Makonda kuomba kibali kuzungumza na wabunge

Muktasari:
- Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema katika kutimiza majukumu yake mapya, anakusudia kukutana na wabunge wanaotokana na chama hicho, ili wamweleze aina ya msemaji wanayemtaka.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema katika kutimiza majukumu yake mapya, anakusudia kukutana na wabunge wanaotokana na chama hicho, ili wamweleze aina ya msemaji wanayemtaka.
Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi Oktoba 26, 2023, katika hafla ya kumpokea iliyofanyika katika ofisi za ndogo za Makao makuu ya chama hicho Lumumba, jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Sophia Mjema.
"Manake mimi naweza kuwa msemaji wa aina yoyote ile, ukitaka mcha Mungu, mnyenyekevu na haki utanipata, ukiwa mcheza rafu, kiburi, mkorofi na dharau utanipata, hapa sifa zote ninazo, ni chaguo lao tu," amesema na kuongeza;
"Nimekusudia kuomba kibali kwa mtendaji wetu, Daniel Chongolo, Katibu Mkuu wa chama chetu, ili nikaongee na wazee wetu...sehemu ambako siasa inapikwa waniambie wanataka msemaji wa aina gani."
Katika hatua nyingine, Makonda ameliomba Jeshi la Polisi nchini kufanya kazi bila kuegemea upande wowote, ikiwa ni pamoja na kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya kisiasa kwa vyama vyote, na hivyo kuondoa dhana iliyozoeleka kuwa chama hicho kinabebwa na jeshi hilo.
"Niliombe Jeshi la Polisi, tuachieni mikutano ya hadhara, tuachieni hao wanaojiita chama cha watoa taarifa, msihangaike nao, kama ni vibali wapeni, kama ulinzi wapeni, safu ya Rais Samia Suluhu Hassan imekamilika," amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuwasogezea wananchi huduma ikiwemo elimu bure hivyo haoni sababu ya kuendelea kushindana na vyama vya siasa kwenye majukwaa ya mikutano ya hadhara inayofanyika maeneo mbalimbali nchini.
"Hoja tunazo, IGP Wambura vibali wapeni tutashindana nao, wala msiwe na wasiwasi, kikubwa watendaji fanyeni kazi na atakayezembea hatutakuwa na mkopo, tutamchukulia hatua hapo hapo," amesema Makonda.
Kufutia kauli zake kwa vyama vya upinzani, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mrema amemkaribisha kwenye ulingo wa siasa akisema katika uwanja huo hakuna mtu wa kumpa maagizo kama alivyokuwa mtendaji serikalini.
"Amekuwa na maneno mengi, tunamkaribisha kwenye ulingo wa siasa, huku tunafanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya vyama vya siasa hakuna mtu wa kumpatia maagizo tunamkaribisha sana," amesema Mrema.