Makardinali wafanya mkutano wa kwanza Vatican

Muktasari:
- Takriban makardinali 60 wamekusanyika asubuhi ya leo Aprili 22, 2025 kuapa kwa katiba kuhusu nafasi iliyoachwa wazi na uchaguzi wa Papa.
Vatican. Mkutano mkuu wa kwanza wa makardinali umeanza asubuhi ya leo Aprili 22, 2025 ikiwa ni siku moja baada ya kifo cha Papa Francis (88).
Kwa mujibu wa mtandao wa Vatican News, mkutano huo ulidumu kwa saa moja na nusu, kuanzia saa 3:00 hadi saa 4:30 (saa za Ulaya).
Imeelezwa waliokuwa katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Sinodi Mpya ni makardinali wapatao 60. Walianza kwa sala kwa ajili ya Papa Francis ambaye mazishi yake yatafanyika Jumamosi Aprili 26, 2025 mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
Taarifa inasema makardinali waliapa kwa kuzingatia uaminifu wa kanuni za Katiba ya Kitume (Universi Dominici Gregis) kuhusu nafasi ya kiti kilicho wazi cha kitume na kuchaguliwa kwa Papa wa Roma, kisha wakaimba wimbo wa kumuomba Roho Mtakatifu awaangazie.
Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya Kitume ilisomwa na Kardinali Joseph Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu Katoliki la Roma, akiwasomea pia waliohudhuria wosia wa Papa Francis uliochapishwa jioni Jumatatu Aprili 21, 2025.
Mkutano wa leo ulitoa uamuzi wa tarehe za uhamisho wa mwili wa Papa Francis na mazishi kama ilivyotangazwa na Ofisi ya Maadhimisho ya Liturujia za Kipapa awali.
Pia umetoa uamuzi wa kusitisha sherehe za kutangazwa mwenyeheri iliyokuwa imepangwa kufanyika hadi hapo patakapotolewa uamuzi wa Papa mpya wa Roma.
Kwa mujibu wa Vatican News, mkutano wa pili wa Baraza la Makardinali utafanyika kesho Aprili 23 saa 11:00 jioni (saa za Ulaya) kwa sababu asubuhi makardinali watashiriki ibada ya kuhamisha mwili wa Papa kutoka kikanisa cha Mtakatifu Marta kupelekwa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.
Misa ya Dominika ya Pili ya Pasaka Aprili 27, 2025 ambayo pia ni ya huruma ya Mungu, itafanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro ikiongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican. Itakuwa misa ya pili kati ya tisa zinazopaswa kwa ajili ya Papa (Novendiali).
Maadhimisho ya misa hizo yatafanyika kila siku saa 11:00 jioni (saa za Ulaya na saa 12:00- saa za Afrika Mashariki na Kati).
Makardinali wa Tume ya kumsaidia Camerlengo wanapigiwa kura katika mkutano huo wa kwanza pia makadinali watatu wa tume inayosaidia Camerlengo kwa uamuzi wa kawaida walipigiwa kura ambao ni makardinali Pietro Parolin, Stanisław Ryłko na Fabio Baggio, mmoja mmoja kwa kila utaratibu ambao baraza linaundwa: ule wa maaskofu, mapadre na mashemasi. Makardinali hao wa tume hiyo wanapigiwa kura kila baada ya siku tatu.