Majaliwa atoa maagizo kulinda zao la mkonge

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya kilimo pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano kuharakisha mchakato wa kutunga kanuni za kudhibiti matumizi ya kamba za plastiki.

Tanga. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza wizara ya kilimo pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano kuharakisha mchakato wa kutunga kanuni za kudhibiti matumizi ya kamba za plastiki.

Amesema mchakato huo utaiwezesha Serikali kupiga marufuku uagizaji wa magunia na kamba za plastiki kutoka nje ili kutoa fursa kwa viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa hizo kwa malighafi ya mkonge kupata soko bila bughudha.

Ametoa agizo hilo leo Jumapili, Desemba 04, 2022 katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde wakati akifungua mkutano wa tatu wa wadau wa mkonge uliofanyika jijini Tanga.

Amesema miongoni mwa kilio cha wakulima na wazalishaji bidhaa za mkonge Tanzania ni ukosefu wa soko la ndani jambo linalosababisha kamba na magunia yanayozalishwa kurundikana kwenye maghala kutokana na magunia na kamba za plastiki kutoka nje kuteka soko lao.

"Nimejulishwa magunia na kamba zinazozalishwa na viwanda vyetu vya mkonge yanatosheleza soko la ndani, wizara zikiharakisha kutunga kanuni tutaweza kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje kwa sababu mbali ya kuharibu mazingira pia zinaharibu mnyororo mzima wa kilimo cha mkonge" amesema Majaliwa.


Kuhusu changamoto ya mikopo kwa wakulima wa mkonge, amesema Serikali imeshaifanyia kazi kwa kuiagiza benki kuu kuziwekea mazingira benki za biashara kupunguza riba kwa wakulima.

Amewapongeza wakulima wa mkonge Tanzania kwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 36,379 mwaka 2010 hadi kufukia tani 43,594 mwaka 2021/22.

Mwenyekiti wa bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Mariam Mkumbi amesema miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya mkonge ni uvamizi wa mashamba ya zao hilo,wakulima wadogo kukosa mitaji ya kutosha na uhaba wa zana za kuzalishia.