Maji Bwawa la Nyerere yafikia mita 136, uzalishaji umeme kuanza Jan 2024

Muktasari:
- Kina cha Maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) kimefikia mita 136.3 kutoka mita 71, Desemba 22, 2022 ulipofanyika uzinduzi na Rais Samia Suluhu Hassan. Ili uzalishaji uweze kufanyika kina kinapaswa kufikia mita 163 ikiwa ni takribani mita 27 zimesalia.
Morogoro. Kina cha maji katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) umefikia 136.3 kati ya mita 163 kinachopazwa kufikiwa ili kuanza uzalishaji.
Ujazaji maji kwenye Bwawa hilo litakalozalisha megawati 2115, ulianza Desemba 22, 2022 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua.
Hadi kufikia juzi, ujazo wa maji umefikiamita 136.3 kutoka mita 71.5, Desemba 22 mwaka jana wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipozindua rasmi ujazwaji maji katika Bwawa hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalishaji Megawati 2,115.
Jana Jumamosi, Machi 11,2023, timu ya Bodi ya Maji Bonde la Rufiji na waandishi wa habari walifika kujionea hali ya mradi unavyoendelea.
Mhandisi Mkazi wa Mradi wa JNHPP, Rutengano Mwandambo alisema hadi kufikia mwishoni mwa Februari 2022 mradi kwa ujumla ulikuwa umefikia asilimia 83.
"Mtakumbuka Rais Samia alizindua ujazaji maji Desemva 2022 mwaka jana na hadi kufikia leo (jana) maji yamefikia mita za ujazo 136.3 kutoka usawa wa bahari," alisema
Mhandisi Mwandambo alisema ili uzalishaji uweze kufanyika lazima maji yafikie mita 163.
Kwa maana hiyo kwa sasa zimebaki mita takaribini 27 na yeye (Mwandambo) alisema,"kwa hali ilivyo hana shaka maji yatajitoshereza."
Alisema matarajio yao hadi kufikia Agosti mwaka huu,"tutakuwa tumemaliza kufunga mtambo wa kwanza. Wa pili utakuwa Oktoba na wa tatu Novemba au Desemba na uzalishaji wa kwanza wa majaribio Januari mwakani kwa mujibu wa ratiba."
Timu hiyo ya Bonde la Rufiji na waandishi wa habari walitembelezwa maeneo mbalimbali na kujionea jinsi maji yalivyojaa na kuanza tengeneza bahar na au ziwa na ufungaji wa mashine na shughuli zingine zikiendelea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bonde la Rufiji, Mhandisi Mhandisi Florence Mahay alisema ili bwawa hilo liweze kujaa lazima wasimamie na kuratibu shughuli za maji kwa sekta zote kutoka vyanzo vya maji na mito wanayoisimamia.
Mhandisi Mahay alisema ili hilo lifanikiwe,"ni kuhakikisha sheria ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji haviharibiwi kwa shughuli za kibinadamu na wamekuwa wakiendelea kushirikiana na jumuiya za watumiaji maji ili kuwadhibiti waharibifu."
Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wakulima, wafugaji na wananchi kwa ujumla kuwa walinzi wa vyanzo vya maji kwani kuviharibu kwa ubinafsi kuna athari kwa watu wengi.
Pia, alibainisha mkakati wa kuajiri vijana 50 waliopata mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) watakaokuwa na jukumu la kuvilinda vyanzo vyote vya maji kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Alisema timu hiyo maalum ya watu 50 waliopata mafunzoJKT,"tutawaajiri kwa kushirikiana na Tanesco ili kuhakikisha tunavilinda vyanzo vya maji dhidi ya waharibifu."
"Sisi Bonde la Rufiji ambao ndio tegemeo la maji la Bwawa la Nyerere, tuwahakikishie Watanzania, litajaa kwa wakati na waharibifu wa vyanzo vya maji wanachukulia hatua," alisema
Naye Profesa Japhet Kashaigili wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) ambaye amekuwa akifanya tafiti mbalimbali za uhifadhi wa mazingira na rasilimali za maji alisema kuna athari nyingi zinazababishwa na shughuli za kibinadamu kama Kilimo, uchomaji wa misiti na kilimo cha kuhamahama.
"Cha msingi, kwa mradi huu mkubwa wa Bwawa, inahitaji kila mmoja kuvilinda vyanzo vya maji na kama tukiweza kupunguza basi tutakuwa tumefanikiwa kwa sehemu kubwa," aliswma Profesa Kashaigili