Majaliwa azionya asasi zinazotoa elimu ya mpiga kura

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akigusa kishikwambi kuzindua uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura. Uzinduzi huo umefanyika Uwanja wa Kawawa Manispaa ya Kigoma Ujiji leo Julai 20, 2024. Picha na INEC
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa lengo la tume ni kupata zaidi ya wapiga kura 34.7 milioni, baada ya kukamilika mchakato wa uboreshaji na uandikishwaji wa Watanzania kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Mwanza. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezionya taasisi na asasi za kiraia 157 zilizopewa kibali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) cha kutoa elimu ya mpiga kura, kujihusisha na majukumu ambayo hayapo kwenye miongozo na makubaliano kati yao na Serikali.
Akizungumza leo Jumamosi Julai 20, 2024 katika uwanja wa Kawawa Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma wakati wa uzinduzi wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Majaliwa amesema pamoja na asasi hizo kupewa vibali, zinapaswa kutambua uwepo wa sheria nyingine za nchi wanapotekeleza majukumu yao.
“Unafanya mambo ya ovyo...unasema mimi nina kibali, kiballi hiki hapa...ninayo haki hapana! Lazima mjue nchi hii ina sheria na tunapoendesha zoezi hili pamoja na sheria yake lakini tuna sheria nyingine za nchi ambazo zinaenda pamoja kwa hiyo tekelezeni masharti hayo,’’ amesema na kuongeza:
‘’Ni vyema wakati wote muepuke masuala ambayo hayapo kwenye miongozo ambayo mmepewa na hayapo kwenye vibali mliivyopewa...Tunataka zoezi hili likamilishwe kama lilivyokusudiwa.’’
Amesema hata taasisi na asasi hizo zikitaka kuelimisha wananchi kwenye vyumba vya mikutano au mikutano ya hadhara, wazungumzie kuhusu uchaguzi tu siyo kuingiza vitu alivyoviita havikubaliki kwenye maeneo hayo.
Mbali na INEC kuruhusu asasi hizo kutoa elimu lakini pia asasi za kiraia na taasisi 33 za ndani ya nchi na nane za nje ya nchi, zimepewa kibali cha uangalizi wa uandikishaji na kutazama uendeshaji wa zoezi la uboreshaji wa daftari hilo.
Katika hatua nyingine, Majaliwa ameliagiza Jeshii la Magereza na vyuo vya mafunzo Zanzibar kuweka miundombinu wezeshi kuwarahisishia INEC kutekeleza majukumu yao kiufanisi inapokwenda kuandikisha na kuboresha taarifa za wafungwa wanaotumikia vifungo chini ya miezi sita.
“Jeshi la Uhamiaji mtawajibika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuwatambua na kutoa taarifa za uwepo wa watu ambao siyo raia wa Tanzania na mtawajibika kutembelea kwenye vituo hivi mara kwa mara wakati wa zoezi la uandikishaji kujiridhisha kama pale hakuna taarifa ya raia wa kigeni kujiandikisha kwenye daftari hilo, kwa kufanya hivyo mnaweza kushirikiana vizuri na wananchi katika kutambua wale wote ambao hawana sifa hasa ya Utanzania,”amesema Majaliwa.
Pia ameliagiza Jeshi la Polisi kutotumia matumizi makubwa ya nguvu wakati wa kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yote uandikishaji utakapofanyika.
Majaliwa ameitaka INEC kuwajibika na kuchukua hatua za haraka kuwaondoa watendaji watakaobainika kwenda kinyume na maadili ya jukumu hilo, akidai wapo wachache ambao hawataki kufuata utaratibu.
“Wamejiona wamefika mahali hapo na kwamba hakuna mwingine yeyote yule halafu wanaanza kufanya mambo ambayo hayakubaliki,’’ ameeleza.
Pamoja na kuvitaka vyama vya upinzani kuhamasisha wananchi kwenda kuboresha taarifa zao na kujiandikisha kwenye daftari hilo, Majaliwa amesema vinayo fursa kisheria kuweka mawakala wao wakati wa uandikishaji kwenye kila kituo cha uandikishaji chini ya kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba moja ya mwaka 2024.
Amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha mawakala hao watakaowaweka kwenye vituo hivyo, wawe wenyeji kwenye eneo daftari linapoandikishwa ili watambue wenye sifa ya kuandikishwa na kupiga kura.
Awali, akitoa taarifa kwa Majaliwa, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema tume hiyo ina wajibu wa kuboresha daftari la wapiga kura mara mbili katika kipindi kinachoanza baada ya uchaguzi mkuu mmoja na kabla ya siku ya uteuzi wa uchaguzi mkuu unaofuata.
“Mara ya mwisho tume kuboresha daftari ilikuwa 2019/20 hivyo uzinduzi utakaofanyika ni uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya kwanza inayoanza leo Julai 20,2024 na kukamilika Machi, 2025 ili kutoa nafasi kwa uboreshaji wa awamu ya pili,”amesema.
Jaji Mwambegele amesema uboreshaji huo utafanyika katika mizunguko 13, wa kwanza ukianza leo na kuhusisha mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi ambapo kila mzunguko utadumu kwa siku saba na vituo vya kuandikisha vitafunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12: 00 jioni.
Amesema Zanzibar zoezi hilo litafanyika kuanzia Oktoba 7 hadi 13, 2024 na kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13 (1)(2) cha sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani sheria namba moja ya mwaka 2024.
Amesema uboreshaji wa daftari utamruhusu mtu yeyote aliyepo Zanzibar ambaye hana sifa za kuandikishwa na tume ya uchaguzi Zanzibar lakini anayo sifa ya kumchagua Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema jumla ya vituo 40,126 vitatumika kwenye uboreshaji wa daftari kati ya hivyo, 39, 709 vipo Tanzania bara na vituo 417 vipo Zanzibar vikiwa ni ongezeko la vituo 2,312.
Kwa mujibu wa takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, wanatarajia kuandikisha zaidi ya wapiga kura 5.5 milioni ambao wametimiza umri wa miaka 18 na ambao watafika umri huo kabla au ifikapo siku ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Amesema maandalizi yote muhimu kuhusiana na uboreshaji wa daftari hilo yamekamilika ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya uandikishaji (BvR Kits) 6,000 vinavyotumia mfumo wa programu endeshi ya android.