayari kuona Ifakara inazama kisa ugomvi wa watumishi.

“Nimepata taarifa mkurugenzi akiagiza jambo lifanyike kwa madiwani halifanyiki, lengo tu mnataka aharibikiwe, sasa tutaanza kushughulika na wao, lakini pia mkurugenzi naye ana mambo yake tutaongea naye, kama hatabadilika tutaomba kuletewa mkurugenzi mwingine.

“Kiu yetu ni kuona ushirikiano miongoni mwa watumishi ukiongezeka na mkifanya kazi kwa pamoja na kuweka kando ugomvi wenu, mnapozozana bila sababu, wananchi ndio wanaumia, hivyo tutaweka jicho letu hapa kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk Mussa Ali Musa, akizungumzia watumishi kwa upande wa halmashauri ya Ifakara, Wilaya ya Kilombero amesema kutofanya kazi kwa ushirikiano, kuzorota kwa miradi ya kimkakati katika halmashauri hiyo kunasababishwa na ushirikiano mbovu uliopo baina ya watendaji.

“Kuna tatizo la kutokamilika kwa miradi ya Serikali hapa Ifakara hadi tunavyozungumza kuna miradi saba haijakamilika na mingine imeshapitwa na wakati, mfano jengo la utawala, nyumba tatu za wakuu wa idara, vyote hivi havijakamilika,” amesema.

Naye mwenyekiti wa halmashauri ya mji Ifakara, Kassim Nakapala amesema watumishi kwenye halmashauri yake watarejea kwenye uchapaji kazi, licha ya changamoto zilizokuwepo.

“Ni kweli tulikuwa na changamoto katika utendaji wa kazi kwenye halmashauri yetu, jambo ambalo lilisababisha kudumaa kwa miradi ambayo tunasimamia, hivyo naamini watumishi wote tumelipokea na tutahakikisha hakuna mkwamo wowote unaotokea kwenye utekelezaji wa kazi za halmashauri,” amesema.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo amemuomba mkuu wa mkoa kuwaita TBA na kuwahoji sababu ya kutokamilika kwa wakati kwa mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi za halmashauri hiyo, licha ya karibu fedha zote kulipwa ambazo ni Sh7.3 bilioni.