Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa: Mikopo ya asilimia 10 ianze kutolewa Januari 2024

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amefungua Wiki ya Huduma ya Fedha Kitaifa, jijini Arusha na kutoa maagizo kwa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Fedha kumaliza mchakato wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 uliokuwa umesitishwa na Serikali.

Arusha. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassimu Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Fedha kukamilisha utaratibu wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 uliokuwa umesimamishwa na Serikali na kuhakikisha unakamilika ifikapo Januari 15, 2024.

Pia, amewaagiza watoa huduma za kifedha nchini kuimarisha mifumo ya ukopeshaji kwa kutokuweka vipengele vya mitego kwenye masharti ya mikopo na wananchi wanapaswa kuelewa taratibu kabla hawajakopeshwa.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maelekezo hayo leo Jumatano, Novemba 22, 2023 jijini hapa  alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya wiki ya huduma za kifedha yanayofanyika katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid.

Serikali ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa makundi maalumu ya wanawake, vijana na wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa mgawanyo wa asilimia 4 kwa vijana, asilimia 4 kwa wanawake na asilimia 2 kwa wenye ulemavu.

Aprili 13, 2023, Majaliwa wakati akiwasilisha hotuba ya kuahirisha shughuli za Bunge, alitangaza uamuzi wa Serikali kusitisha utoaji mikopo hiyo hadi utaratibu mwingine utakapoelekezwa.

Uamuzi huo uliungana na kauli aliyoitoa mapema Rais Samia Suluhu Hassan aliposema unaandaliwa utaratibu mzuri wa ukopeshaji wa fedha hizo kupitia benki, ili kuwasaidia zaidi wahitaji.

Serikali ilifanya uamuzi huo kufuatia kelele nyingi za wabunge kuhusu namna ya ukopeshaji mikopo hiyo  ikiwamo Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambao walisema fedha hizo zinaliwa na wajanja, hivyo kukosa mwendelezo wake.

LAAC walikuwa wanajikita katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyebainisha kasoro hususani za ukopeshaji kwa vikundi hewa pamoja na mamilioni ya fedha kuwa hatarini kutorejeshwa.

Majaliwa amesema mchakato wa kuangalia utaratibu mpya wa utoaji mikopo hiyo unapaswa kukamilishwa ili Januari 2024 halmashauri zote nchini ziruhusiwe kuendelea kutolewa na wajasiriamali waendelee kunufaika.

 “Japokuwa tulistitisha mikopo ile Aprili, kwa hiyo fedha yote kuanzia mwezi huo  hadi sasa ipo, naamini kila halmashauri ina mabilioni ya kutosha kukopa, watu wetu waende,” amesema Majaliwa.

Vilevile, ameziagiza halmashauri kuhakikisha zinaendelea kuratibu vikundi vya wajasiriamali ikiwemo vya wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na kuwatafutia soko, kubuni maonyesho ndani ya wilaya na mikoa ili waweze kutangaza biashara zao.

Kuhusu taasisi za fedha, amesema ni wakati wa kuongeza ubunifu na huduma wanazotoa ziendane na soko, kuangalia makundi mbalimbali na kuwaunganisha wajasiriamali na fursa za fedha.

“Imarisheni mifumo yenu jengeni uelewa wa kutosha kwa wananchi kabla ya kuingia nao mikataba, waelewesheni mambo muhimu anayopaswa kuelewa, msiweke vipengele vya mitego ili mkopaji apate madhara kila mmoja anawajibika kumwelewesha mwenzake ili aweze kufanikiwa,” amesema.

Kuhusu matumizi ya huduma rasmi za kifedha, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Fedha ina wajibu wa kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kutumia mifumo rasmi ya fedha badala ya kutumia mifumo isiyo rasmi, pamoja na taasisi za fedha ikiwemo benki kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma za kifedha.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema masuala ya fedha yanahitaji nidhamu na Watanzania wengi wakipewa mkopo, lile jambo waliloombea hawalitekelezi, wanafanya mambo mengine.

Amesema baadhi ya taasisi za benki pamoja na kazi nzuri  wanazofanya lakini inapofika mteja wao analegalega  jukumu la kulea wanalikosa, unakuta mtu ameshalipa robo tatu ya kile anachodaiwa amekwama moja ya nne, wanachukua dhamana yake ambayo ni kubwa kuliko kilichobaki katika mkopo anaodaiwa, hili ni jambo  linaloharibu kazi yote  nzuri iliyofanyika.

“Elimu ya masuala ya kifedha ni mambo ya msingi sana, Taifa letu linajali undugu, kwa hiyo mambo mengi tunafanya kwa kuaminiana. Ndugu zangu Watanzania niwaambieni, masuala ya kifedha yanahitaji kumbukumbu rasmi na nidhamu ya hali ya juu sana.

“Wengine akishapewa uhakika maombi yake ya mkopo yamekubaliwa, anachukua karatasi anasaini kwenye jina lake tu anasubiri mkopo hata waliosoma hawasomi masharti ya mikopo yaliyopo,” amesema Dk Mwigulu.

Ameongeza: “Wengi wao wanaandika jina wanasaini, wakati wa kudaiwa anaanza kuwaona waliomkopesha ni wabaya lakini kimsingi alipohakikishwa mkopo hakujadiliana nao kuhusu masharti yake, wenzetu waliosoma sheria wanatuelekeza mambo yanayohusu mkataba, pitia kila sentensi neno kwa neno.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema kwa mujibu wa utafiti wa Finscope 2023, Arusha ni miongoni mwa mikoa mitano inayofanya vizuri katika sekta ya fedha. Amesema utafiti huo unaonyesha  upatikanaji  wa huduma jumuishi za fedha umeongezeka kufikia asilimia 82.2 mwaka 2023 kutoka asilimia 74 mwaka 2017.

“Katika kipindi hicho upatikanaji na utumiaji wa huduma jumuishi za fedha katika sekta ya benki umeongezeka hadi kufikia asilimia 34 kutoka asilimia 29, huduma jumuishi za fedha katika sekta ndogo za bima, masoko ya mitaji na dhamana, hifadhi ya jamii na huduma ndogo za fedha uliongezeka kufikia asilimia 48 kutoka asilimia 45,” alisema.

Mongela alitaja changamoto kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya fedha miongoni mwa wananchi na watoa huduma ndogo za fedha hususani daraja  la pili kutokuwa na uwazi katika utoaji wa mikopo, hivyo kusabaisha wananchi wa mkoani hapa kukabiliwa na changamopto ya mikopo umiza au kausha damu.