Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makali ya maisha, maumivu kila mahali

Dar/Mikoani. Maumivu kila mahali. Hivi ndivyo unaweza kueleza kile ambacho wananchi wanakipitia kwa sasa kutokana na upatikanaji wa huduma za umeme, maji, joto kali na kupanda kwa gharama za maisha kutokana na bidhaa muhimu bei zake kupaa.

Wananchi katika maeneo tofauti nchini wamekuwa wakipitia adha hizo, huku wakiandamwa na magonjwa ya mlipuko kama vile 'red eyes' ambao umesambaa zaidi ya mikoa 23 Tanzania Bara. Pia, ugonjwa huo umekwisha kufika visiwani Zanzibar.

Mambo hayo yamekuwa yakiwapunguzia ufanisi katika shughuli za maendeleo wanazozifanya.

Kupanda kwa nauli katika vyombo vya usafiri wa umma pamoja na bei ya mafuta ni mambo mengine yanayoongeza hali ngumu ya maisha kwa wananchi, na kuchochea kupanda kwa bei ya vyakula sokoni.

Mambo hayo yameibua malalamiko ya wananchi ambao wanaguswa na wakipambana kila siku katika mazingira hayohayo kuhakikisha maisha yao yanaendelea, licha ya changamoto zinazowakabili.

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inaondoa changamoto hizo kwa kuchukua hatua za haraka.

Mtaalamu wa saikolojia, Ramadhani Masenga alisema tatizo mojawapo linaloweza kusababishwa na mgawo wa umeme, maji, joto na kupanda kwa gharama za maisha ni msongo wa mawazo kwa wananchi.

“Mtu anavyopata msongo wa mawazo athari anayokumbana nayo ni kukosa usingizi, kuharibu mfumo wa kinga ya mwili, kinga ikishaharibika inakuwa rahisi kushambuliwa na magonjwa, hivyo ikifikia hatua hii mtu hawezi kuishi muda mrefu," alisema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa saikolojia, Josephine Tesha alisema mabadiliko yoyote katika maisha ambayo mtu hakuwa na muda mzuri wa kujiandaa ni lazima yaathiri akili.

"Athari hizo zinaweza zisionekane kwa haraka, ila madhara yanakuwa yanajitokeza kidogokidogo kwenye maisha na kusababisha hali ya mifarakano ndani ya familia," alisema.


Licha ya kuathiri shughuli za ujasiriamali na viwanda, kukosekana kwa umeme kumekuwa kero kubwa kipindi hiki cha joto kali ambapo watu wanategemea nishati hiyo kupunguza makali ya hali hiyo.

Mgawo wa umeme nchini ulianza tangu Septemba mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa ni kupungua kwa uwezo wa uzalishaji wa nishati hiyo kwenye mabwawa ya kufua umeme kulikosababishwa na vyanzo mbalimbali kukosa maji.

Mfanyabiashara wa kuku, Bernard Chuwa kutoka Mbezi, Dar es Salaam alisema amepata hasara ya Sh800,000 kutokana na mzigo wake wa kuku kuharibika.

“Niliweka kuku kwenye jokofu usiku, usiku umeme ukakatika, asubuhi nilikuta kuku wote wameharibika,” alisema.

Msemaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Kenneth Boymanda alisema sababu ya kutokea kwa mabadiliko ya ratiba ya mgawo wa umeme ni upungufu kuongezeka.

“Sasa ni kitu gani kinatokea, ukitengeneza makisio ya ratiba ikitokea wakati wa utekelezaji moja ya mashine ya kuzalisha umeme ikipata hitilafu maana yake upungufu utaongezeka,” alisema.

Alisema mambo muhimu wanayozingatia kwenye utengenezaji wa ratiba ya mgawo ni makisio ya uzalishaji wa umeme kulingana na mahitaji ya wateja.

Boymanda alifafanua lengo la mgawo ni kuhakikisha kiwango kidogo cha umeme kinachozalishwa kinagawanywa kwa wananchi wote.


Mgawo wa maji nao ni miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo wananchi kwa sasa, jijini Dar es Salaam baadhi ya wananchi hawapati huduma hiyo maeneo mengine hadi mwezi mmoja, hivyo wananunua dumu la lita 20 kwa Sh700.

Tatizo hili linatajwa kuwa mfupa mgumu kutokana na kujirudia rudia kila nyakati na hakuna suluhisho la kudumu.

Mkazi wa Mburahati, Salma Hassan alisema maji yametoka mara tatu tangu mwaka huu uanze na wamekuwa wakiuziwa dumu moja la lita 20 kwa Sh700.

“Wakati mwingine kuna gari la maji safi linapita wanatuuzia ndoo Sh300 hadi Sh400 na ukichelewa hupati,"alisema.

Mgina Mdeme, mkazi wa Kimara Baruti alisema mwezi mzima hawapati maji, walifanya mawasiliano na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) bila mafanikio ya kutatuliwa changamoto hiyo.

“Nimefuatilia Dawasa wananipiga danadana, mara maji hayatoshi, pampu ni ndogo, ukiwatafuta tena wanakuambia tatizo limeshatatuliwa,” alisema.

Akizungumzia tatizo la maji Dar es Salaam kwenye mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) juzi, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu alisema changamoto ya ukosefu wa maji ya uhakika inatokana na kuharibika kwa miundombinu.


Kipindi hiki, Watanzania katika mikoa zaidi ya 10 tofauti wanashuhudia joto kali lisilo la kawaida. Wengi wanatumia mbinu tofauti za kujipatia nafuu, ikiwemo kutumia viyoyozi, feni au maji.

Mtaalamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Rose Senyengwa alisema mikoa 14 imekuwa na ongezeko la joto ikiongozwa na Mkoa wa Kilimanjaro, ambayo imefikia nyuzi joto 35.

Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro, Visiwa vya Unguja na Pemba, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Shinyanga, Simiyu na Tabora kiwango cha joto ni nyuzi 34. “Kwa kawaida kipindi cha Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia, Tanzania ni nchi mojawapo huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine,” alisema.

James Thobias (70), mkazi wa Msaranga mkoani Kilimanjaro alisema, “hatujawahi kushuhudia joto la namna hii tangu enzi na enzi, mpaka uzee wangu huu hakuna wakati ambao tulishawahi kupata mateso ya namna hii, nasema haya ni mateso kwa kuwa sio mchana wala usiku, hali ni mbaya sana,” alisema.

Hata hivyo, mtaalamu mshauri wa afya, Festo Ngadaya alisema ni muhimu wananchi kunywa maji ya kutosha kulingana na mahitaji ya mwili.

Balozi wa mazingira nchini na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya maendeleo na mazingira Kilimanjaro (KCDE), Aidan Msafiri alisema sababu za ongezo la joto katika mkoa huo ni kupotea kwa uoto wa asili ambao umeharibiwa na shughuli za kibinadamu.

Vyakula, nauli bei juu

Mbali na umeme, maji na joto yanayowaandama wananchi, maumivu mengine ni kupanda kwa gharama za maisha kutokana na bei za baadhi ya bidhaa muhimu kupanda, mathalani sukari, viazi mbatata, vitunguu, pilipili hoho na kabichi.

Kupaa kwa bei ya bidhaa hizo kunazidisha hofu kwa waumini wa dini ya Kiislamu ambao Machi 10 au 11 mwaka huu wanatarajia kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Pia, waumini wa Kikristo wako kwenye mfungo wa Kwaresima.

Kwa mujibu wa wakazi wa baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam waliozungumza na Mwananchi, kilo moja ya sukari inauzwa kati ya Sh4,500 hadi Sh5,000, huko Arusha hali ikiwa mbaya zaidi, kilo moja ya bidhaa hiyo inapatikana kwa Sh5,000 hadi Sh6,000 sawa na mikoa ya Mtwara, Lindi, Mbeya, Mwanza na Kigoma.

Bei hizo za sukari zinaendelea kipindi ambacho zimepita takriban wiki mbili tangu Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), itangaze bei elekezi ya kuanzia Sh2,800 na isizidi Sh3,200

Kwa upande wa vitunguu maji, gunia moja lililokuwa linauzwa kwa Sh250,000 hadi Sh300,000 kwa sasa linapatikana kwa Sh500,000 hadi Sh550,000 katika Soko la Mabibo, jijini hapa.

Maumivu yanaendelea kwenye usafiri, ambapo mwaka jana Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilieleza daladala zilizokuwa zinatoza Sh1,000 (umbali wa kilomita 31 hadi 35) bei itapanda hadi Sh1,300 na zile zenye ruti ambazo umbali wake ni kati ya kilomita 36 hadi 40, nauli imepanda kutoka Sh1,100 hadi Sh1,400.

Pia, kwa daladala zenye ruti isiyozidi kilomita 10 imepanda kutoka Sh500 hadi Sh600, ruti ya kilomita 11 hadi 15 nauli imeongezeka kutoka Sh550 hadi Sh700 na ruti ya kilomita 16 hadi 20 nauli imeongezeka kutoka Sh600 hadi Sh800.